WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kimkakati cha maegesho ya magari makubwa katika eneo la Nyakanazi wilayani Biharamulo, Kagera.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 18, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Nyakanazi baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho ambao unagharimu sh. bilioni 2.6 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2021.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa kuwaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera wahakikishe wanasimia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ukiwemo na huo wa ujenzi wa kituo cha maegesho ya magari makubwa kwa maendeleo ya wananchi.
Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kuhakikisha eneo la Nyakanazi linapimwa na kuanisha matumizi ya kila eneo ikiwemo makazi, Huduma za Jamii, Viwanda, Viwanja vya Michezo na maeneo mbalimbali ya uwekezaji