Home LOCAL WAZIRI DKT. NCHEMBA AWASILISHA BUNGENI TAARIFA ZA HALI YA UCHUMI NA...

WAZIRI DKT. NCHEMBA AWASILISHA BUNGENI TAARIFA ZA HALI YA UCHUMI NA MPANGO WA MAENDELEO

Waziri wa Fedha na Mipnago Mhe.Dkt.Mwigulu Nche,ba akiwasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi na Taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.

UTANGULIZI.

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22. Pamoja na hotuba hii, nawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22. Taarifa hizo ndiyo msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 nitakayowasilisha katika Bunge hili Tukufu leo alasiri.
  1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kukutana kwa mara nyingine katika Bunge hili baada ya majadiliano ya bajeti za mafungu mbalimbali. Mkutano huu wa Tatu wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu katika kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu. 
  1. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena, nitumie fursa hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwako wewe Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wote, Chama cha Mapinduzi na Watanzania wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi, Amina. Aidha, nitoe pole kwa Taifa kwa kuondokewa na Viongozi Wakuu, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Balozi Mhandisi John Kijazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi. Amina.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu kuapishwa kwake tumeshuhudia namna anavyoendelea kuliongoza Taifa letu kwa busara, hekima, weledi na umahiri mkubwa na kuendeleza mashirikiano na nchi mbalimbali. Aidha, niungane na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu, ujasiri na afya njema ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi wake kikamilifu. 
  1. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nampongeza Mhe. Othman Masoud Othman Sharif kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, natoa pongezi kwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuaminiwa na Mhe. Rais kuendelea kuwatumikia watanzania katika wadhifa wake wa Waziri Mkuu.
  1. Mheshimiwa Spika, kipekee natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais na Watanzania wote kuwa nitatekeleza jukumu hili kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo wa kiwango cha hali ya juu. 
  1. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na athari za UVIKO-19. Athari hizo zimesababisha kushuka kwa shughuli za kiuchumi duniani, ikiwemo uzalishaji, biashara, sanaa na burudani, utalii na usafirishaji wa bidhaa. Katika kukabaliana na athari hizo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa biashara duniani ili kutumia fursa zitokanazo na athari za UVIKO-19 kwa manufaa mapana ya Taifa na kuendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa na ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya.
  1. Mheshimiwa Spika, Taarifa za Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 zimezingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa wadau katika hatua za uandaaji na maamuzi katika ngazi zote serikalini. Ni vigumu kuwataja wadau wote waliotoa maoni na ushauri hadi kufikia hapa, lakini ni vyema nitambue mchango mkubwa wa Bunge lako Tukufu chini ya uongozi wako Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Sillo Daniel Baran (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na wajumbe wote wa Kamati kwa ushauri makini waliotupatia. Uandaaji wa taarifa nilizowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu umenufaika kwa kiasi kikubwa na mchango, ushauri na busara za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti. 
  1. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 imeandaliwa kwa kuzingatia mwenendo wa viashiria vya uchumi jumla na sekta mbalimbali kwa mwaka husika, ikilinganishwa na mwaka 2019. Aidha, maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 yamezingatia vipaumbele vya Serikali vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akilihutubia rasmi Bunge hili la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021. Aidha, Mpango umezingatia Sera na Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050; Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Vilevile, Mpango huu umeandaliwa kwa kuzingatia misingi ya mipango ya awali iliyolenga kuimarisha na kukuza uchumi fungamanishi, jumuishi na shindani unaohimili utandawazi. Katika kutekeleza Mpango wa mwaka 2021/22, msukumo mkubwa utawekwa katika kuliwezesha Taifa letu kutumia kikamilifu fursa zilizopo ili kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2020

Uchumi wa Dunia

  1. Mheshimiwa Spika, taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2021 inaonesha kuwa, mwaka 2020, dunia ilikuwa na mdororo wa uchumi kwa kupata ukuaji hasi wa asilimia 3.3 ikilinganishwa na ukuaji chanya wa asilimia 2.8 mwaka 2019. Ukuaji hasi ulisababishwa na kupungua kwa shughuli za kiuchumi duniani hususan, biashara, usafirishaji na utalii kutokana na mlipuko wa UVIKO-19. Hata hivyo, uchumi wa dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6.0 mwaka 2021 na asilimia 4.4 mwaka 2022. Hii inatokana na matarajio ya kurejea kwa shughuli za kiuchumi kutokana na kuendelea kusambazwa kwa chanjo ya UVIKO-19 na hatua za kuinua chumi zinazochukuliwa na nchi mbalimbali.

