Na.WAMJW-DSM,Dar es Salaam.
Serikali imeagiza kuandaliwa kwa kadi maalum {Performance Scorecard} itakayotumika kufuatilia uwazi na uwajibikaji kila ngazi inayohusika na usimamizi wa masuala ya mnyororo wa ugavi wa dawa hadi kwa mtumiaji wa mwisho {mteja}, katika ngazi ya kituo cha afya.
Serikali imeagiza kuandaliwa kwa kadi maalum {Performance Scorecard} itakayotumika kufuatilia uwazi na uwajibikaji kila ngazi inayohusika na usimamizi wa masuala ya mnyororo wa ugavi wa dawa hadi kwa mtumiaji wa mwisho {mteja}, katika ngazi ya kituo cha afya.
Agizo hilo limetolewa leo Jiji ni Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao na wataalamu na wadau wa masuala ya mnyororo wa ugavi wa dawa.
Dkt. Gwajima amesema, ni kweli wataalamu na wadau hao kwa pamoja wameisaidia nchi kutengeneza miongozo mingi mbalimbali ya masuala ya usimamizi wa dawa lakini inashangaza kwamba bado wananchi wana kilio cha ukosefu wa dawa.
“Miongozo iliyotengenezwa inatosha kwa sasa na mifumo iliyopo inawasiliana na wataalamu wanaweza kutambua ufuatiliaji wa dawa kwenye mfumo wa dawa kuanzia ngazi ya Taifa hadi vituoni.
Ameongeza kuwa Wadau hao wameendelea kufanyia kazi na hata kuishauri Serikali kuongeza bajeti ya dawa, sasa mmeshauri pia MSD isitegemee bajeti ya vituo badala yake ipewe bajeti yake ili ijitegemee, Serikali ni sikivu na inafuatilia. “Mmefanya vitu vingi upande wa miongozo, juzi tu mmetueleza tutumie dawa gani nchini zinazotufaa kwa mazingira yetu na ambazo zinadumu, tukazindua mwongozo wa matibabu.” amewaeleza wataalamu hao.
“Ipo pia miongozo mingine mbalimbali ukiwamo ule wa kupima viashiria vya utendaji kazi katika mfumo wa ugavi na ule wa kufuatilia mauzo ya dawa na fedha zitokanazo na mapato hayo {faida} zitumikaje.Mmefanya kazi nzuri”.
Dkt.Gwajima aliendelea kusema kuwa Serikali haina shida na hilo,kwani wameshashafanya vikao mbalimbali na wakati wote, fedha nyingi zimekuwa zikitumika kuboresha huduma za afya. “Lakini pamoja na haya yote yaliyofanyika, bado tuna changamoto ambazo na ninyi ni mashahidi, bado wananchi wanalalamika hamna dawa. Tulienda Halmashauri ya Same, nikaingia ‘stoo’ ya dawa nikaziona zipo, nikaenda kwenye kikao, kuongea na wananchi, wakasema hatupati dawa.
“Sasa unahusianisha vipi, {tunasema} dawa muhimu zipo asilimia 95, wananchi wanasema hawapati dawa, hapa ndipo kwenye mtihani, miongozo tumeitengeneza, lakini wananchi wanasema hamna dawa, wakati huo huo kuna kituo A dawa zinaharibika na huku kituo B kina uhitaji. Tunafanyaje?,” amehoji.
Dk. Gwajima amesema Serikali inazidi kufanya mabadiliko makubwa ili kuimarisha mifumo yake ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ikiwamo ujenzi wa viwanda mbalimbali.
“Katika ngazi ya kitaifa kuna mabadiliko makubwa, Makambako, Njombe tuna kiwanda kitazalisha dawa aina mbalimbali, tunaanza na gloves, vidonge vya kunywa, maji, na ‘antibiotik’, kwa hizo aina tano tu za bidhaa tutaokoa bilioni 33,” amesema. Ameongeza “Hivyo wananchi wanataka uwazi, ukweli na wenyewe wawe sehemu ya kuona kinachoendelea… mtengeneze ‘tracking tool’ inayoonesha {dawa} zilitoka zikafika huko, kama bidhaa zilitoka kwa mgonjwa, kuna cheti cha daktari ziwe zipo na ushahidi kwamba alipata fulani.
“Kama tulienda kununua nje ya MSD tulinunua kwa thamani ya makubaliano yaleyale au kuna mmoja wetu alipotoka akaenda kununua nje ya makubaliano iwe kwenye kadi maalum ya ufuatiliaji. “Mniambie kama mtu alienda kununua nje ya MSD, kuna utaratibu au anaelekeza vinginevyo naye aingie kwenye ‘perfomance score card’ kwamba hakuwajibika, kamati ya dawa nayo ifanye kazi yake, tuone.
Ameongeza “Bidhaa zinapitwa na wakati tujue, asilimia ngapi inapitwa na wakati, tunakuwaje na bidhaa zilizoisha muda na wadau wapo, mahitaji yapo, maana yake ufuatiliaji na tathmini hapa hatujawekeza vizuri pamoja na miongozo yote tuliyonayo.
“Kuna watu wanawaelekeza wagonjwa kwenye maduka kule, kumbe ni ya akina Gwajima, lazima ioneshwe kwenye ‘perfomance score card’ tujue wangapi amewaelekeza kule, TAMISEMI nao wapo hapa waelewe maana wana vituo zaidi ya asilimia 70 tunaenda kwenye ‘perfomance score card’ kama ilivyo kwenye ajenda ya lishe na malaria.” amesisitiza.
Naye,Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema kikao hicho ni matokeo ya kikao cha awali ambacho, kiliainisha maeneo 16 ya mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya ambayo yalionesha thamani na upotevu wa fedha uliotokea. Tanzania ina viwanda vipya zaidi ya 18, vingi vipo katika hatua za majaribio kwenye uzalishaji wa bidhaa na bado kuna wawekezaji wengi wanaokuja nchini kuwekeza.
Akitolea mfano amesema katika Mkoani wa Pwani kipo kiwanda cha majitiba {drip} ambacho nacho tayari kimeanza kufanya majaribio na kwamba mapema kesho Waziri Gwajima anatarajiwa kuzindua kiwanda cha barakoa kilichosimikwa huko Kigamboni. “Kwa hiyo viwanda vipo mbalimbali lengo letu kufikia mwaka 2030 Tanzania inakusudia kuwa na uwezo wa kupunguza kiwango cha dawa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kuwa zinatengenezwa ndani ya nchi, kutoka asilimia 88 hadi 50.
“Kwa kasi ya Serikali ya awamu ya sita, {Tanzania} itaweza kufikia lengo hilo la kuzalisha zaidi ya asilimia 50 ya dawa ndani ya nchi,” amebainisha Msasi na kusisitiza kwamba kikao hicho kitajadili kwa kina yote yaliyoagizwa na Waziri Gwajima.