Home LOCAL OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR, MEYA JIJI LA ZANZIBAR...

OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR, MEYA JIJI LA ZANZIBAR KUSHIRIKIANA KUIRUDISHA ZANZIBAR KWENYE HADHI YAKE.


ZANZIBAR.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Ofisi yake ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Meya wa Jiji la Zanzibar ili kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake.
 
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo (Julai 27) alipokutana na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mhe. Mahmoud Mohamed Musa, pamoja na ujumbe wake uliofika ofisini kwake  Migombani Mjini Unguja.
 
“Watu kutoka maeneo mbalimbali, yakiwemo Afrika ya Magharibi, walikuwa wakija Zanzibar kwa lengo la kujifunza namna ya kupanga mji, lakini kwa bahati mbaya sana kwa sasa Zanzibar imepoteza sifa hiyo,” alisema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais.
 
Aidha, Mheshimiwa Othman amemuahidi Meya wa Jiji la Zanzibar kwamba ofisi yake itatoa ushirikiano katika kuirudisha haiba ya Mji wa Zanzibar.
 
 “Tupo tayari na tutaungana nanyi sio tu katika kuweka mazingira ya jiji la Zanzibar kuwa safi bali tutatoa msaada zaidi hata  kuirudisha Zanzibar  katika uzuri na haiba yake,” aliahidi Mheshimiwa Othman.
 
Meya huyo aliyefika kwa Makamu wa Kwanza kwa ajili ya kusalimia na kubadilishana mawazo, awali alikukutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Saada Salum Mkuya, na Katibu Mkuu wake, Mhe. Khadija Khamis, pamoja na Watendaji wa Ofisi hiyo.
 
Mhe. Othman amesema Ofisi yake itatoa ushirikiano wa dhati kwani taasisi hizi za Serikali zitafanikiwa zaidi zitakapokuwa na uzalendo wa kusaidiana katika kufikia malengo yake, kwani kuna muingiliano mkubwa wa majukumu hasa idara ambazo zipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kama vile idara ya Mazingira, Idara ya Watu Wenye Ulemavu, Tume ya Ukimwi na Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya.
 
Mhe. Mkuya amemueleza Makamu wa Kwanza yakwamba, awali kikao chao na Meya huyo wa Jiji kimeonesha mustakbali mwema kuelekea katika mashirikiano,jambo ambalo litaifanya Zanzibar kuwepo katika muonekano bora zaidi.

Naye Meya wa jiji la Zanzibar, Mhe. Mahmoud, alimshukuru Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa nasaha zake pamoja na kuahidi kuitumia vyema fursa ya mashirikiano kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza ili kufikia malengo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.  Hussein Ali Mwinyi, ya kuufanya  mji wa Zanzibar kuwa safi kwa kiwango kinachotakiwa.

Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here