Uchumi wa Afrika na Kikanda

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2020, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zilikuwa na ukuaji hasi wa uchumi wa wastani wa asilimia 1.9, ikilinganishwa na ukuaji chanya wa wastani wa asilimia 3.2 mwaka 2019. Mdororo wa uchumi katika baadhi ya nchi  ulitokana na athari ya zuio la  baadhi ya  shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwa ni njia ya kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19. Aidha, zuio la baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii lilisababisha kushuka kwa mauzo ya bidhaa nje ya kanda na kupungua kwa shughuli za utalii. Ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara  unatarajiwa kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2021 na asilimia 4.0 mwaka 2022.
  1. Mheshimiwa Spika, Nchi zinazotegemea utalii kama chanzo kikubwa cha ukuaji wa uchumi zikiwemo Carpe Verde na Mauritius na zile zinazotegemea mafuta (Angola, Cameroon, Chad, Congo, Jamhuri ya Guinea, Gabon, Nigeria na Sudan ya Kusini) zilipata athari kubwa kutokana na UVIKO-19 na kuchangia ukuaji hasi wa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa ujumla mwaka 2020, nchi 32 kati ya nchi 45 za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara zilikuwa na ukuaji hasi wa uchumi sawa na asilimia 71.1 ya nchi zote, nchi mbili zilikuwa na ukuaji wa asilimia sifuri (0) na nchi kumi na moja (11) ikiwemo Tanzania zilikuwa na ukuaji chanya wa uchumi.

Uchumi wa Taifa

Pato la Taifa

  1. Mheshimiwa Spika, licha ya mlipuko wa UVIKO-19 ulioathiri uchumi wa nchi nyingi duniani, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji chanya wa uchumi kwa mwaka 2020. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2019. Ukuaji chanya ulitokana na hatua ya Serikali ya kuruhusu shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea na wakati huohuo wananchi wakisisitizwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya. Aidha, kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini kulichangiwa na athari za UVIKO-19 katika nchi washirika wa kibiashara pamoja na mafuriko  yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.
  1. Mheshimiwa Spika, athari za janga la UVIKO-19 zilijitokeza zaidi katika shughuli za kiuchumi za malazi,  huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi kwa mwaka 2020. Sekta zilizokua kwa viwango vya juu kwa mwaka 2020 ni pamoja na: Sekta ya Ujenzi  (asilimia 9.1); Habari na Mawasiliano (asilimia 8.4); Uchukuzi na Uhifadhi wa Mizigo (asilimia 8.4); Huduma zinazohusiana na Utawala (asilimia 7.8); Shughuli za Kitaalamu, Sayansi na Ufundi (asilimia 7.3); Madini na Mawe (asilimia 6.7); na Afya na Huduma za Jamii (asilimia 6.5).
  1. Mheshimiwa Spika, Pato ghafi la Taifa lililozalishwa nchini lilikuwa shilingi trilioni 148.5 mwaka 2020, ikilinganishwa na shilingi trilioni 139.6 mwaka 2019. Aidha, mwaka 2020, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu milioni 55.9, ikilinganishwa na watu milioni 54.2 mwaka 2019. Hivyo, Wastani wa Pato kwa Mtu lilikadiriwa kufikia shilingi 2,653,790, sawa na dola za Marekani 1,151.0 mwaka 2020 ikilinganishwa na shilingi 2,573,324, sawa na dola za Marekani 1,118.9 mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1.

Mwenendo wa Bei

  1. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulipungua kutoka wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2019 hadi asilimia 3.3 mwaka 2020. Aidha, mfumuko wa bei umebaki  katika wigo wa  asilimia 3.3 Mei 2021. Mwenendo wa mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha, kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti.

