Home BUSINESS DKT. KABATI ATOA VIFARANGA ZAIDI YA 200 KWA WAJASIRIAMALI MKOANI IRINGA

DKT. KABATI ATOA VIFARANGA ZAIDI YA 200 KWA WAJASIRIAMALI MKOANI IRINGA


DAR ES SALAAM.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Dkt. Ritta Kabati ametoa vifaranga zaidi ya 200 kwa Wajasariamali wadogo mkoani Iringa baada ya kupatiwa mafunzo ya Kilimo, Ufugaji na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali yaliyotolewa na kampuni ya Star inayojishughulisha na utoaji mafunzo ya ujasiriamali nchini.

Katika hafla hiyo ya utoaji vifaranga iliyofanyika katika ukumbi wa Welfare maarufu kama Olofea, Manispaa ya Iringa, Kabati amesema wajasiriamali wote waliopatiwa mafunzo na kupewa vifaranga hao wanapaswa kuvitunza  na kuona vinathamani kuelekea katika ukombozi wa uchumi wao.

Kabati ameeleza kuwa Watanzania hususani vijana wa mkoa wa Iringa wanapaswa kuwa na mkakati wa pamoja wa kuanzisha viwanda vidogo ili kuongeza ajira nchini na pato kwa Taifa kutokana na mkoa wa Iringa kuwa miongoni mwa Mikoa yenye fursa ya Ardhi ya Kilimo na hali ya hewa nzuri.


“vijana wa mkoa wa Iringa pamoja na watu wote tunapaswa kuwa na mkakati wa pamoja wa kuanzisha viwanda vidogo kwani mkoa wetu huu unafursa ya ardhi kubwa na yenye rutuba, ndio maana mazao mengi yanapatikana huku”

Kabati amewataka vijana na makundi maalum kutumia fursa ya uwepo wa mikopo nafuu katika halmashauri za mkoa wa Iringa kujipatia mitaji na kuanzisha biashara zinazoweza kuwakomboa kiuchumi.


“katika halmashauri zetu kuna mikopo yenye unafuu na isiyo na riba kwa vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu, hembu tutumie fursa hiyo kujikomboa kiuchumi. Hiyo ndiyo mitaji inayotolewa na serikali”

 
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa UWT Iringa Mjini, Bi Ashura Jongo amewaasa wajasiriamali wote waliopokea mafunzo hayo kuyatumia kwa vitendo badala ya kuyaacha tu katika makaratasi yao kwa kuwa ni elimu yenye kuweza kuwasaidia kiuchumi.

Jongo amewataka wadau zaidi kujitokeza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na Vijana nchini ili kuwajengea uwezo wa kutambua fursa zilizopo pamoja na kuzitumia.

Nae mkurugenzi wa Kampuni ya Star, Danford Kesaga amesema ni kampuni yao iko tayari kusaidia makundi yote ya Watanzania katika kuwapatia elimu ya ujasiriamali kwa kuwa kufanya hivyo kutaongeza uzalishaji nchini katika nyanja tofauti.

Danford Kesaga ameeleza kufurahishwa kwake na muitikio wa makundi yote katika jamii ya mkoani Iringa, ambapo vijana pamoja ma wazee wameweza kuhudhuria mafunzo hayo yaliyofanyika kwa wiki moja kwa mafanikio makubwa. “maeneo mengi tulipeleka barua, na tunafuraha kuwa wengi wameitikia vizuri watu wamejitokeza kwa wingi na ni makundi yote yapo hapa”

Nao wajasiriamali waliopokea Mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata katika kipindi cha wiki moja ya mafunzo hayo kwa kuwa elimu hiyo itawasaidia katika kuendeleza shughuli zao za uzalishaji za kila siku.


“mafunzo tuliopata hapa ni mengi lakini yote yatatusaidia kuboresha shughuli zetu za kila siku tunazozifanya za kutuingizia kipato”

Aidha wameeleza elimu waliyoipata kuhusu kilimo biashara itawasaidia wengi kujiingiza katika kilimo cha baishara na kuachana na kilimo cha mazoea ambacho wengi wamekuwa wakipata hasara.


“elimu ya kilimo biashara itatusaidia kujiingiza katika kilimo chenye tija, sio kile tulichokuwa tunalima kabla ya kupata mafunzo haya ambacho kimsingi ni kupata hasara”

Previous articleARSENAL YAPOKEA KIPIGO KINGINE CHA 2-0 NA CHERSEA
Next articleHABARI KUU MAGAZETI YA LEO J.TATU AGOSTI 23-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here