Na: Maiko Luoga Tanga.
Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga linaendelea na ziara ya matembezi ya msalaba kwa miguu kwa lengo la kutangaza injili kwa vitendo ishara ya kuenzi maisha na matendo ya Yesu Kristo aliyoyafanya alipokuwa duniani akisaidia jamii kupitia neno la Mungu.
Washiriki wa matembezi hayo ya msalaba Dayosisi ya Tanga walianza rasmi septemba mosi 2021 huko Buiko na kilele chake kitafanyika septemba 19/2021 katika eneo la Magila msalabani kwa ibada kubwa itakayowakutanisha viongozi na waumini wa Kanisa Anglikana kutoka Dayosisi mbalimbali Tanzania.
Askofu mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Dkt, Maimbo Mndolwa amesema licha ya kutangaza Injili kwa watu wote matembezi hayo huwasaidia washiriki kufanya mazoezi pindi wanapotembea kwa miguu ili kulinda Afya zao sambamba na kufanya utalii katika maeneo tofauti wanayopita.
Baadhi ya washiriki wa matembezi ya msalaba 2021 katika Dayosisi ya Tanga wakiwemo Kasisi Canon Aidan Kamote, Mama Mbelwa, Canon James Waziri na Vijana wengine wanaoshiriki wamesema matembezi hayo yanawajengea ukakamavu pamoja na kuilinda miili yao na magonjwa kwakuwa wanafanya mazoezi.
Huduma mbalimbali hufanyika katika matembezi hayo ikiwemo ibada za Kipaimara, Ujana, ushirika mtakatifu, ubatizo, kufungua na kupanda makanisa mapya, mikutano ya injili, kuombea wagonjwa na watu wenye shida ambao wameeleza kufunguliwa mara baada ya kuushika msalaba pindi uwapo kwenye maeneo yao.Maeneo mengine ni Dimbwi, Kihurio, Lasa, Bendera, Mkomazi, Mazinde na Septemba 11/2021 wamewasili Mombo kisha Septemba 12/2021 wataendelea na safari kuelekea maeneo ya Msambiazi hadi kuingia Magila msalabani hapo Septemba 19/2021 ambapo watakuwa wametumia siku 19 kutembea kwa miguu jumla ya kilomita 440