Home LOCAL TANZANIA NA KENYA WAKUBALIANA KUZIPATIA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZA KUPIMA UVIKO 19 WASAFIRI.

TANZANIA NA KENYA WAKUBALIANA KUZIPATIA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZA KUPIMA UVIKO 19 WASAFIRI.

Na.WAMJW-Nairobi

Tanzania na Kenya wamekubaliana ndani ya  wiki nne zijazo kufanyia kazi changamoto kubwa nne katika eneo la kupima wasafiri UVIKO 19.

Makubaliano hayo yamefanyika leo kwenye mkutano wa pamoja baina ya Mawaziri wa Afya wa Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima na Waziri wa afya nchini Kenya Sen. Mutahi Kagwe mjini Nairobi.

Moja ya makubaliano ya kufanyia kazi changamoto hizo ni pamoja na kushusha gharama za upimaji wa UVIKO-19 kwa wasafiri wanaoingia na kutoka katika nchi hizo mbili ili kuchochea masuala ya biashara na utalii baina na nchi hizo mbili.

Nchi hizo pia zimekubaliana kufanyia kazi changamoto ya kulipisha fedha kipimo cha haraka cha Corona (PCR) kwa wasafiri wanaotumia njia ya barabara ikiwemo kuona uwezekano wa kushusha kwa kiasi kikubwa gharama hizo kwa wasafiri  wanaotumia ndege.

Kwa upande wa madereva wanaosafirisha mizigo na bidhaa muhimu  wamekubaliana kufanyia kazi uwezekano wa kutokutozwa gharama kwa kipimo cha Corona ili kupunguza mzigo kwa wasafirishaji ikiwa ni njia ya kuchochea uchumi kwa nchi hizo mbili.

Aidha Tanzania na Kenya wamekubaliana kuona uwezekano wa kutumia mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya kufuatilia afya za wasafiri pamoja na  kudhibiti wasafiri wasio kuwa waaminifu kwa  kugushi vyeti hivyo wanapopita mipakani.

Hata hivyo katika mkutano huo Mawaziri hao wamekubaliana kufanyia kazi mpango wa kuvitambua vyeti vya  upimaji vinavyotolewa na mamlaka za afya za nchi hizo mbili, pamoja na kubadilishana taarifa zinazohusu masuala ya afya ili kuimarisha udhibiti wa magonjwa mbalimbali yanayowaathiri wananchi wa pande hizo mbili ikiwemo Malaria, Polio na Corona.

Akiongea wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Waziri wa Afya Dkt. Gwajima amesema kuwa tatizo la ugonjwa wa Corona ni la dunia nzima hivyo lazima  kuangalia ni namna gani halitowadhuru sana ili uchumi na ustawi wa jamii na nchi uendelee kwa kuweka makubaliano ya kuishi kwa Amani kama watu wanaoishi katika kijiji kimoja cha afrika mashariki.

Dkt. Gwajima amesema ugonjwa huo uliowafika hauwezi kuwaacha iwapo kutakuwa hakuna suluhu ya pamoja ya kuudhibiti kwani hadi sasa ugonjwa huu umetufundisha mengi na viongozi wa nchi zote mbili wamekuwa wakitoa maono mengi. Hivyo, kama Mawaziri wenye dhamana kwa kushirikiana na wataalam watahakikisha wanatafsiri dhamira ya viongozi wakuu wa nchi ili kuja na uhalisia.

Aliongeza kuwa janga hilo ni kubwa hivyo ni lazima kuendelea kushirikiana katika kudhibiti  na kuzuia anuai mpya za ugonjwa wa Corona kwa pamoja kwani miundombinu ya uchumi inashuka katika nchi zetu na kwa jamii pia.

“Baada ya kutokea janga hilo wasafiri na madereva walikua wanatakiwa kuendelea kusafirisha abiria,mizigo na bidhaa muhimu hivyo kubwa ni lazima kuweka jitihada ili kuwarahisishia wananchi kuendelea na shughuli za uchumi na maisha kwa usalama kwa ushirikiano baina ya nchi zetu hizi”.

Naye Waziri wa Afya nchini Kenya Sen.Mutuhi Kagwe  amesema kwamba Tanzania na Kenya ni majirani wa muda mrefu  hivyo vyovyote watakacho fanya hawawezi  kuwaacha majirani zao ambao ni Tanzania.

Katika kukabiliana na Corona Waziri Kagwe amesema lazima kujifunza kuishi nao  hivyo ni jambo la kuelewa kwamba hakuna nchi itakayokuwa na nguvu bila kushirikiana.

“Sisi ni wamoja lazima tuendelee kujisaidia wenyewe Katika mapambano haya na vile vile kwenye Malaria,Polio kwa wananchi wetu mipakani” Alisisitiza.

Aliongeza kwamba nchi hizo mbili zina mashirikiano ya muda mrefu  katika maeneo  na sio tu masuala ya afya tu, hivyo wataimarisha ushirikiano hata katika maeneo mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here