Home LOCAL SERIKALI YAAHIDI KUSIMAMIA KIKAMILIFU MKOPO NAFUU WA SHILINGI TRILIONI 1.3 ULIOTOLEWA NA...

SERIKALI YAAHIDI KUSIMAMIA KIKAMILIFU MKOPO NAFUU WA SHILINGI TRILIONI 1.3 ULIOTOLEWA NA IMF KUKABILIANA NA ATHARI ZA UVIKO -19

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Jens Reinke wakati wa mkutano kuhusu fedha zilizotolewa na IMF kwa Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar, jijini Dodoma.
 

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambapo shirika hilo limetoa kiasi cha sh. trilioni 1.3 ambazo zitatumika kwa Tanzania Bara na Zanzibar, jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu fedha zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) ambapo shirika hilo limetoka kiasi cha sh. trilioni 1.3 ambazo zitatumika kupambana na athari za Uviko-19kwa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, jijini Dodoma.


Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Jens Reinke, akieleza kwa Wanahabari kuhusu fedha zilizotolewa na IFM kwa Tanzania ambapo alisema kuwa kiasi cha sh. trilioni 1.3 kilichotolewa na Taasisi yake kitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi wake..

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambapo shirika hilo limetoa kiasi cha sh. trilioni 1.3 zitakazotumika kwa Tanzania Bara na Zanzibar, jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, na kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Jens Reinke.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WFM – Dodoma)

Na: Ramadhani Kissimba, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewahakikishia Wanzania kuwa Mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 567.3 sawa na shilingi trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kukabiliana na athari za Uviko-19 zitasimamiwa kikamilifu ili kuleta tija iliyokusudiwa.

Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma, Dkt. Nchemba alisema kuwa kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 189.1 ni mkopo nafuu usio na riba ambao umetolewa kupitia dirisha la Rapid credit Facility (RCF), na dola za Marekani milioni 378.2 ni mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument (RFI),” alisema Dk. Nchemba.

Aliongeza kuwa fedha hizo tayari zimepokelewa nchini na zitatumika ndani ya mwaka wa fedha 2021/21 katika sekta zilizoathiriwa na UVIKO – 19 ambazo ni  afya, elimu, utalii, maji, pamoja na kusaidia kaya masikini kupitia mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Aidha Dk. Nchemba alisema kuwa ili kupambana na ugonjwa huu ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi Serikali itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa hasa katika kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, wagonjwa hospitalini na kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali hapa nchini.

‘’Fedha hizi zitatumika katika kujenga madarasa au kujenga shule mpya ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani na kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO -19, aidha pesa hizi zitatumika katika kuongeza upatikanaji wa mitungi ya hewa ya oksijeni hasa katika hospitali zilizo pembezoni mwa mji ili kuweza kuokoa maisha ya Watanzania’’, alisema Dk.Nchemba.

Pia Dk. Nchemba amezitaka sekta zote zitakazopata fedha hizo kuhakikisha kuwa zinatumika kwa kuzingatia makubaliano kati ya Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kulingana na mpango uliondaliwa kwa pamoja na sekta husika wa kukabiliana na athari za UVIKO-19.

Kwa upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, alilishukuru Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kuipatia Tanzania mkopo huo ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepatiwa dola milioni 100 ambazo zimeelekezwa kutumika katika sekta mtambuka zilizoathirika na UVIKO -19 hasa katika sekta ya Utalii.  

Mhe. Ali alisema kuwa pamoja na sekta zingine kuathirika na janga la UVIKO – 19, Zanzibar imeathirika zaidi katika sekta ya Utalii ikizingatiwa kuwa utalii ndio kitovu cha uchumi wa visiwa hivyo.

“Zanzibar ilikuwa inapokea watalii takribani 567,000, lakini kutokana na janga la UVIKO – 19, kwa mwaka jana pekee imepokea watalii chini la 100,000, hivyo upatikanaji wa fedha hizo utasaidia sekta hizo ili kuweza kukuza uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema Mhe. Ali.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Jens Reinke alisema shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini ili kupambana na maambukizi ya UVIKO -19 na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Bw. Reinke aliongeza kuwa ofisi yake ipo tayari kufanya kazi na wadau wote wakiwemo waandishi wa habari kwa ajili ya utoaji wa taarifa zitakazo saidia kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii ukiwemo UVIKO-19 pamoja na kupambana na umasikini.

Aliahidi kuwa Taasisi yake inaendelea na majadiliano mengine na Tanzania kwa ajuili ya kuiwezesha Zaidi kifedha kwa ajili ya kujenga uchumi wake pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambao umeathirini uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here