Utekelezaji wa Sera ya Fedha 2020/21

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, malengo ya sera ya fedha yalikuwa ni kama ifuatavyo:
  1. Ukuaji wa wastani wa fedha taslimu usiozidi asilimia 9.0;
  2. Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) usiozidi asilimia 10.0;
  3. Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi usiozidi asilimia 13.5; na
  4. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi 4.0.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza baadhi ya viwango vya riba katika masoko ya fedha hususan riba za mikopo. Wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ulipungua hadi asilimia 16.58, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 16.91 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja zilipungua na kufikia wastani wa asilimia 16.05 kutoka asilimia 16.37. Aidha, wastani wa riba za amana kwa ujumla ulikuwa asilimia 6.95 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.69 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Riba za amana za kipindi cha mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ikilinganishwa na asilimia 8.01 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Ujazi wa Fedha na Karadha

  1. Mheshimiwa Spika, ujazi wa fedha uliendelea kukua kwa kasi inayoendana na mahitaji ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka na kufikia shilingi trilioni 31.0 Aprili 2021 ikilinganishwa na shilingi trilioni 28.76 Aprili 2020, sawa na ongezeko la asilimia 7.8. Aidha, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) uliongezeka kufikia shilingi trilioni 23.59 Aprili 2021 ikilinganishwa na shilingi trilioni 22.03 Aprili 2020, sawa na ongezeko la asilimia 7.1. Ongezeko hili la ujazi wa fedha ni matokeo ya usimamizi thabiti wa sera ya fedha.

Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi

  1. Mheshimiwa Spika, Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 4.8 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Ukuaji mdogo wa mikopo kwa sekta binafsi ulitokana na athari za UVIKO – 19 kwenye shughuli za kiuchumi nchini. Aidha, sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa katika shughuli binafsi ambazo zilipata asilimia 35.8 ya mikopo yote, ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 15.7, uzalishaji viwandani asilimia 10.1 na kilimo asilimia 8.0.

Ukuzaji Rasilimali

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2020, ukuzaji rasilimali kwa bei za miaka husika ulifikia shilingi trilioni 59.2 kutoka shilingi trilioni 55.8 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 6.2. Aidha, ukuzaji rasilimali za kudumu kwa bei za miaka husika uliongezeka kwa asilimia 7.8 kutoka shilingi trilioni 59.4 mwaka 2019 hadi shilingi trilioni 64.0 mwaka 2020. Vilevile, thamani ya limbikizo la rasilimali kwa bei za miaka husika ilipungua kwa shilingi trilioni 4.8 mwaka 2020 ikilinganishwa na upungufu wa shilingi trilioni 3.7 mwaka 2019. Ukuzaji rasilimali katika sekta ya umma uliongezeka kwa asilimia 7.8 kufikia shilingi trilioni 19.0 mwaka 2020 kwa bei za miaka husika wakati katika sekta binafsi uliongezeka kwa asilimia 7.8 kufikia shilingi trilioni 45.0 mwaka 2020. 

Sekta ya Nje 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021, urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje uliimarika kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 1,177.2, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 1,443.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa kulichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu na bidhaa za maua na mbogamboga sambamba na kupungua kwa thamani ya uagizaji wa mafuta na vyombo vya usafiri.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma ilifikia dola za Marekani bilioni 8.5 kutoka dola za Marekani bilioni 9.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Upungufu huo ulitokana na kupungua kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii, ikiwa ni matokeo ya hatua zilizochukuliwa na mataifa mengine duniani ili kupunguza kasi ya maambukizi ya UVIKO-19, hususan kuzuia safari za kimataifa. Aidha, katika kipindi hicho, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje ilifikia dola za Marekani bilioni 9.3, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 10.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Hali hiyo  ilitokana na kupungua kwa thamani ya uagizaji wa mafuta, vyombo vya usafiri na vifaa vya ujenzi.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021, thamani ya mauzo ya bidhaa iliongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 6.35 kutoka dola za Marekani bilioni 5.67 kipindi kama hicho mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 12.0. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa asilia na zisizo asilia ikiwemo dhahabu, madini mengineyo, bidhaa za maua na mbogamboga pamoja na bidhaa za viwandani. Aidha, thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ilipungua kwa asilimia 7.4 kutoka dola za Marekani bilioni 8.75 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2020 hadi dola za Marekani bilioni 8.11 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Hali hiyo ilitokana na kupungua kwa uagizaji wa baadhi ya bidhaa kufuatia kuimarika kwa uzalishaji katika viwanda vya ndani, hususan bidhaa za ujenzi kama vile marumaru, nondo na saruji.
  1. Mheshimiwa Spika, mapato yatokanayo na huduma yalipungua kutoka dola za Marekani bilioni 3.89 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2020, hadi dola za Marekani bilioni 2.20 Aprili 2021. Aidha, malipo ya huduma yalipungua na kufikia dola za Marekani bilioni 1.19 kutoka dola za Marekani bilioni 1.73 kutokana na kupungua kwa malipo yanayohusiana na usafiri wa nje. 

