Mhe. Rosemary Senyamule Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema mpaka leo Septemba 25, 2021 mpango wa kuchangia damu unaoendelea kwenye banda la damu Salama kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa na Waandishi wa Habari umefanikisha kupata chupa za damu 288 kutoka kwa wananchi mbalimbali waliojitolea kuchangia.
Mhe. Senyamule amesema hayo leo baada ya yeye mwenyewe kutoa damu kwenye Banda hilo huku akiungwa mkono na wananchi mbalimbali ambao kwa baada ya kusikia wito wake walihamasika na kuamua kusaidia kuokoa maisha ya wananchi kwa Jambo hilo.
“Niwashukuru wote ambao wameshiriki kwa namna tofauti kuja kutoa damu zao niendelee kuwashukuru wote kuja kuendelea kutoa damu, nataka miseme wazi kwamba ndani ya siku ya 10 tangu maonesho ya Madini yalipoanza tumepata Chupa 288 mpaka sasa.” Mhe. Senyamule akipongeza.
“Natamani kuwa na wananchi wenye afya njema na nimeona sio jambo sahihi kuwahamasisha wengine alafu mwenyewe nisitoe damu na ndio maana nipo hapa leo na nimeshatoa damu, nawashukuru wote walioniunga mkono na ninamshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa mchango wake Tshs. laki tatu alionipatia ili kufanikisha jambo hili.” Mkuu wa Mkoa.
“Mara nyingi Waandishi wa Habari tumekua tukiandika Habari za wananchi tena wengine wakiwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kuishiwa damu sasa tukaona tusiishie kuripoti tu nasi tuwe sehemu ya msaada kwa kuchangia na kuhamasisha wengine kutoa damu.” Mutta Robert, Mwandisi wa Gazeti la Majira.