Home LOCAL TAFITI ZA WADUDU WADHURIFU ZILETE MATOKEO CHANYA KWA TAIFA UDHIBITI WA MAGONJWA-DK.SUBI

TAFITI ZA WADUDU WADHURIFU ZILETE MATOKEO CHANYA KWA TAIFA UDHIBITI WA MAGONJWA-DK.SUBI


Na.WaMJW,Dar es Salaam.

Serikali imeagiza tafiti mbalimbali za kitaalamu zinazofanywa kuangazia wadudu wadhurifu zisiishie kwenye makaratasi bali zilete matokeo chanya kwa Taifa katika kukabili na kudhibiti magonjwa yaenezwayo na wadudu hao.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Leonard Subi alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha kamati ya Kitaifa ya masuala ya wadudu wadhurifu.

“Tunataka tafiti na shule zao wazitafsiri katika utekelezaji wa kuondosha kero na adha kwa wananchi, haya maradhi yaondoke,” amesema.

Dkt. Subi amebainisha baadhi ya aina za wadudu wadhurifu wanaosababisha magonjwa mbalimbali kwa binadamu ni pamoja na mbu, nzi, mbung’o, kupe na wengineo.

Amesema wadudu hao hueneza magonjwa kama vile dengue, malaria, malale, matende na mabusha, vikope, usubi na mengineyo.

Ameitaka Kamati hiyo, pamoja na kukaa ngazi ya Taifa, waangalie pia ngazi ya mikoa, hata baadhi ya vikao vyao waende ‘field’ kutazama hali halisi na kuwashirikisha viongozi waandamizi katika eneo husika kile walichobaini ili wachukuwe hatua dhidi ya magonjwa hayo

“Tunakuwa na miradi mingi, nataka kila mradi ufuatiliwe, mara nyingi huwa tunaandika, tunakubaliana MOU lakini utekelezaji wa ule mradi tunataka tujue shilingi ngapi zilitengwa, ngapi zililetwa katika robo husika, zimetumika na shughuli ngapi zimefanyika.

“Kwa mfano vyandarua vimegawiwa kwa watu wangapi na nani?. Kwa hiyo, kama wataalamu ni lazima tuwe na kamati maalum ya kufuatilia utekelezaji wa afua na miradi mbalimbali ambayo Serikali tumesaini na wadau mbalimbali,” ameagiza.

Ameongeza “Kuna miradi ya kupulizia ukoko tulianza na wilaya 18 sasa tupo wilaya sita, angalieni jinsi gani tutaweza kutumia rasilimali tulizonazo Tanzania kuweza kubadilisha mifumo.

“Kwa mfano sasa hivi Tanzania tunazalisha mimea ambayo inatengeneza dawa ya ALu tunapeleka nje ya nchi, mtueleze ni nini tutakifanya ili tuweze kutengeneza dawa hii ndani ya nchini.

“Tunanunua vitendanishi vya kupimia ugonjwa wa malaria kutoka nje ya nchi kama wanasayansi watafiti na wasomi je… Sisi hatuwezi kutengeneza vitendanishi vya namna hiyo?

“Kwa sababu kama sayansi na teknolojia ya molecular sasa Tanzania ipo, mtueleze mnakwama wapi tuweze kutengeneza vitendanishi vya kupimia ugonjwa wa malaria wenyewe.

Dkt. Subi amesisitiza “Hadubini tunazo lakini tunataka twende katika ‘level’ kubwa ya ‘molecular technology’.

Amewahimiza Wanasayansi hao wasikae tu kuandika bali wafikirie ili Taifa liweze kufanya mageuzi katika nyanja hiyo.

“Tuweze ku-transform mambo kama yale ambayo yako ndani, tuna mimea mingi ila bado tunanunua madukani dawa za kupuliza ndani ili kuua mbu.

“Je mwananchi ataweza hizi, mtuambie ni mimea gani ambayo mwananchi kama anataka kuua mbu kule kijikini akipuliza au akichoma mule ndani kwa dakika 15 mbu wote walioko mule ndani ule moshi uwaue.

“Mtuambie ni mimea gani ambayo itakuwa salama kwa Afya za binadamu na itumikeje,” amesema.

Dkk. Subi amesema Serikali inataka watafiti hao wabobezi waje na vitu vya ubunifu wa kisayansi ambavyo havitakuwa na madhara.

“Kwa sababu yapo mambo ambayo tafiti za Tanzania, wasomi wa Tanzania wamefanya, kwa mfano ule wa uvumbuzi wa vyandarua vya PBO Net ambayo inatengeneza Arusha.

“Tafiti za kisayansi zilifanyika hapa ikiwamo Taasisi yetu ya magonjwa ya binadamu NIMR, sasa mtuambie ni namna gani haya tutayafanya,” amesisitiza.

Ameongeza “Hiki kikao ni cha muhimu sana na ndiyo maana binafsi kama Mkurugenzi wa Kinga, ninataka vikao vyenye matokeo chanya kwa wananchi na Serikali,

“Tulitengeneza Mpango Mkakati wa Kupambana na Wadudu Wadhurifu mnapokaa basi mu- evaluate kwamba katika utekelezaji wa Mpango mkakati tuliouandika tuna-utekekezaje.

“Maana ndani ya mkakati ule kukikuwa na viuatilifu, hizi dawa tutakazotumia ni aina gani, zitakuwa na madhara gani, zitumikeje tunataka ‘mu-evaluate into reality’,” ameagiza.

Akizungumza, Msimamizi wa Kitengo kinachosimamia Udhibiti wa Magonjwa katika Wizara Charles Mwalimu amesema wamepokea maelekezo hayo na kwamba watayafanyia kazi ipasavyo.

“Tupo na watafiti kwenye kikao hiki, tumepokea maelekezo ikiwamo hili la kuhakikisha tunatafuta mbinu ya kuangamiza mbu kwa kutumia njia za jadi kama majani ambayo yanaweza kutumia kufukuza mbu,” amesema.

Ameongeza “Kikao hiki lengo lake kubwa ni kuishauri Serikali ni jinsi gani bora ya kupambana na wadudu wanaoeneza magonjwa.

“Kikao cha leo tumetekeleza maazimio mbalimbali ikiwamo kuangalia jinsi gani bora kuhakikisha tunatekeleza hii afua ya kuangamiza mazalia ya mbu lakini vile vile usambazaji wa vyandarua kwenye kaya.

Amesema wameazimia kuangalia pia jinsi gani ya kuviteketeza vinavyotumika ngazi ya kaya baada ya muda kuisha.

Previous articleMAKAMU WA RAIS ASHIRIKI MISA YA KUMBUKIZI YA HAYATI MKAPA
Next articleTIMU YA AZAM FC YAWAONDOA KIKOSINI WACHEZAJI WANNE WA KIMATAIFA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here