Yatanunuliwa kuanzia Jumatatu Septemba 13, 2021.
BUNGENI, DODOMA.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa sh. bilioni 50 ambazo zitatumika kununua mahindi kutoka kwa wakulima ili kuwanusuru na kudodora kwa bei ya zao hilo.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 10, 2021) Bungeni wakati akiahirisha mkutano wa nne wa Bunge la 12, jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 2, mwaka huu.
“Jana tarehe 9 Septemba 2021, Bunge lako tukufu lilipokea hoja binafsi kutoka kwa Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo ambayo iliungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge. Serikali imesikia kilio cha wakulima kupitia Waheshimiwa Wabunge. Tayari tumepata shilingi bilioni 50 na ununuzi utaanza Jumatatu, tarehe 13 Septemba, 2021,” amesema.
Akitaja hatua nyingine ambazo Serikali imechukula ili kunusuru bei ya zao hilo, Waziri Mkuu amesema awali Serikali ilitoa sh. bilioni 15 kuuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mahindi maeneo mbalimbali nchini. Amesema pia, Serikali ilishatoa sh. bilioni 10 kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ili kuongeza mtaji wa ununuzi wa mazao.
“Naiagiza Wizara ya Kilimo izisimamie kwa karibu NFRA na CPB ili zinunue mahindi ya wakulima pekee, tena watoke ndani ya nchi. Aidha, ongezeni vituo vya kununulia mahindi hadi wilayani na kwenye miji midogo,” amesema.
Akibainisha hatua zaidi zilizochukuliwa, Waziri Mkuu amesema Serikali imetafuta masoko ya mahindi kwa kukamilisha mikataba mipya ya ununuzi wa mahindi na nchi za Sudan ya Kusini, DRC na Zimbabwe kama njia ya kuhakikisha wakulima hao wanapata soko la mahindi waliyozalisha.
“Hatua nyingine tuliyochukua ni kufungua mipaka kwa kipindi cha miezi miwili kwa ajili ya masoko ya nje ya nchi ambapo vibali vya usafirishaji hutolewa bure kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya na kwa njia ya mtandao ili wafanyabiashara waweze kuvipata kwa urahisi. Upelekaji wa chakula utafanywa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na hifadhi ya kutosha ya chakula,” amesisitiza.
Amezitaja hatua nyingine kuwa ni kuwaunganisha wafanyabiashara wa nafaka hapa nchini na wafanyabiashara wa nje kupitia Balozi za Tanzania na kuongeza thamani ya mazao.
Mbali na ununuzi wa nafaka, Waziri Mkuu amesema Serikali inafuatilia mwenendo wa upatikanaji wa mbolea ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wingi na bei nafuu. “Lengo la Serikali ni kuwawezesha wakulima kumudu gharama za mbolea,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wakulima na wanunuzi wa mazao waendelee kuuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa vile umeonesha matokeo makubwa yenye manufaa.
“Mfumo wa stakabadhi ghalani ndiyo pekee uliothibitika na kuonesha matokeo makubwa yenye manufaa. Hivyo basi, tuendelee kuuimarisha katika mazao yote ya biashara nchini ili kuleta mafanikio kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.”
Amesema Serikali imeondoa mifumo isiyo rasmi ya ununuzi wa mazao ambayo imekuwa ikiwakandamiza wakulima na kuwanufaisha baadhi ya wanunuzi wasiokuwa waaminifu. “Tuliondoa mifumo kama vile kangomba, butula, chomachoma, kula maua, njemke na mingineyo ambayo ilikuwa ikimpunja na kumnyonya mkulima.”
Ameyataja baadhi ya mazao yaliyonufaika na mfumo huo kuwa ni korosho, ufuta, dengu, choroko na kakao na kuongeza kuwa ufanisi wa mfumo huo, umekuwa kichocheo katika kupunguza umaskini na kuongeza uchumi wa nchi na wakulima.
“Taarifa zinaonesha kuwa kuuza mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na ushirika kunatoa nguvu ya pamoja kwa wakulima ya upatikanaji wa soko sambamba na kuimarisha bei ya mazao. Minada iliyofanyika imesaidia kuongezeka kwa bei ya mazao yaliyotumia mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo korosho, ufuta, dengu, choroko na kakao.
“Mwaka 2020, bei ya choroko iliongezeka kutoka shilingi 600 hadi 800 kwa kilo na kufikia shilingi 900 hadi 1,300 kwa kilo katika vituo vya Magu, Uzogele, Igunga na Manyoni. Hivi karibuni tumeona bei ya kakao ikiongezeka maradufu kutoka shilingi 2,500 hadi 5,000 kwa kilo baada ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.”
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo ifanye kazi kwa karibu na vyama vya ushirika na vyama vya msingi kuhakikisha wanawawezesha wakulima kupata elimu na manufaa ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani bila usumbufu ili uwapatie tija.