Home BUSINESS RC SENYAMULE AIMWAGIA SIFA TANTRADE, KAMATI YA MAANDALIZI MAONESHO YA MADINI GEITA

RC SENYAMULE AIMWAGIA SIFA TANTRADE, KAMATI YA MAANDALIZI MAONESHO YA MADINI GEITA

Na: Mwandishi wetu, GEITA.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule ameipongeza TANTRADE kwa kushirikiana na Kamati ya Maandalizi kwa kuweza kufanya uratibu mzuri katika Maonesho ya Nne ya Teknolojia kwenye Sekta ya Madini yaliyofanyika kwa Siku 10 Mkoani humo


Mhe. Senyamule ametoa pongezi hizo kwenye hotuba yake  wakati wa hafla ya kuyafunga maonesho hayo yaliyofikia kilele chake mwishoni mwa wiki iliyopita  ambapo amesema kuwa TANTRADE wameweza kufanyakazi kubwa ya uratibu, nakwamba uwepo wao kwa kushirikiana na Kamati kumewezesha kuratibu vizuri maonesho hayo.


“Naomba niipongeze sana TANTRADE kwa kushirikiana na Kamati nzima ya Maandalizi wameweza kutusaidia kufanya uratibu mzuri wa Maonesho haya ambayo mwaka huu yamekuwa Bora sana na kupata ushiriki wa wafabiashara na Taasisi nyingi zaidi ya mwaka jana” alisema Mhe. Rosemary huku akisema kuwa zaidi ya washiriki 5000 walijitokeza kushiriki maonesho hayo.


Aidha kwenye maonesho hayo kulifanyika Kliniki maalum ya Biashara ambapo zaidi ya wananchi 2000 waliweza kuhudumiwa kupitia Kliniki hiyo iliyokuwa chini ya Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE).

 

Katika maonesho hayo ya siku 10 yaliyofana sana Kliniki hiyo  maalum ya Biashara ilihusisha jumla ya Taasisi 13 ambazo kwa pamoja waliweza kukaa pamoja na kutoa huduma za pamoja kwa wananchi waliokuwa na changamoto mbalimbali za kibiashara na kuzitafutia ufumbuzi.

 

Akizumza kwenye mahojiano maalum  mara baada  kumalizika kwa hafla ya kufunga maonesho hayo, mratibu na msimamizi Mkuu wa Kliniki hiyo Ofisa Masoko ya nje wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Bi. Upendo Nduguru alitoa tathimini ya namna ambavyo Kliniki hiyo ilivyoweza kutoa msaada wa hapo kwa papo kutokana na kuwepo kwa Taasisi zote muhimu zinazogusa moja kwa moja maeneo ya wananchi hao hususani wafanyabiashara na wajasiriamali.

“Kliniki hii imekuwepo hapa mahususi kwaajili ya kutoa majawabu ya maswali mbalimbali ya wananchi hasa kwenye eneo la Bishara, kama masuala ya Leseni za Biashara, namna ya kupata Masoko ya Biashara zao, Mambo ya uwekezaji na mengine mengi” alieleza Upendo. 

Aliongeza kuwa TANTRADE imekuwa ikiendeesha Kliniki za aina hiyo kwenye maonesho mbalimbali kwani inatambua kuwa hiyo ni njia bora ya kuzifikia changamoto za wafanyabiashara na wajasiriamali ambao wamekuwa wakiangahika kutafuta taarifa sahihi za huduma hizo nakwamba kwa kufanya hivyo inawasaidia kuzifanyiakazi changamoto zao kwa wakati mmoja.

 

“Hapa kwenye hii Kliniki tuna Taasisi mbalimbali ambazo ni TANTRADE, BRELA, TIA, SIDO, FCC, TRA, TIRA, TIC, EPZA, GS1, NEEC, na Mkeamia Mkuu wa Serikali. ambazo zote hizi zimejipanga katika kutoka majawabu ya maswali ya wafabiashara na kutatua changamoto zao hapo kwa papo” aliongeza Upendo.

Katika Kliniki hiyo pia ilitembelewa na ujumbe wa wafabiashara kutoka nchini Marekani waliofika kwenye maonesho kujifunza na kuona fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji wakiongozana na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ambao waliweza kupata kufahamu taratibu zote za namna ya kuweza kuwekeza na kufanyabiashara nchini Tanzania na kupongeza kazi zinazofanywa na Kliniki hiyo.

 

Kwa upande wao baadhi ya wafabiashara na wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo wameipongeza TANTRADE kwa ubunifu mkubwa ambao umewafanya kuweza kupata huduma zote kwenye eneo moja.

 

“Maonesho ya mwaka huu ni mazuri sana hii ni mara yangu ya tatu kushiriki lakini nimeona mwaka huu kumekuwa na tofauti kubwa, kuna wenzetu ni wajasiriamali wadogo wamefika hapa kila kitu wamepata  Vyeti vya BRELA na huduma ya TRA wamekamilisha hapa hapa kwakweli nawapongeza sana waandaji” alizungumza Mjasiriamali wa Bidhaa za Viungo Bi Sasha.

 

Kumalizika kwa maonesho hayo kunatoa fursa kwa waandaaji hususani uongozi wa Mkoa wa Geita ambao umetangazwa rasmi kuandaa maonesho hayo Kitaifa na Kimataifa kuweza kufanya tathimini itakayowawezesha kuandaa maonesho mengine ya mwaka 2022 yatakayofanyika katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa.

 


 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here