Home LOCAL MAKASISI WATATU NA SHEMASI WAAMURIWA ZANZIBAR, WITO WATOLEWA KUSIMAMIA VIAPO NDANI YA...

MAKASISI WATATU NA SHEMASI WAAMURIWA ZANZIBAR, WITO WATOLEWA KUSIMAMIA VIAPO NDANI YA KANISA

 Na: Maiko Luoga Zanzibar.

Watumishi wa Mungu wakiwemo makasisi na mashemasi wameshauriwa kuishi na kusimamia viapo vyao kwa kutangaza injili ya kweli ili kupitia wao watu waokoke hatimae kuliweka Kanisa katika msingi uliobora.

Wito huo umetolewa na Kasisi Canon Edward Haule kutoka Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga wakati akihubiri kwenye ibada ya kuwaamuru Makasisi watatu na shemasi mmoja iliyofanyika Agosti 24/2021 katika Kanisa Anglikana Mt. John Mbweni Dayosisi ya Zanzibar.

“Kanisani kuna kondoo wa aina mbalimbali wapole na wakali, sisi tumepewa kibali na Mwenyezi Mungu kuwachunga, tunapaswa kuwaleta pamoja ili wamkiri Yesu kisha wawe wamoja, ninyi mlioamriwa leo kuwa makasisi na shemasi mnapaswa kusimamia viapo vyenu ili kuitangaza vyema injili ya Bwana” Canon Edward Haule.

Akizungumza mara baada ya ibada hiyo kukamilika Mhashamu Askofu wa Dayosisi ya Zanzibar Michael Hafidhi ameshukuru ujumbe uliotolewa na Canon Haule na kuahidi kuwa Kanisa Anglikana Zanzibar litaufanyia kazi ili kuboresha zaidi kazi ya Mungu katika eneo hilo na Tanzania kwa ujumla.

Tunakushukuru Canon Haule kwa ujumbe huu, kwa niaba ya Kanisa la Zanzibar tumeupokea tunaufanyia kazi kwa pamoja ili kuendeleza umoja na mshikamano kati ya sisi wahudumu na wakristo hatimae kazi ya Bwana iweze kusonga mbele” Askofu Hafidhi Zanzibar.

Askofu Hafidhi amesema hatua ya kuamuru makasisi watatu na shemasi mmoja ni mwendelezo wa kupanua injili ya Kristo katika Dayosisi ya Zanzibar kwakuwa baada ya hapo watumishi hao watapangiwa vituo vya kazi bila kujali mazingira ambayo bwana amewatuma.

Wakizungumza mara baada ya kuamuriwa na kula kiapo cha utii kwa Askofu, Makasisi watatu Frank Mshihiri, Nebarth Ally, Daniel Maganga na Shemasi Sunday Majaliwa wamesema, watasimamia viapo vyao kumtangaza Kristo wakweli popote katika Dayosisi ya Zanzibar na kumshauri kwa upendo Askofu wa Dayosisi hiyo Michael Hafidhi itakapobidi ili kuimarisha uhai wa Kanisa.

Baadhi ya waumini walioshiriki ibada hiyo wameonesha kufurahishwa na hatua ambayo Makasisi na Shemasi wamefikia huku wakisema wanaamini watakuwa chachu ya kuimarisha umoja na upendo ndani ya kanisa pamoja na kutumia vipawa vyao kupeleka huduma ya kiroho na kwa watu wasiomjua Mungu.

Previous articleDKT.MPANGO ASHUHUDIA UTIAJI SAINI KUONDOA HOJA ZA MUUNGANO ZILIZOPATIWA UFUMBUZI ZANZIBAR.
Next articleMAGAZETI YA LEO J.TANO AGOSTI 25-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here