Home BUSINESS WAZIRI BITEKO ATEMBELEA MGODI WA LUKALASI UNAOMILIKIWA NA MZAWA

WAZIRI BITEKO ATEMBELEA MGODI WA LUKALASI UNAOMILIKIWA NA MZAWA

Waziri wa Madini Dotto Biteko kushoto na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge kulia,wakimsikiliza jana mmiliki wa mgodi wa dhahabu Lukalasi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Jonson Nchimbi katikati wakati wa ziara ya Waziri wa madini alipotembelea mgodi huo ili kujionea kazi zinafanywa na mwekezaji huyo.

Mmiliki wa mgodi wa dhahabu Lukalasi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Jonson Nchimbi kulia,akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa dhahabu kwa Waziri wa Madini Dotto Biteko katikati, aliyetembelea mgodi huo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma,kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge. ( Picha na Muhidin Amri).

Na: Muhidin Amri,MBINGA

WAZIRI wa madini Dotto Biteko, ametembelea mgodi wa dhahabu wa Lukalasi  katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma unaomilikiwa na mzawa Jonson Nchimbi na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na mwekezaji huyo.


Waziri Biteko amesema, wizara ya madini itaendelea kumuunga mkono mwekezaji huyo mzawa katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.


Kwa mujibu wa Waziri Biteko,  katika kipindi kifupi mwekezaji huyo  amechimba dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 3 na amelipa  zaidi ya Sh milioni 200 kama kodi kwa Serikali.


Amewaomba wananchi wanaofanya kazi katika mgodi huo kufanya kazi kwa uaminifu  na kujiepusha na vitendo vya wizi vinavyoweza kumvunja moyo mwekezaji huyo mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma.


Amesema, haya madini ni nyenzo pekee ambaye Watanzania tumepewa na Mungu ili tuondoa umaskini wetu,kwa hiyo ni lazima tuchimbe kwa haki,kulipa kodi na kufuata sheria na taratibu za nchi badala ya kutugombanisha.


Waziri Biteko amesema,kwa kutambua uwekezaji huo, Serikali itaendelea kumsaidia kwa kumpatia wataalam ili aweze kuchimba dhahabu kisasa na kumkutanisha na taasisi mbalimbali za fedha ili  kupata mikopo.


Amesema, lengo  ni kumwezesha kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini kwa  sababu bado ana vifaa vya kizamani.


Amesema, serikali  inatambua leseni zote na baadhi bado hazijafanyiwa kazi na nyingine zimeisha muda wake, hivyo wizara ya madini itazifuta ili kupewa watu wengine watakaokuwa tayari kuchimba na kuachana na watu wenye tabia ya kushikilia maeneo bila ya kuyafanyia kazi.


Amesema,uchimbaji  wa madini ni safari ndefu na serikali inawahitaji sana wachimbaji wakubwa na wadogo  na kamwe wizara haitaruhusu kuwepo kwa wachimbaji wakubwa pekee yake kwani inahitaji watu wengi kufanya utafiti ili kufahamu kiasi cha madini kilichopo katika nchi yetu.


Ameiagiza,ofisi ya Mkuu  wa Ruvuma na mkuu wa wilaya Mbinga kuhakikisha inapitia upya maeneo na leseni zote ambazo hazijaendelezwa ili maeneo hayo yaweze kupewa vikundi vidogo kwa ajili ya uchimbaji.


Mmiliki wa mgodi huo Jonson Nchimbi amesema,tangu mgodi ulipoanzishwa wameweza kuzalisha dhahabu yenye thamani ya Sh.bilioni 3,038,167,518.24 na kulipa mrabaha wa Sh.182,290,051.09,ada ya ukaguzi Sh. Milioni 30,381,675.18 pamoja na ushuru wa Halmashauri jumla ya Sh.9,114502.55.


Aidha amesema,mgodi  unashiriki  shughuli mbalimbali za kijamii na  za maendeleo katika kijiji cha Lukalasi na umetoa ajira kwa wananchi wasiopungua 300 wanaofanya kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa dhahabu juu ya ardhi.


Hata hivyo amesema, kwa kuwa eneo hilo limeanza kujulikana kuwa na uzalishaji mzuri wa dhahabu kumeanza kutokea migogoro michache ya kuingiliana katika  leseni za uchimbaji na kuishukuru wizara ya madini kumaliza moja kati ya migogoro hiyo.


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge amesema,serikali inatambua uwezo wa mgodi huo katika kuongeza ajira na mapato ya serikali na mapato binafsi.


Balozi Ibuge,amewataka wananchi wanaishi kuzunguka mgodi huo kutambua juhudi za uwekezaji  na kazi inayofanyika  katika mgodi huo ambao tangu ulipoanzishwa umeshaleta manufaa makubwa.


Hata hivyo,ametaka kufanyiwa kazi tatizo la  kushuka kwa uzalishaji wa dhahabu katika mkoa huo ambapo kwa Mwezi Julai dhahabu iliyopatikana ni kilo  2,wakati mwezi Juni ilikuwa kilo 4, na Mwezi Mei kilo 5.


Amesema, serikali ya mkoa itaendelea kuunda vikundi vingi na kuwataka viongozi wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Ruvuma kuhamasisha wanachama wake kwa kuwa lengo la Serikali ya mkoa ni kutoa ajira na kuongeza mapato yatokanayo na madini.

MWISHO.


Previous articleMADIWANI DAR WAGOMA KUPITISHA TAARIFA ZA TARURA
Next articleZAIDI YA WATU LAKI MBILI WAPATIWA CHANJO KWA HIARI HADI SASA TANZANIA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here