Home BUSINESS FURSA ZA KUWEKEZA KATIKA VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA NA KUREJESHWA SERIKALINI

FURSA ZA KUWEKEZA KATIKA VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA NA KUREJESHWA SERIKALINI

23 Agosti, 2021 – DAR ES SALAAM.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb) ametangaza fursa za uwekezaji katika Viwanda 20 vilivyokuwa vimebinafsishwa na kurejeshwa Serikalini 

Waziri Mkumbo ameyasema hayo wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu fursa za kuwekeza katika Viwanda vilivyobinafsishwa na kurejeshwa Serikalini leo tarehe 23 Agosti 2021 katika ukumbi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jijini Dar es salaam.

Akiongea na Waandishi hao, Prof. Mkumbo amefafanua kuwa Serikali ilifanya tathimini mwaka 2017 katika Viwanda 156 vilivyobinafsishwa  tangu mwaka 1990 na kubaini kuwa Viwanda 88 vinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya mikataba husika na  Viwanda 68 vilikuwa havifanyi kazi kwa mujibu wa mikataba husika.

Akiendelea kufafanua zaidi, Prof. Mkumbo amesema Serikali ipo katika hatua ya kurudisha Viwanda 48 kati ya Viwanda 68 visivyofanya kazi kwa mujibu wa mikataba husika kwa hatua zingine za uwekezaji ambapo hadi sasa Viwanda 20 havina mgogoro wa kisheria na viko katika hatua ya uwekezaji.

Prof. Mkumbo pia amefafanua utaratibu wa kuwekeza katika Viwanda hivyo 20  kwa kuvigawa Viwanda 10 kwa wawekezaji kutoka Sekta binafsi ili waviendeleze,  Viwanda  nane (8) vimekabidhiwa kwa Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje EPZA kwa ajili ya wawekezaji katika maeneo hayo na Viwanda viwili (2) vitakabidhiwa mashirika ya umma ili waviendeleze kwa kuingia ubia na wawekezaji wa sekta binafsi.

Viwanda 10 vitakavyokabidhiwa kwa Sekta Binafsi  kwa ajili ya uwekezaji ni pamoja na  Kiwanda cha Kilimanjaro Paddy Hauling kilichopo Kilimanjaro, Polysacks Company Ltd kilichopo Dar es salaam, NMC Isaka Rice Mill Company Limited kilichopo Shinyanga na  Multpurpose Oil seed Processing Co.ltd (MOPROCO). Alitaja Prof. Mkumbo.

Vingine vilivyotajwa  na Prof. Mkumbo ni pamoja na CDA Intergrated Concrete Industry Kilichopo Dodoma, Manawa Generies Ltd kilichopo Mwanza, NMC Tabora Rice Mill kilichopo Tabora, Musoma Textikes Mills kilichopo Musoma, NMC Mzizima Maize Mill kilichopo Dar es salaam na Pesticides Manufacturers limited  – Moshi kilichopo Kilimanjaro .

Viwanda nane (8) vinavyokabidhiwa kwa EPZA ni pamoja na Mwanza Tanneries kilichopo Mwanza, TPL Shinyanga Meat Plant kilichopo Shinyanga, Mafuta Ilulu kilichopo Lindi, Nachingwea Cashewnut kilichopo Lindi, TPL Mbeya kilichopo Mbeya,  Sikh Sawmill Limited kilichopo Tanga  na National Steel Corporation kilichopo Dar es salaam. Alitaja Prof. Mkumbo.

Prof Mkumbo pia alibainisha Viwanda viwili (2) vitakavyokabidhiwa Mashirika ya Umma ni pamoja na Mag’ula Mechanical MachineTolls kilichopo Mororgoro kitakabidhiwa kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Mbeya Ceramics Co. Ltd kitakabidhiwa kwa  Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO).  

Aidha amesema  Wawekezaji wenye nia  na uwezo wa kuwekeeza katika Viwanda hivyo wawasilishe maombi yao Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo zoezi la kuwapata wawekezaji litafanyika kwa uwazi na ushindani na taratibu za maombi hayo zitatolewa katika vyombo vya habari.

Wakati huohuo, Prof Mkumbo amesema kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana Ofisi Taifa ya Takwimu (NBS) imekamilisha utafiti wa awali wa kutathimini ya maendeleo ya viwanda nchini  ambapo kwa sasa Tanzania ina viwanda 80,969 kati ya hivyo  Viwanda Vidogo sana vevye uwezo wa kuajili mtu 1 – 4 na mtaji usiozidi milioni tano (5), ni 60,463, Vidogo  vyenye uwezo wa kuajiri  watu 5 hadi 49 na mtaji  wa milioni tano (5) hadi milioni 200 ni 17, 267,  vya Kati venye uwezo wa kuajiri watu 50 hadi 99 na mtaji wa milioni200 hadi milioni 800 ni  684  na Vikubwa vyenye uwezo wa kuajiriwatu 100 na zaidi na mtajizaidi ya milioni 800 ni 618.

Vievile, wakati wa Mkutano huo Prof Mkumbo alisema Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) limebuni mitambo midogo itakayotumika kuzalisha sukari kwa wakulima wadogo katika mikoa yenye uwezo wa kulima miwa ya sukari ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa sukari nchini. 

Naye Mkurugenzi wa TEMDO Prof. Fredrick Kahimba amesema  utengenezaji wa mitambo hiyo yenye uwezo wa kuchakata tani 10 za miwa na kuzalisha tani 1 ya sukari aina ya “brown sugar’  utakamilika kabla ya mwezi Disemba 2021 na kuanza kutumika kabla yam waka wa Fedha 2021/22 kuisha.

Kutokana na ubunifu huo, Prof. Kahimba amewasihi wakulima wadogo katika mikoa yenye mabonde yanayoweza kulimwa miwa ya sukari kulima na kuungana ili kuanzisha Viwanda vidogo vya kuzalisha sukali katika maeneo yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here