Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akipanda mti nyumbani kwa Hayati Benjamin William Mkapa mara baada ya kukamilika kwa misa ya kumbukizi yam waka mmoja wa kifo cha Hayati Benjamin William Mkapa, Julai 24,2021.
PICHA – OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango, leo Julai 24, 2021 ameshiriki misa ya kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha hayati Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa iliofanyika Kijiji cha Lupaso Wilaya ya Masasi.
Akizungumza baada ya misa hiyo, Makamu wa Rais amesema mchango wa hayati Benjamin Mkapa kwenye mageuzi ya kiuchumi; mapambano dhidi ya rushwa ambayo yalipelekea watanzania kumpa jina la “Bwana Msafi”; mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi; kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa Umma; na usuluhishi wa migogoro ya kisiasa katika nchi za DRC, Burundi, Kenya kamwe hautafutika.
Makamu wa Rais amesema viongozi wanajifunza kutoka kwa Hayati Benjamin William Mkapa ujasiri na uthubutu wake katika kufanya maamuzi magumu kwa manufaa ya Taifa. Aidha amesema hayati Mkapa ameacha alama ya umuhimu wa kuwajibika na kusimamia misingi ya haki na usawa katika kuwahudumia wananchi wote.
Aidha Makamu wa Rais amesema Hayati Benjamin William Mkapa alitambua kwamba Utegemezi una hatari nyingi na hivyo ni lazima kujizatiti kujitegemea kama nchi. Alisema hatima ya Tanzania na Afrika iko mikononi mwa watanzania na Waafrika wenyewe. Na alihimiza muda wote kwamba wajibu wa kwanza ni kutatua matatizo ya nchi yetu na ya bara letu la Afrika wenyewe iwe ni matatizo ya kijamii, kisiasa au kiuchumi ili kukuza ustawi wa Taifa na bara zima.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Korona ambao umeingia katika wimbi la tatu lililo hatari Zaidi. Amewasihi viongozi wa dini pamoja na waumini wa dini zote kumwomba Mungu msamaha ili afukuze ugonjwa huu duniani ili watu wake wamtukuze na kumwabudu kwa furaha na amani bila hofu ya KORONA. Aidha amewaomba viongozi wa dini na watanzania wote kuendelea kuiombea nchi amani na kuwaombea viongozi wa Serikali hekima itokayo kwa Mungu mwenyezi ili kuongoza taifa kwa ufanisi.
Akitoa mahubiri katika misa hiyo, Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo amesema watanzania wanatakiwa kuendelea kumuombea Hayati Benjamin Mkapa na kuyaenzi yale yote mema alioyafanya akiwa duniani.
Kwa upande wake msemaji wa familia ya Hayati Bnjamin Mkapa bwana William Urio amesema Hayati Mkapa aliilinda imani ya dini yake wakati wote wa Maisha yake na kumtanguliza Mungu katika shughuli zake zote. Aidha ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaunga mkono katika kufanikisha shughuli ya kumaliza msiba wa Hayati Benjamin Mkapa.