Home LOCAL DKT. GWAJIMA APONGEZA MAENDELEO YA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA...

DKT. GWAJIMA APONGEZA MAENDELEO YA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA GEITA.

 

Na: WAMJW- Geita. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amepongeza maendeleo ya huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Dkt. Gwajima amesema hayo leo akiwa anaendelea na ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya kwa wananchi na shughuli za Maendeleo ya Jamii katika Mkoa wa Geita, iliyoanza katika mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza. 

“Nimefurahi, maagizo niliyotoa yametekelezwa hasa kwenye kitengo cha kuimarisha huduma za meno, niliagiza mumwamishe Mtaalamu kutoka Mbogwe, nafurahi kuona ujio wa Mtaalamu umeongeza huduma nyingine tisa mpya na kufanya huduma hizo kufikia 15 sasa na kubaki 4 tu ambazo zinazotokana na kukosekana kwa x-ray” amesema Dkt. Gwajima. 

Hata hivyo, Dkt. Gwajima ameagiza uongozi kuhakikisha ndani ya siku 30 inunuliwe mashine ya x-ray ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi mara moja, huku akisisitiza wafutilie barua kutoka MSD ili kuruhusiwa kupata kibali cha kununua mashine hiyo na kuanza huduma ndani ya siku 30.

“X-ray hiyo ambayo ukinunua kwa bei za kawaida ni milion tano, lakini ukienda MSD ni milion kumi na nane, mfuatilie hiyo barua ya MSD mwende mkanunue nyinyi wenyewe, uwezo wa hela sina mashaka nao, siku 30 muwe mshapata ili tuikomboe idara hii kukamilika” amesema. 

Aliendelea kusema kuwa, Kama msimamizi wa huduma za Afya Nimefurahi kuona huduma nyingine za magonjwa mengine zikiendelea kutolewa kwa ubora jambo ambalo linasaidia kupunguza malalamiko kwa wananchi kwa kiasi kikubwa. 

Aidha, Dkt. Gwajima ameagiza kuanza kujengwa kwa jengo la uzazi katika Hospitali hiyo litalosaidia wakina mama na watoto kupata huduma bora jambo litalosaidia kupunguza vifo vitakanavyo na uzazi kwa kiasi kikubwa ngazi ya Mkoa na taifa kwa ujumla. 

Aliendelea kusema kuwa, tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametenga kiasi cha shilingi Bilion 3.8 kwenye bajeti ya mwaka 2021-2022 kwaajili ya kumalizia kazi za nje, kujenga jengo la mama na mtoto na wodi katika jengo hilo ambalo tayari limefikia asilimia 95 ili kukamilika. 

Hata hivyo, amewaagiza viongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha wana ainisha vifaa tiba vyote kwani Serikali imeshatenga fedha kwaajili ya ununuzi wa vifaa hivyo vitavyotumika katika kutoa huduma za matibabu kwenye Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa. 

“Niagize, sasa andaeni mahitaji ya vifaa vyote vinavyohitajika, Nimefurahi kuona mashine za Maabara zinafanya kazi” amesema. 

Nimefurahi kuona mitambo ya hewa ya oksijeni tayari imefungwa, na baada ya wiki mbili Serikali italeta vifaa kwaajili ya kukinga hewa ya oksijeni na kuanza kusambaza katika maeneo mengine nchini, alisisitiza Dkt. Gwajima. 

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here