Home BUSINESS RC ROSEMARY ATOA NENO KWA WACHIMBAJI WADOGO JUU YA UHIFADHI WA MAZINGIRA...

RC ROSEMARY ATOA NENO KWA WACHIMBAJI WADOGO JUU YA UHIFADHI WA MAZINGIRA GEITA.

Na: Paul Zahoro, RS Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule amewataka wachimbaji wadogo kuzingatia Sheria na Taratibu zinazoendesha Shughuli zao ili pamoja na uwekezaji wao waweze kuhifadhi Mazingira kwa ajili ya uhai wa viumbe hai.

Mhe. Senyamule amesema hayo leo tarehe 20 Agosti, 2021 wakati akizindua Rasmi Mradi wa Jitihada za pamoja za Ufikiwaji wa Haki katika Sekta ya Uziduaji (CLARITY) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa zaidi ya Tshs. Bilioni 2.7 kwa miaka Mitatu kuanzia Aprili 2021 kwenye Mikoa ya Mara na Geita.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa amewashukuru Umoja wa Ulaya na Mashirika kwa kuwawezesha VSO, LEAT na TWCC wataotekeleza Mradi huo katika kuhakikisha Makundi ya Wanawake, Vijana, Walemavu na wajasiriamali wanajengewa uwezo kwenye masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya utawala bora na Mazingira.

“Tunalo tatizo la uharibifu wa Mazingira kutoka kwa wachimbaji wadogo, natoa rai kwa wataalam kuendelea kuwaelimisha namna ya kuondoka kwenye mfumo huo na kutumia teknolojia ya kisasa kwenye Shughuli za Uchimbaji ili wasiharibu misitu” Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Aidha, Mhe. Senyamule ameshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka Mazingira rafiki ya wachimbaji madini kwenye makundi yote kunufaika ikiwemo kuwamilikisha wachimbaji wadogo vitalu vyenye leseni ambavyo havijaendelezwa na wachimbaji wakubwa ili viwanufaishe wenye uhitaji.

Mhe. Senyamule ametumia wasaa huo kuwaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwenye mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 ikiwemo na kutumia fursa ya Chanjo ya hiyari dhidi ya Ugonjwa huo ambayo inatolewa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za Afya Mkoani Geita.

Ndugu Elvis Chuwa kutoka Shirika la VSO amefafanua kwamba kata 80 zitanufaika na Mradi wa kupiga chapuo kwenye haki za binadamu kwenye sekta za Uziduaji, kuwezesha Wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa madini, na kuongeza usawa, uwajibikaji na utawala bora kutoka kwenye Halmashauri tano za Bunda, Tarime, Butiama na Geita na Geita Mji.

Mwenyekiti wa Shirika la TWCC Bi. Mercy Sila amesema kupitia mradi huo Makundi ya wanawake, vijana na Wenye Ulemavu watapata msaada wa Masoko ya bidhaa na msaada wa Sheria ili kufikia na usawa kwenye biashara.

“Mazingira ni dhana pana ambayo yanagusa ardhi, utawala bora na sera za uwezeshaji wa jamii hivyo tushirikiane katika yote haya.” Amesema Bi. Valeria Macha kutoka LEAT.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here