Home Uncategorized MAKALA TAASISI YA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI ANGLIKANA MT, AUGUSTINE SAMIHAS MUHEZA...

MAKALA TAASISI YA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI ANGLIKANA MT, AUGUSTINE SAMIHAS MUHEZA MKOANI TANGA

 

Na: Maiko Luoga, TANGA.

Katika kuandaa Wataalamu wenye ujuzi na maarifa Taasisi ya Afya na Sayansi shirikishi SAMIHAS iliyopo chini ya Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga, imeendelea kuimarisha mfumo wa kutoa mafunzo kwa Wanafunzi wanaosoma katika Taasisi hiyo iliyopo ndani ya Hospital teule ya Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.

Canon Edward Komba Naibu Mkurugenzi mipango fedha na utawala katika Taasisi hiyo amesema, Tasisi inatoa kozi tatu za Utabibu, uuguzi na Maendeleo ya jamii kwa ngazi ya cheti na Diploma, kwa kuzingatia utaratibu wa NACTE, lengo likiwa kuisaidia Serikali kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kulitumikia Taifa.

“Tangu mwaka 1939 ilipoanzishwa na Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga, Taasisi hii imezalisha Wataalamu wengi wa Afya ambao wamesambaa nchi nzima ikiwemo Hospital zetu kubwa zilizopo nchini, ukifika huko lazima utaonana na wataalamu waliozalishwa na Taasisi hii ya Afya SAMIHAS” alisema Canon Edward Komba.

Bi, Jamila Mpandi mwalimu wa Taasisi hiyo na Bw, Lawrence Mbezi muuguzi mkuu katika Hospital teule Mt, Augustine Wilaya ya Muheza ni miongoni mwa Wanafunzi waliozalishwa na Taasisi hiyo miaka kadhaa iliyopita, wamesema Taasisi imewapa maarifa na ujuzi katika maisha yao sasa wanaendelea kulitumikia Taifa huku wakitoa wito kwa jamii kuitumia Taasisi hiyo yenye historia kubwa nchini.

“Kidini mimi ni muislamu lakini nimeishi na Taasisi hii tangu nilipojiunga nayo mwaka 1998 na 1999 ilipokuwa ikiitwa Muheza Nursing School nikiwa mwanafunzi kisha niliajiriwa na Kanisa Anglikana kama muuguzi mkunga katika Hospital Teule ya Wilaya ya Muheza, baadae Kanisa likanipeleka katika mafunzo ya ualimu hadi sasa nafundisha hapa” alieleza Bi, Jamila Mpandi.

“Naifahamu vema Taasisi hii imetoa wataalamu wengi nikiwemo mimi, faida kubwa wanayoipata wanafunzi wetu hapa ni kufanya mazoezi kwa vitendo katika Hospital teule ya Wilaya ya Muheza ambayo inaushirikiano mkubwa na Taasisi hii, kwakuwa zote zipo chini ya Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga” alieleza Bw, Lawrence Mbezi.

Bi. Sophia Ngayoma mkuu wa idara ya uuguzi na Dkt, Obrey Maonga Mkuu wa idara ya utabibu Taasisi ya Afya na sayansi shirikishi SAMIHAS Mkoani Tanga wametumia nafasi hiyo kuwaalika watanzanania wenye Vijana wanaotafuta vyuo kujiunga na Taasisi hiyo ya afya kwakuwa inauzoefu na uwezo mkubwa wa kutimiza ndoto zao.

“Kupitia idara zetu tumejipanga kuhakikisha tunatoa elimu bora kwa jamii ili Wanafunzi wanaojiunga nasi wasijute kujumuika na Taasisi hii, wale wanaokuja kusoma masomo ya sayansi sifa ni ufaulu wa alama D katika masomo ya Kemia, Fizikia, Baolojia na Hesabu tunampokea” Dkt, Obrey Maonga.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika Taasisi hiyo akiwemo Bw, Shaban Mohamed na Bi, Vaileth Kinanga wamesema mazingira ya Chuo hicho yanapendeza hivyo ni fursa kwao kujifunza na walimu kufundisha na Bw, Mohamed Yusuph Mohamed anavutiwa kusoma katika Taasisi hiyo kwakuwa haina itikadi ya dini licha ya kuwa chini ya umiliki wa Kanisa Anglikana.

“Jambo la kufurahisha Chuo hiki kipo karibu na Hospital kubwa Teule ya Wilaya ya Muheza hapa mkoani Tanga baada ya kumaliza vipindi Darasani tunaenda kujifunza kwa vitendo katika Hospital hatua hii inatujengea uwezo na ujuzi kwa haraka” walieleza wanafunzi hao. 

Bi, Khadija Daud mwalimu wa masomo ya sayansi katika Chuo hicho amesema kabla ya kwenda kufanya mazoezi ya vitendo katika Hospital teule ya Wilaya ya Muheza wanafunzi hupita katika chumba cha mazoezi ambacho kina vifaa vyenye mfano wa mwili wa binadamu hutumika kuwapa uzoefu kabla ya kuanza kutibu wagonjwa.

“Hapa tulipo ni chumba maalumu cha mafunzo (Skill Larb) kwaajili ya wanafunzi wanaojifunza hatua tofauti kabla ya kwenda mawodini kufanya kazi kamili kwa wagonjwa, leo tunatumia mfano huu wa binadamu kupima presha ili wakienda kwa mgonjwa wanajua cha kufanya” alieleza mwalimu Khadija Daud.

Bi, Grace Makoko mkazi wa Muheza Mjini amesema uwepo wa Taasisi hiyo katika eneo lao imesaidia kuongeza idadi ya Vijana wenye elimu pamoja na kufungua fursa za uchumi kwao kwakuwa wameanzisha biashara kuzunguka Taasisi hiyo ikiwemo biashara za chakula.

“Uwepo wa Chuo hiki sisi jamii tumefurahi kwakuwa kinasaidia kuwaleta vijana wetu katika eneo la karibu na nyumbani pia ulipaji wa ada zao hauna usumbufu, tunalipa kwa awamu nne kwa mwaka pia tunafanya biashara kwakuwa hii ni Taasisi kubwa” alisema Bi, Grace Makoko mkazi wa Muheza mkoani Tanga.

Mwisho.

Previous articleMHE. RAIS SAMIA APOKEA TAARIFA YA UKAGUZI MAALUM YA MATUMIZI YA FEDHA ZILIZOTOLEWA NA BENKI KUU BOT PAMOJA NA TAARIFA YA SENSA YA WATU NA MAKAZI INAYOTARAJIWA KUFANYIKA MWEZI AGOST 2022
Next articleMAGAZETI YA LEO IJUMAA JULAI 2-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here