Meneja wa KAIZEN Wizara ya Viwanda na Biashara Jane Lyatuu akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu KAIZEN na namna inavyofanyakazi katika ukumbi wa Chuo cha Biashara Jijini Dar es Salaam. (PICHA NA: HUGHES DUGILO)
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Sileja Lushibika Mratibu na Mkufunzi wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara akifundisha. (PICHA NA: HUGHES DUGILO) |
DAR ES SALAAM.
Wizara ya Viwanda na Biashara imeendesha mafunzo maalum ya falsafa ya KAIZEN kwa waandishi wa habari na wasanii ili kuwajengea uwezo katika kuifahamu falsafa hiyo muhimu inayotekelezwa hapa nchini kupitia wizara ya Viwanda na Biashara.
Akizungumza katika mafunzo hayo leo yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biashara (CBE) Jijini Dar es Salaam Meneja wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Jane Lyatuu amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kwenye maadhimisho ya falsafa ya KAIZEN ambapo kwa mwaka huu Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo ya siku tatu yatakayoanza tarehe 24 hadi 26 Agosti,2021 na kufunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo.
Bi. Jane ameongeza kuwa Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na nchi zipatazo 20 kwa njia ya mtandao ambapo baadhi ya washiriki watakutana na kupata fursa ya kuzungumzia mambo kadha wa kadha yanayohusiana na KAIZEN na kusisitiza kuwa hiyo itatoa fursa kwa Tanzania kama mdau kuvutia wawekezaji kwa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji nchini pamoja na Bidhaa za Kitanzania.
“Katika maadhimisho haya nchi yetu ya Tanzania itapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa nchi hizo mbinu bora za kutumia falsafa ya KAIZEN katika kukuza sekta ya viwanda na biashara nchini”. Amesema Bi.Jane.
KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya ‘badilika’ kwa ubora/uzuri na hutumika katika biashara, na shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi, mfumo, michakato na nyanja zote za kuendesha biashara.