Akiba ya Fedha za Kigeni

  1. Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Hadi Aprili 2021, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 4.97 ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi 5.8. Kiwango hicho ni zaidi ya lengo la nchi la kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa muda wa miezi 4.0 na ni zaidi ya lengo la miezi 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwenendo wa Thamani ya Shilingi

  1. Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imeendelea kuwa tulivu ambapo dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,298.5 Aprili 2021, ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,291.3 Aprili 2020. Utulivu wa shilingi umetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa Sera za Fedha na Bajeti, kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya nchi pamoja na mwenendo chanya wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Vilevile, hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kusimamia misingi ya uwazi katika ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni nchini zimechangia thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani kuwa tulivu.

Deni la Serikali

  1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2021, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 60.9, ikilinganishwa na shilingi trilioni 55.5 kipindi kama hicho mwaka 2020. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 43.7 na deni la ndani ni shilingi trilioni 17.3. Ongezeko hilo lilitokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2020 inaonesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa. 

MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2020/21

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi 2020/21, Serikali ilikuwa inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 kupitia Mipango ya Maendeleo ya mwaka mmoja mmoja. Dhima kuu ya Mpango wa Pili ilikuwa ni “Ujenzi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Serikali ilijenga miundombinu ya msingi ili kuwezesha wananchi kujiletea maendeleo na kuchochea uwekezaji katika viwanda. Katika kipindi hicho, mafanikio mbalimbali yalipatikana hususan kuimarika kwa ustawi wa uchumi na maisha ya watu. Mafanikio hayo yanajumuisha:
  1. Miundombinu ya Reli: Kufikia asilimia 91 ya ujenzi wa Reli ya Kati ya Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR) kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) na asilimia 61 kwa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422); na kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07. Mafanikio mengine ni: kukamilika kwa ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam – Isaka (km 970); kukamilika kwa ukarabati na kuanza kutoa huduma za reli ya Tanga hadi Arusha (km 439); na kukarabatiwa kwa mabehewa 347 ya mizigo.
  1. Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Kukamilika kwa ujenzi wa njia ya kuchepusha maji (Diversion Tunnel); kuendelea na ujenzi wa bwawa (main dam and spillways),  ujenzi wa njia kuu za kupitisha maji (tunnels), ujenzi wa kituo cha kuzalishia umeme (Power House) na ujenzi wa kituo cha kusafirisha umeme (Switch yard) ambapo utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 52.
  1. Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania: Kununuliwa kwa ndege mpya 11 ambazo zinasafirisha abiria na mizigo ndani na nje ya nchi; kuboreshwa kwa karakana ya ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro; ununuzi wa jozi ya injini za akiba kwa ndege aina ya Dash 8 Q400; na kulipa bima za ndege Boeing 787-8 Dreamliner na Dash 8 Q400.
  1. Miradi ya Umeme: Kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 kutoka Makambako hadi Songea; kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Bulyanhulu – Geita; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 91.6; kukamilika kwa asilimia 80 ya utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo – MW 80; kuendelea na utekelezaji wa  mradi wa Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea na kuhuisha upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya Kufua Umeme wa Maji ya Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222; kukamilika kwa upembuzi yakinifu na uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi; na kuunganishwa umeme kwa jumla ya vijiji 10,312 kati ya vijiji 12,317, sawa na asilimia 83.7 ya vijiji vyote nchini.
  1. Ujenzi na Ukarabati wa Viwanja vya Ndege: Kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Geita (asilimia 95), Songea (asilimia 95) na Mtwara (asilimia 55); kukamilika kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni 759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga vitakavyogharimu Euro milioni 50 sawa na shilingi bilioni 136.85; kukamilika kwa upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege cha Dodoma; na kufungwa kwa mifumo ya kuongoza ndege katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Tabora na Mwanza.
  2. Uendelezaji wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: Kuboreshwa kwa gati namba 1 – 5; kukamilika kwa ujenzi wa gati la kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na uboreshaji wa gati namba 6 na 7. Bandari ya Mtwara: kukamilika kwa ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia makasha. Bandari ya Tanga: kukamilika kwa uongezaji wa kina cha lango la kuingia meli kutoka mita nne (4) hadi mita 13, kuweka vifaa vya kuongozea meli pamoja na ujenzi wa magati mawili (2) kwenye kina kirefu. 

