Home LOCAL WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AJADILI FAIDA ZA MKATABA WA AfCFTA NA...

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AJADILI FAIDA ZA MKATABA WA AfCFTA NA KATIBU MKUU MTENDAJI WA SEKRETARIETI YA AFCFTA

DAR ES SALAAM.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo  (MB) amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Mtendaji wa  Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Wamikele Mene ambaye yupo hapa nchini kufanya mikutano mbalimbali yenye lengo la kuonesha faida zinazoweza kupatikana kwa Tanzania kujiunga na mpango huo.

Akizungumzia ziara hiyo Waziri Kitila Mkumbo amesema kwa sasa wanafanya mikutano ya kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili kujenga uelewa kwa wafanyabiashara kufahamu fursa zinazoweza kupatika kwa Tanzania kujiunga na AfCFTA.

Prof Mkumbo amesema suala la Tanzania kurudhia kujiunga na AfCFTA lipo chini ya Bunge lakini kwa sasa wizara hiyo inatoa elimu kuhusiana na faida za kujiunga na soko hilo ikiwemo upatikanaji wa ajira, ukuaji wa biashara na soko kubwa lenye watu takribani bilioni 1.2.

Mkataba huo unatoa fursa ya nchi za Afrika kuwa na nguvu ya pamoja katika kuhimili ushindani wa bidhaa zake katika soko la dunia hivyo kukuza uchumi na kuondoa umasikini miongoni mwa wananchi wake. Amesema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Mtendaji wa AfCFTA Wamikele Mene amesema, faida zinazopatikana katika soko hilo ni kubwa na linatoa fursa kwa watanzania kuuza bidhaa zao kwenye soko kubwa la Afrika, kuongeza ajira hasa kwa vijana na wanawake.

Aidha baada ya Mazungumzo hayo  Waziri wa Viwanda na Biashara akiambatana na Katibu  Mkuu Mtendaji wa AfCFTA walihudhuria warsha ya majadiliano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa lengo la kutoa elimu na kupata maoni ya wananfunzi hao  juu ya faida za Tanzania kuridhia kujiunga na Mkataba.

Akiongea na wanafunzi hao, Katibu Mkuu Mtendaji wa AfCFTA amesema utekelezaji wa mkataba huo umegawanyika katika makundi matatu ili kuwezesha biashara kwa wingi na kukuza biashara ndani ya Bara la Afrika. Kundi la kwanza ni ufunguaji/uondoaji wa kodi kwenye bidhaa kwa asilimia 90 ndani ya kipindi cha miaka 10,  Kundi la pili ni undoaji wa kodi kwa asilimia 7 ya bidhaa katika kipindi cha miaka 13 toka kuanza ufunguaji na Kundi la mwisho ni asilimia 3 ya bidhaa ambazo hazitofunguliwa kabisa.

Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuridhia Mkataba huo ambao hadi sasa nchi 38 kati ya nchi 54 za Umoja wa Afrika zimeridhia na mkataba huo.  Tanzania inatarajia kunufaika na kutumia fursa zote za kibiashara zitakazotokana na Mkataba huo.

Previous articleRAIS SAMIA AZUNGUMZA NA WAHARIRI NA WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI IKULU JIJINI DAR.
Next articleRC MAKALLA AFURAHIA KUPOKEA MABASI 70 KATIKA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here