Maafika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA)na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) wakipata maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Agosti 02, 2021.
RUVUMA.
Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini katika maeneo yote nchini wametakiwa kuacha tabia ya kuhamisha nguzo za umeme zilizosimikwa kwakuwa kufanya hivyo ni kuchonganisha Serikali na Wananchi wake.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani alieleza hayo wakati akizindua Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, katika Kijiji cha Matiri wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Agosti 02, 2021.
Dkt. Kalemani alieleza kuwa, mkandarasi yeyote aliyesimika nguzo, haruhusiwi kuondoa nguzo hizo na kupeleka sehemu nyingine badala yake ahakikishe anasambaza umeme katika eneo hilo na kuunga wateja wa eneo hilo, na atafute nguzo zingine za kupeleka eneo alilokusudia na kutekeleza mradi.
“Sitaki kuona mkandarasi anafikisha nguzo ‘Site’ anazisimika, au mwingine amezirundika hapo baada ya muda anazitoa wakati hapo na hakuna umeme anapeleka sehemu nyingine ni marufuku!, huku ni kugombanisha Serikali na Wananchi wake, Wananchi wanafahamu serikali imetoa fedha nyingi kuhakisha vijiji vyote vinapata umeme bila kurukwa, unapohamisha nguzo hizo unapeleka ujumbe gani kwa wananchi!” alisema Dkt.Kalemani.
Akizungumzia Usambazaji wa Umeme katika Wilaya ya Mbinga, Dkt. Kalemani alisema kuwa wilaya hiyo inajumla ya Vijiji 169, kati ya hivyo 71 vimepatiwa umeme na 98 vitapatiwa umeme katika mradi huo wa REA III mzunguko wa pili kwa gharama ya shilingi Bilioni 14.34.
Hata hivyo aliwaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi huo Kampuni ya NAMIS kuanza kusambaza umeme katika Kijiji cha Matiri kuanzia mwezi huu (Agosti), 2021.
Aliwasisitiza wakandarasi hao kuwa serikali haitaongeza muda kwa mkandarasi yeyote atakayechelewa kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba, na kwamba 10% ya malipo yake yatakakwa kwa kuchelewesha kazi husika.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Vijiji 554 ambapo vijiji 289 tayari vinaumeme na 265 bado havijafikiwa katika Wilaya za Songea , Mbinga, Nyasa,Tunduru na Mamtumbo kwa gharama za Bilioni 71.95 kwa mkoa mzima.