Afisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti Iginas Maembe wa pili (Kushoto)akikata utepe wa kuzindua Kituo cha Polisi Jamii Mtaa wa Amani Kata ya Liwiti Leo Julai 25/2021 (kulia)Mkuu wa Polisi TABATA SP Colle Senkondo na Mwenyekiti wa Serikali Amani Grace Mwingira na Viongozi wa chama(PICHA NA HERI SHAABAN). |
Polisi Jamii Mtaa wa Amani Kata ya Liwiti wakiwa katika mazoezi Dar es Salaam Leo Julai 25/2021 Wakati wa kuzindua Kituo cha Polisi kitakachoimalisha ulinzi katika Kata hiyo (PICHA NA HERI SHAABAN) |
NA: KHERI SHAABAN (ILALA)
Kituo hicho cha Polisi Jamii kimefunguliwa Dar es Salaam Leo na Afisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti IGINAS MAEMBE na Makanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam na Mkuu wa Polisi TABATA.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kuzindua Kituo hicho katika Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Liwiti Afisa Mtendaji Iginas Maembe alisema kujengwa kwa Kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa Walinzi wa Mtaa huo watashirikiana na Jeshi la Polisi katika kuimalisha Ulinzi kila siku.
Ignas Maembe, amekipongeza kikundi hicho na kuwataka wananchi kukitumia vizuri ili kukomesha vitendo vya uhalifu kwenye maeneo yao.
“Tunaunga mkono jitihada za Mkuu wa Jeshi la Polisi hasa katika jukumu la ulinzi, sisi tunatekeleza maelekezo yake na tuna imani ulinzi utaimarika zaidi,” alisema Maembe.
Naye Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata Mkaguzi wa Polisi, Colle Senkondo, alisema kupitia kituo hicho wahalifu watapatikana kwa urahisi na suala zima la uhalifu litapungua kama si kuisha kabisa.
“Uzinduzi wa kituo hiki ni faraja kwetu kwa sababu sisi kama polisi hatutoshi bila kushirikiana na wananchi.
Kupitia kituo hiki watatusaidia kwa kuwa hawa wako karibu na wananchi na huko ndiko ambako wahalifu wanapatikana,” amesema Senkondo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Grace Mwingira, amewataka wananchi kulipa ada za ulinzi shirikishi kwa wakati ili kuwatia moyo vijana hao.
Amesema kila kaya huchangia Sh 3,000 kwa mwezi kwa ajili ya tozo ya Ulinzi .
“Wakati naomba kura kwa wananchi nilisema mtaa huu unasumbua kuhusu vibaka lakini nitahakikisha unakuwa na amani kama jina lake lilivyo, sasa hivi tunalala bila matatizo yoyote,” amesema Mwingira.
Kamanda wa Ulinzi Shirikishi Mtaa wa Amani, Erick Massawe, amesema uhalifu umepungua hasa eneo la Ladwa na kwamba wameshirikiana na polisi kuondoa vijiwe vyote vya bangi, dawa za kulevya na gongo.
Hata hivyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile kutokuwa na vifaa vya kutosha yaani pingu, tochi, filimbi, virungu, sare na usafiri wa kupeleka wahalifu kituoni.
Kikundi hicho chenye vijana 31 kina miaka miwili tangu kianzishwe huku wakimshukuru mama Joseph Shola na familia yake kwa kukubali kutoa jengo lake kuwa ofisi ya polisi jamii.
Mwisho.