Bandari za Maziwa Makuu: Kukamilika kwa ujenzi wa magati ya Nyamirembe, Magarine, Lushamba, Ntama na Mwigobero katika Ziwa Victoria; kukamilika kwa  ujenzi wa magati ya Sibwesa na Kabwe pamoja na kuendelea na ujenzi wa Bandari za Karema, Ujiji, Kibirizi na Lagosa katika Ziwa Tanganyika; na kukamilika kwa ujenzi wa sakafu ngumu katika bandari ya Kiwira na Itungi katika Ziwa Nyasa.

  1. Kuboresha Huduma za Usafiri na Usafirishaji wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu

Ziwa Victoria na Tanganyika: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambao umefikia asilimia 74; na kukamilika kwa ujenzi wa chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza chenye uwezo wa kubeba meli au chombo chenye uzito kuanzia tani moja (1) hadi tani 4,000.

Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja; na kukamilika na kuanza kufanya kazi kwa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo.

  1. Barabara na Madaraja Makubwa: Serikali imeendelea kujenga na kukarabati mtandao wa barabara nchini kwa lengo la kufungulia fursa za kiuchumi katika maeneo mbalimbali, kuongeza wigo wa utoaji huduma za msingi na ustawi wa maisha ya watu. Mafanikio yaliyopatikana yanajumuisha: ujenzi wa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,209 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) hivyo kufanya mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami kufikia kilomita 13,044. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni: kukamilika na kuanza kutumika kwa daraja la juu la Kijazi (Kijazi Interchange); kukamilika kwa asilimia 87.38 ya upanuzi wa barabara sehemu ya  Kimara – Kiluvya (km 19.2); kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.5 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 27; kuendelea na ujenzi wa Daraja jipya la Tanzanite (Dar es Salaam) ambao umefikia asilimia 77.19; na Daraja Jipya la Wami (Pwani) asilimia 50.
  1. Huduma za Afya: Ujenzi wa hospitali 99 za halmashauri ambapo hospitali 67 zimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje; kujengwa kwa hospitali 10 za rufaa za mikoa; kukamilika kwa ujenzi wa zahanati 1,198; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wodi namba 18 ya Sewa Haji pamoja na ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa binafsi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la mionzi katika Hospitali ya Rufaa Dodoma; kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru – Dodoma ambayo imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje; kununuliwa kwa mashine za kidigitali za mionzi na ultrasound, vifaa vya maabara na mashine za uchunguzi wa kifua kikuu kwa kuotesha vimelea BACTEC 960 (Mycobacteria Growth Indicator Tube – MGIT) na Blood culture machine katika Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu – Kibong’oto; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala umefikia asilimia 98; ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Rufaa Njombe umefikia asilimia 73; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la ghorofa moja la huduma za upasuaji, radiolojia na maabara na kufikia asilimia 51 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Simiyu; kufikia asilimia 98 ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Burigi (Chato); na ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo upatikanaji wa aina 30 za dawa zenye kukidhi magonjwa ya msingi (30 tracer medicines) ulifikia asilimia 86 na upatikanaji wa aina 312 za dawa muhimu umefikia asilimia 74. 
  1. Elimu: Kuendelea kutekeleza Sera ya Serikali ya kuongeza fursa za elimu bora kwa kila mtoto nchini kwa kugharamia elimumsingi bila ada ambapo wastani wa shilingi bilioni 20.8 zinatolewa kila mwezi; kujengwa kwa miundombinu muhimu katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na Sekondari 883), mabweni 547, nyumba 101 za walimu, majengo ya utawala 25 na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa maboma 2,815 katika shule za msingi 2,133; kukarabatiwa kwa shule kongwe 84 kati ya 89; kuongezeka kwa wigo wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu; kuanzishwa kwa vituo vya umahiri vya mafunzo katika taasisi za elimu ya ufundi; kuimarishwa kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji katika taaluma za anga na Chuo cha Ufundi Arusha katika taaluma ya nishati; na kuendelea kugharamia chakula na malazi kwa wanachuo wote katika vyuo 35 vya mafunzo ya ualimu vya Serikali.
  1. Maji Mijini na Vijijini: Kukamilika kwa miradi 1,845 ya maji mijini na vijijini hivyo kuwezesha huduma za maji kufikia asilimia 85 kwa wananchi waishio mijini na asilimia 72.3 vijijini hadi Machi 2021. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika kwa miradi ya maji katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 90), Mwanza (asilimia 76) na Arusha (asilimia 62); na kukamilika na kuzinduliwa kwa Mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega. Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
  1. Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Kilimo: Kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji hivyo kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa skimu 17 za umwagiliaji zenye ukubwa wa hekta 8,536 kupitia ASDP II na skimu tano (5) za Kigugu – Mvomero (hekta 195), Msolwa Ujamaa (hekta 40), Njage – Kilombero (hekta 75), Mvumi – Kilosa (hekta 249) na Kilangali Seed Farm – Kilosa (hekta 400) kupitia mradi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga – Expanded Rice Production Project (ERPP); kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 76,726 mwaka 2020; na kukamilika kwa ujenzi wa maabara ya mbegu katika makao makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo – Morogoro.

