Home BUSINESS STAMICO NA TANESCO KUSHIRIKIANA KUZALISHA UMEME KWA MAKAA YA MAWE YA KIWIRA

STAMICO NA TANESCO KUSHIRIKIANA KUZALISHA UMEME KWA MAKAA YA MAWE YA KIWIRA

 

 

DODOMA.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini hati ya makubaliano na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutekeleza Mradi wa kufufua umeme wa Megawati 200 kwa kutumia Makaa ya Mawe yanayopatikana Kiwira mkoani Songwe.

Makubaliano haya yamefikiwa leo Agosti 10, 2021 baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini wa Hati ya Makubaliano uliofanyika ofisi za TANESCO Makao Makuu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka katika Taasisi hizo mbili.

Akielezea umuhimu wa makubaliano hayo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema utekelezaji wa mradi huu unaenda kuyaongezea thamani madini ya makaa ya mawe kwa kuwa kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki kimamilifu katika uzalishaji wa umeme kwa ajili ya kulisha kwenye gridi ya Taifa.

Dkt. Mwasse amesema, amefurahi kuona umefika wakati sasa Taasisi za Serikali zinashirikiana katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na makubaliano haya ni mwanzo wa utekelezaji wa mradi huu ambao unaenda kuongeza ajira kwa watanzania na kuboresha uchumi wa wazawa wa maeneo hayo.

Ameongeza kwa kusema taasisi hizi mbili zinafanya kazi tofauti lakini zinategemeana katika kuliletea Taifa maendeleo. Hivyo mashirikiano hayo yataiwezesha STAMICO kuongezea thamani katika madini ya makaa ya mawe wakati huohuo TANESCO inapata Malighafi zitakazowawezesha kuzalisha umeme wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya nchi na kuwezesha uwepo wa viwanda nchini.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa TANESCO kwa kushirikiana bega kwa bega tangu STAMICO ilipoanza mchakato wa kuhuisha mradi huu unaolenga kuokoa rasilimali madini zilizopo katika mgodi ili ziweze kuwanufaisha watanzania

Akiongea kwa upande wa TANESCO Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Tito Mwinuka amesema makubaliano haya ni hatua ya awali inayotoa nafasi kwa kila Taasisi kufanya majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano, ambapo hatua hii itafuatiwa na kufanyika kwa upembuzi yakinifu ili kuweza kubainisha mambo mbalimbali ikiwemo teknolojia na gharama halisi ya utekelezaji wa mradi huu.

Amebainisha majukumu ya kila Taasisi katika makubaliano hayo yatakayodumu kwa muda wa miaka miwili yakuhusisha kufufua mgodi wa chini ya ardhi, kujenga mgodi wa wazi, kujenga mitambo wa kuzalisha MW200 na kujenga njia ya kufarisha ya msongo KV. 400 yenye urefu wa km 100.

Amezitaja faida za mradi huu zikiwemo; utekelezaji wa mradi huu utaongeza kasi ya kusambaza umeme katika maeneo yakayopitiwa na mradi huu, kutekeleza lengo la kibiashara la kuuza umeme kwenye nchi Jirani ikiwa ni dhima kuu ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini wa Afrika. Aidha amesema kuongeza matumizi ya rasilimali nishati kwenye uzalishaji umeme (Power Generation Mix) na kuboresha mifumo ya njia ya kusafirisha umeme.

STAMICO na TANESCO wametia Saini Hati ya Makubaliano ya kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe ikiwa ni hatua ya awali katekelezaji wa mradi huo, ambapo STAMICO itahusika na ujenzi wa mgodi wa wazi wa kuchimba makaa ya mawe, wakati TANESCO itahusika na ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa MW200 (Power Plant) sambamba na njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Kiwira kwenda Mwakibete na kuunganisha na gridi ya Taifa.

 

Previous articleTANZANIA YAINGIA MAKUBALIANO KUANZISHWA TAASISI YA UDHIBITI DAWA UMOJA WA AFRIKA
Next articleKUTOKA MEZA YA MAGAZETI ASUBUHI HII LEO J.TANO AGOSTI 11-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here