Home LOCAL WATUMIAJI HUDUMA ZA MTANDAO WASISITIZWA KUTUMIA VEMA FURSA ZA MTANDAO

WATUMIAJI HUDUMA ZA MTANDAO WASISITIZWA KUTUMIA VEMA FURSA ZA MTANDAO

Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul akizungumza katika kikao cha Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Dkt. Jabiri Bakari akimpa maelezo ya utendaji wa Mamlaka hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul wakati wa kikao na Menejimenti ya Mamlaka hiyo.

Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul akitembelea makumbusho ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alipotembelea Mamlaka hiyo.

·      Uteuzi Wajumbe wa Kamati ya Maudhui waiva

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imehimiza matumizi bora na salama ya mfumo wa Mtandao, ili kuhakikisha maudhui mtandaoni yanasalia kuwa yenye manufaa kwa watumiaji wote na kuhakikisha makosa ya uvunjifu wa sheria za mtandao yanapungua, watumiaji wamekumbushwa kutumia vema huduma hizo ili kuchagiza ukuaji wa uchumi na kuepuka matumizi ya mitandao yanayokiuka sheria za nchi, kanuni na maadili.

Akiwa katika ziara ya utendaji, alipotembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul alibainisha hayo na kuongeza kuwa matumizi sahihi na salama ya mitandao yatawezesha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo kwa watumiaji binafsi na kuiwezesha Serikali kuongeza tija katika maendeleo ya uchumi.

Katika ziara hiyo ambayo Naibu Waziri pia alipata fursa ya kujifunza namna Mamlaka hiyo inavyofanya kazi alitoa wito kwa vituo vya utangazaji wa redio na televisheni nchini kuhakikisha vinarusha maudhui yanayozingatia maadili ya kitaifa badala ya kuweka kipaumbele urushaji maudhui yasiyofaa  yanayotweza na kubomoa maadili na Utamaduni wa Jamii.

“TCRA tunashirikiana nao kwa upande wa Wizara yetu kuhakikisha kwamba maudhui ambayo yanapelekwa na vyombo vya Habari kwa wananchi yanakuwa sahihi lakini pia yanaangalia maadili ya Taifa letu. Nitoe tu rai kwa jamii, tunapotumia mitandao hii tutumie kwa namna ya kujenga na si kubomoa” alisisitiza Naibu Waziri.

Naibu Waziri pia, alihimiza umuhimu wa kuzingatia Sheria na Kanuni kwenye Sekta ya Utangazaji wa Redio na Televisheni, kwa ajili ya Umoja, Mshikamano na Maendeleo ya Nchi.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Gekul alipata fursa ya kupokea wasilisho juu ya utendaji kazi wa TCRA na kushauriana na Menejimenti ya TCRA juu ya masuala mtambuka yanayoangukia katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo Naibu Waziri alipokea Maelezo na kupata ufafanuzi namna Mamlaka hiyo inavyosimamia huduma za maudhui ya utangazaji na mtandaoni.

Akizungumzia Kamati ya Maudhui ambayo hufanya kazi na TCRA, Naibu Waziri amebainisha kuwa wajumbe wa Kamati hiyo watateuliwa hivi karibuni baada ya waliokuwa wakihudumu katika Kamati hiyo muda wao wa utumishi kutamatika.

“Kamati ile ya Maudhui muda wake ulikuwa umeisha lakini tumekubaliana ndani ya wiki ijayo Kamati wale wajumbe wawe wameshateuliwa na Mheshimiwa Waziri amelifanyia kazi hili jambo, kwa hiyo nimewahakikishia TCRA kwamba wasiwe na wasiwasi, hiyo Kamati ikiingia basi Waziri atakapokuwa amewateua wataendelea na kazi hiyo ya kudhibiti maudhui katika mitandao” alisema na kuongeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Kuwe Bakari alibainisha kuwa katika mitandao ya kijamii zimo fursa nyingi za maendeleo kwa ajili ya wananchi na Taifa na kuwatolea wito wananchi kuzitumia vilivyo fursa hizo ili kujinufaisha kiuchumi badala ya kutumia mitandao isivyopasa kinyume na Sheria za nchi.

“Kwa hiyo tunapoingia kwenye (cyber space) mtandaoni, ambayo ina nafasi kubwa sana ya kutengeneza ajira unaweza ukapata fursa ya biashara au kazi nzuri tu ya kufanya ukiwa ndani ya mtandao, badala ya kuingiza, kutengeneza au kuzungusha maudhui ambayo hayafai kwa Jamii”alisisitiza Kuwe.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Gekul alitembelea kituo cha Makumbusho ya Mawasiliano, Dawati la Huduma kwa Wateja wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano na Kituo cha Kufuatilia Maudhui.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here