Home BUSINESS WAZIRI WA UWEKEZAJI ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA

WAZIRI WA UWEKEZAJI ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA

 

GEITA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Geofrey Mwambe ameridhishwa na utendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) hasa katika kuwafikia wadau wake popote  walipo.
 
Kauli hiyo ameitoa Agosti 11, 2921  katika banda  la BRELA kwenye Tamasha la kuhamasisha Utalii na Maonesho ya biashara linaloendelea Chato, Geita.
 
Akiwa katika banda hilo Waziri Mwambe alielezwa madhumuni ya BRELA kushiriki katika maonesho hayo na jinsi inavyowafikia  wafanyabiashara katika maeneo yao.
 
Akitoa ufafanuzi kwa Waziri Mwambe, Ofisa Msaidizi wa Usajili kutoka BRELA, Bw. Seleman Seleman alieleza kwamba ushiriki wa taasisi hiyo ni sehemu ya jitihada za kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao na kuwatatulia changamoto zao.
 
“Hivi sasa mtu yeyote anayehitaji huduma zetu haina haja ya kusafiri kuja ofisini. Usajili unafanyika kwa njia ya mtandao ukiwa popote na muda wowote”.alieleza Bw. Seleman na kuongeza kuwa licha ya kutoa huduma kwa njia ya mtandao, BRELA imechukua hatua zaidi kwa kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao na kuwapatia huduma za papo kwa papo.
 
Aidha Bw. Suleman ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Geita na jirani kutumia fursa hiyo kufika katika maonesho hayo ili kupata elimu na usaidizi wa haraka.
 
Katika hatua nyingine Wafanyabiashara washiriki wa Tamasha hilo wameipongeza BRELA kwa huduma wanayotoa katika maonesho hayo.
 
Hayo yamebainishwa na Wafanyabiashara hao kwa nyakati tofauti tofauti walipofika katika banda la BRELA kwa ajili ya kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na utatuzi wa changamoto mbalimbali ambao unafanyika papo kwa papo.
 
Bi. Haliswa Chobba mfanyabiashara na mshiriki wa maonesho hayo akitokea Dar es Salaam aliyefanikiwa kusajili Jina la Biashara papo kwa papo amesema kwamba, amefurahishwa na huduma aliyopata BRELA tangu amefika katika banda hilo na kufanikiwa kupata cheti cha usajili.
 
Naye Bw. Jovin Mwarabu aliyepata huduma ya kulipia Mizania ya Mwaka (Annual returns) ameeleza kuwa huduma hii itawahamasisha watu wengi sana kufanya usajili hasa wasiokuwa na uelewa mpana na matumizi ya mitandao na ameiomba  BRELA kufika katika maeneo hayo walau mara moja kwa Mwaka.
 
Katika maonesho hayo Ili kuweza kufanya Usajili wa papo kwa papo wadau wanatakiwa kufika na namba ya kitambulisho cha Taifa, namba ya simu inayofanya kazi pamoja na anuani ya barua pepe inayofanya kazi.
 
Kwa wale ambao wametuma maombi ya huduma mbalimbali na bado hayajakamilika, wanahimizwa kufika katika Banda la BRELA ili kupata maelekezo na usaidizi wa haraka wa kukamilisha maombi yao.
 
Katika Maonesho hayo pia huduma zinazotolewa ni pamoja na Usajili wa Makampuni, Majina ya biashara, Alama za biashara na huduma, kupata Leseni za Biashara kundi A na kupata Hataza.
 
Tamasha la kuhamasisha Utalii na Maonesho ya biashara yalianza Agosti 7 na kuzinduliwa rasmi na Waziri Mwambe Agosti 11, 2021 na yanatarajiwa kufikia tamati Agosti 15.

Previous articleKUTOKA MEZA YA MAGAZETI ASUBUHI HII YA LEO IJUMAA AGOSTI 13-2021
Next articleTANZANIA KINARA UWEKEZAJI AFRIKA MASHARIKI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here