Mifugo: Kuimarishwa kwa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji kilichopo Usa River Arusha kwa kununua kifaa (Chiller) kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha kimiminika cha naitrojeni; kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati vya nyama vya Tanchoice (Pwani), Elia Food Oversees Limited (Arusha) na Binjiang Company Limited (Shinyanga); kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverage Company Limited (Arusha); kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience Africa Limited (Pwani) chenye uwezo wa kuzalisha chanjo aina 37; kuendelea kuboresha huduma za malisho ya mifugo na majosho; na kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Vingunguti.

Uvuvi: Kuongezeka kwa uvunaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 362,645 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.48 mwaka 2015/16 hadi tani 497,567 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 2.34 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara kutoka tani 23,000.6 mwaka 2015/16 hadi tani 27,596.3 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda masoko ya Ulaya ambapo katika mwaka 2019/20, jumla ya tani 777.8 za mabondo zilisafirishwa; kuongezeka kwa mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 379.3 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 506.2 mwaka 2019/20; na kuendelea na maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na ununuzi wa meli nne (4) za uvuvi.

  1. Madini: Kupitia na kutunga Sheria, Sera na mikataba ya madini; kuanzishwa kwa kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzania (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84) ambapo imetoa gawio la shilingi bilioni 100; kuanzishwa kwa kampuni ya Tembo Nickel Corporation ambayo ni ubia kati ya Serikali ya Tanzania (hisa asilimia 16) na kampuni ya LZ Nickel Mining Limited (hisa asilimia 84) kwa ajili ya uchimbaji wa madini wa Nickel Kabanga; kuanzishwa kwa kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) kwa ajili ya kuchenjua dhahabu; kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 50 vya kuuzia madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya; kuimarishwa kwa ulinzi wa rasilimali za madini kwa kujenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24 wa Mirerani Manyara pamoja na kujenga one stop centre, kufunga vifaa vya ulinzi ikiwa ni pamoja na taa na CCTV Camera kuzunguka ukuta na barabara ya kuzunguka ukuta wa ndani; na kukamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) vya mfano vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Lwamgasa (Geita), Katente (Bukombe) na Itumbi (Chunya).
  1. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi hicho umewezesha kuimarika kwa uchumi jumla, hivyo kuiwezesha Tanzania kuingia katika kundi la nchi za hadhi ya kipato cha kati cha chini Julai 2020. Katika kuhakikisha kuwa mafanikio ya Tanzania kuingia kipato cha kati yanakuwa endelevu, Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuweza kustahimili changamoto zozote zitakazojitokeza ikijumuisha: kuimarisha viashiria vya uchumi mpana na kuhakikisha ukuaji endelevu wa uchumi; kuhakikikisha kuwa ukuaji wa uchumi ni shirikishi ili kupunguza umaskini; na kujenga na kuimarisha tabaka la watu wa pato la kati kwa kuendeleza rasilimali watu na uboreshaji wa huduma muhimu za msingi.
  2. Mheshimiwa Spika, Mafanikio yaliyopatikana yanajenga msingi wa kuendelea kutekeleza Mipango ya Maendeleo kwa kasi zaidi hususan kwa kuzingatia kaulimbiu ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya “Kazi Iendelee”. Maono na miongozo yake inatoa dira na mwelekeo mpya wa Taifa katika kutumia vema fursa mbalimbali za kikanda na kimataifa. Natoa rai kwa watanzania wenzangu tuyaenzi mafanikio haya na tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuliletea mafanikio zaidi Taifa letu.

