Home LOCAL WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA 20

WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA 20

DODOMA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi magari ya wagonjwa 20 yenye thamani ya sh. bilioni 2.24 ambayo yatapelekwa kwenye vituo vya afya 13, hospitali za halmashauri tano, ya wilaya moja na ya rufaa ya mkoa moja katika mikoa 17.

Akikabidhi magari hayo leo (Jumanne, Juni mosi, 2021) katika hafla fupi iliyofanyika Ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zitenge fedha za matengenezo (motor vehicle services) ili kuhakikisha magari hayo yanadumu kwa muda mrefu zaidi.

“Iko tabia katika baadhi ya Halmashauri kutosimamia haya magari kwa maana ya kutotenga fedha za kuyafanyia service kila inapotakiwa. Lazima gari lihudumiwe ili litumike kwa muda mrefu zaidi,” amesema.

Amewaomba Wabunge waliopokea magari hayo wakayasimamie ili yatoe huduma inayotarajiwa kwa wananchi. “Msisite kuyaeleza haya masuala kwenye mabaraza ya madiwani ili wahusika wazingatie jukumu la kuyatunza,” amesisitiza

Amesema mwaka jana alikabidhi magari 50 ya kubebea wagonjwa kati ya 70 yaliyokuwa yamepangwa kutolewa ili kuboresha huduma za afya nchini.

“Mhehishimwa Rais Samia ameridhia magari haya yatolewe na yaende yakatoe huduma kwa wananchi. Pia ameridhia hospitali za mikoa na wilaya ziwe na magari ya kubeba wagonjwa na kuwaleta kwenye huduma kwa haraka.”

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu ninatoa shukrani za dhati kwa ufadhili huu wa magari haya ambayo yatatumika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na Wabunge waliofika kupokea magari hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima alisema magari hayo 20, yatapelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, hospitali ya wilaya ya Masasi, hospitali za halmashauri tano na kwenye vituo vya afya 13. 

Alisema magari mitano yamepelekwa kwenye hospitali za Halmashauri za Mkalama (Singida), Ngorongoro (Arusha), Chunya (Mbeya), Buhigwe (Kigoma) na Nyamwaga iliyoko Tarime mkoani Mara.

Amevitaja vituo vya afya 13 vilivyopatiwa magari ni cha Kifanya (Njombe Mjini), Bwina (Chato), Iyula (Mbozi), Lubanda (Ileje), Kibaoni (Kilombero), Nakapanya (Tunduru Kaskazini), Kilongwe (Mafia) na Bwisya (Ukerewe). Vingine ni Kibutuka (Liwale), Nalasi (Tunduru Kusini), Mlete (Songea Mjini), Kambi ya Simba (Karatu) na Mnazi (Lushoto).

Previous articleWATAALEM SEKTA YA MANUNUZI WAASHWA KUWA WAADILIFU.
Next articleBUNGE LAPITISHA ZAIDI YA SH.BILIONI 54 YA WIZARA YA HABARI KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here