Home LOCAL RAIS SAMIA KUZINDUA RASMI ZOEZI LA UTOAJI WA CHANJO DHIDI YA UVIKO-19...

RAIS SAMIA KUZINDUA RASMI ZOEZI LA UTOAJI WA CHANJO DHIDI YA UVIKO-19 (COVID-19) JULAI 28, 2021 IKULU DSM.

 

 DAR ES SALAAM.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi zoezi la chanjo ya Uviko 19 utakaofanyika Julai 28, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Mheshimiwa Rais atachanjwa.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima  ameleeza kuwa zoezi hilo litaanza majira ya saa 3 Asubuhi ambapo baada ya uzinduzi huo Wizara ya Afya itaendelea na taratibu zingine za usambazaji wa chanjo hiyo na kutoa utaratibu wa utoaji wa chanjo katika Mikoa yote.

“Uzinduzi wa zoezi la uchanjaji unaweka historia kwa Taifa letu katika kuendeleza mapambano dhidi ya UVIKO-19 ikiwa ni nyongeza mahususi ya afua zinginezo za chanjo ikiwemo unawaji mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, uvaaji wa barakoa katika maeneo hatarishi, ufanyaji wa mazoezi na upataji wa lishe bora na matumizi ya tiba asili zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili”

“Utoaji wa chanjo ni moja ya afua muhimu na inayoaminika Duniani kote katika kupambana na maradhi hususani ya kuambukiza ikiwemo ugonjwa wa UVIKO-19 hivyo watanzania tutumie fursa hii muhimu” Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha Dkt. Gwajima ameongeza kuwa mara baada ya uzinduzi wa zoezi hilo Serikali inatarajia kuendelea kupokea chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanachanja.

“Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto inatoa Pongezi na Shukrani za Dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mfano na kuongoza njia katika zoezi hilo muhimu” 

Aidha Wizara imeendelea kutoa wito kwa viongozi wengine wote kuiga mfano huo na kuonesha njia kwa wananchi wote katika kupata huduma ya chanjo hii ya kujikinga na UVIKO 19 kwa hiari na bila malipo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here