Na: Stella Kessy, DAR ES SALAAM.
KIKOSI cha timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, kesho kitashuka dimbani kucheza mchezo wa pili wa kutafuta nafasi ya kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Madagascar mtanange utakaopigwa kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Kim Poulsen , amesema kuwa utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Madagascar, ambao timu yao imekaa pamoja kwa muda mrefu hivyo anatarajia ushindani mkubwa.
“Katika mazoezi ya mwisho tuliyofanya wachezaji wote wako vizuri hatuna majeruhi yoyote ila tunapaswa kucheza kwa nguvu ili tuweze kupata matokeo
“Lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa kufanya mabadiriko ya wachezaji kutokana na aina ya wapinzani wetu, nimefurahi kumuona Samata ni mchezaji mzuri anayecheza soka la kulipwa ulaya nitaangalia kama ninaweza kumtumia ” amesema Poulsen.
Naye nahodha wa Taifa Stars, Erasto Nyoni, amesema kuwa wachezaji wote wako fiti hakuna mwenye majeruhi kilichobaki ni maombi ya watanzania ili kuhakikisha tunashinda mchezo huu.
“Tumejiandaa vizuri tunajua Madagascar wana timu nzuri wana wachezaji wengi wanaocheza ulaya, tumejipanga kuhakikisha tunashinda kila mchezo,Kama timu tumejipanga kuhakikisha tunakusanya pointi zote tisa katika uwanja wa nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri,” alisema Nyoni.