“Tumekuja hapa kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya mmiliki wa leseni na mkandarasi mwenye mitambo hii ya kusaga kokoto, sitaki tena kusikia mtambo huu umezimwa eti kwa sababu ya mgogoro, sisi siyo Wizara ya Migogoro, sisi ni Wizara ya Madini,” amesema Waziri Biteko.
Aidha, Waziri Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya bilioni 300 kwa ajili ya kujenga mradi wa barabara ya mzungunguko pamoja na majengo makubwa jijini Dodoma ili kukuza uchumi na kuepuka foleni jijini humo.
“Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan anataka mradi wa barabara ya mzunguko uishe kwa wakati na kwa gharama ndogo, tunavyochelewa, tunawachelewesha wananchi kupata huduma ya barabara bila sababu ya msingi,” amesisitiza Waziri Biteko.
“Tumekuja hapa kutatua mgogoro ulio dumu kwa muda mrefu kati ya aliyepewa leseni na mkandarasi anayejenga mtambo huu wa kusaga kokoto, tumekubaliana na pande zote mbili kwamba mradi uanze leo na huu mtambo uliozimwa sitaondaka hapa mpaka mtambo uwashwe na uanze uzalishaji leo,” ameongeza Waziri Biteko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amempongeza Waziri Biteko kwa kufika katika kijiji cha Mndem kutatua changamoto zilizokuwepo kwa kipindi kirefu ambapo amesema amefurahi kwa kuambiwa nani aliyepewa leseni katika eneo hilo na sas anamfahamu.
Pia, Munkunda amesema kuwa, sehemu kubwa ya madini ya ujenzi yatakayotumika katika ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko ya kilometa 110 jijini Dodoma mengi yatatoka wilaya ya Bahi.
Munkunda amemuhakikishia Waziri Biteko kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watu wote wanaomiliki leseni katika wilaya ya Bahi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu.
Sambamba na hilo, Mwanahamisi ametoa wito kwa wawekezaji wengine kuja wilayani Bahi kuwekeza kufuatia maeneo mengi wilayani humo yanahifadhi kubwa ya madini ya ujenzi.