Home LOCAL TULIHIMIZA MATUMIZI YA TIBA ASILI KWA SABABU HAPAKUWA NA NJIA NYINGINE YA...

TULIHIMIZA MATUMIZI YA TIBA ASILI KWA SABABU HAPAKUWA NA NJIA NYINGINE YA KUPAMBANA DHIDI YA CORONA.

Na: WAMJW- Nairobi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania ilihimiza matumizi ya tiba asili wakati wa mlipuko wa wimbi la kwanza la Corona kwa kuwa zilionesha kuwasaidia watu wengi kwenye kipindi hicho ambapo Dunia haikuwa na njia mbadala yoyote ya kupambana dhidi ya Corona ukilinganisha na uwepo wa chanjo katika kipindi hiki. 

Dkt. Gwajima amesema hayo wakati akiongea na Waandishi wa habari wa nchini Kenya ambapo wamefanya mkutano wa pamoja wa kujadili changamoto zinazowakabili nchi hizo mbili ikiwemo ya UVIKO-19 kwa upande wa mipakani.

“Ugonjwa huu uliingia Wuhan nchini China Disemba 2019, wakati Dunia ilikuwa haielewi ifanye nini, Dunia nzima ilikuwa haina chanjo, haina formula ya dawa, haielewi ifanye nini kwa mfano; wakati huo nyoka ameshaingia ndani na wewe ndio mama na Watoto wamekuzunguka na nyoka yupo mlangoni, inatakiwa unapigana kwa mwiko kwa kummwagia uji au kwa chochote na ndivyo ilivyokuwa ” alisema

Aliendelea kusema kuwa, Tiba asili Kwa upande wa Tanzania lipo Baraza la kitaalamu kisheria ambayo imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kiasi kikubwa zimeonesha kusaidia watu wenye matatizo ya kifua  kwa kuona umuhimu katika mapambano hayo ilikuwa ni muhimu kutumia tiba hizo ili kunusuru maisha ya Watanzania.

Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema kuwa, Tiba asili zilikuwepo toka zamani kabla ya dawa nyingine hazijaja, na zilisaidia kutibu magonjwa mengi, hata katika vita dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona kwenye wimbi la kwanza tiba asili ilionesha mafanikio makubwa sana.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa, licha ya kutumia tiba asili katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Serikali ilihimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga nyingine ikiwemo kufanya mazoezi, kula chakula bora (lishe bora), kuvaa Barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na kuepuka misongamano isiyo yalazima.

Hata hivyo, Dkt. Gwajima alisisitiza kuwa, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliielekeza Wizara ya Afya kujiridhisha  usalama na ubora wa chanjo zitakozo gunduliwa kabla ya kuziruhusu kwa Watanzania, kupitia Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Aliendelea kusema kuwa, Baada ya Serikali ya awamu ya sita inayosimamiwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, kazi ya kutafiti usalama iliendelea na kupitia Kamati ya Wataalamu aliyounda ilijiridhisha usalama wa Chanjo kutokana na kutumika katika nchi zaidi ya 170 kupitia Covax Facility kuwa chanjo inapunguza ukali wa ugonjwa na vifo.

Ametoa rai kwa wananchi kutumia fursa hii kupata chanjo ili kupunguza uwezekano wa kupata kifo au kupunguza ukali wa ugonjwa, huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu, kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kuvaa Barakoa, kuepuka misongamano isiyo yalazima, kufanya mazoezi, kutumia Lishe bora, na kuwakinga walio na umri mkubwa na waishio na magonjwa sugu.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here