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2021/22

Malengo na Shabaha za Uchumi Jumla kwa Mwaka 2021/22

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/22, shabaha za uchumi jumla zilizozingatiwa katika Mpango ni kama ifuatavyo:
  1. Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.6 mwaka 2021;
  2. Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 hadi 5.0 katika muda wa kati;
  3. Mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 na wastani wa asilimia 16.3 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2023/24;
  4. Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21;
  5. Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa ili kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
  6. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).

Miradi ya Kipaumbele kwa Mwaka 2021/22

  1. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 ni wa kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Mpango huu utatekeleza miradi na programu ambazo utekelezaji wake haukukamilika katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Hivyo,  miradi ya kipaumbele kwa mwaka 2021/22 inaakisi maeneo matano (5) ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. Aidha, maeneo ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ni: kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.
  1. Mheshimiwa Spika, miradi ya kipaumbele inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka 2021/22 ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. Miradi hiyo inajumuisha miradi ya kielelezo ambayo ni: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kwa kuendelea na ujenzi wa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) na kipande cha Mwanza – Isaka (km 341); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115; kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; miradi ya Magadi Soda Engaruka, Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Chuma – Liganga; miradi ya Kufua Umeme wa Maji ya Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222)  – Njombe; ujenzi wa madaraja makubwa na barabara za juu za Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na ununuzi wa meli za uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; utafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; Kanda Maalumu za Kiuchumi; na kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalumu (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi, msukumo utawekwa katika miradi  inayolenga kuwa na utulivu wa uchumi na uendelezaji wa reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini, usafiri wa anga, nishati, bandari, viwanja vya ndege pamoja na utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji. Katika eneo hili, miradi ifuatayo itatekelezwa: 

Uendelezaji wa Miundombinu

  1. Reli: Katika mwaka 2021/22, shughuli zitakazopewa kipaumbele ni pamoja na: Ukarabati wa njia kuu ya reli katika maeneo ya Tabora – Kigoma (km 411), Tabora – Isaka – Mwanza (km 385) na matengenezo ya njia ya reli ya Tanga – Arusha (km 470); ukarabati wa karakana na majengo ya reli; ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa na ukarabati wa mabehewa; ukarabati wa mfumo wa ishara na mawasiliano wa reli; na uwekaji alama za mipaka katika maeneo ya reli.
  1. Barabara na madaraja: Kipaumbele kitawekwa katika barabara za lami zinazofungua fursa za kiuchumi ambazo ni: barabara za Kidatu – Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha/Songea (km 499); Lukuyufusi – Mkenda (km 122.5); Ifakara – Kihansi – Mlimba – Madeke – Kibena (km 220); Tabora – Ipole – Koga – Mpanda (km 365.36); barabara ya Makutano  – Natta – Mugumu/Loliondo – Mto wa Mbu (km 235); Manyoni – Itigi – Tabora (km 259.75); Handeni– Kiberashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboloti – Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (Km 460); Dodoma – Mtera – Iringa (km 273.3); Dodoma – Babati (km 243.8); Mbeya –  Chunya – Makongolosi – Rungwa – Itigi – Mkiwa (km 528); Kigoma – Kidahwe – Uvinza – Kaliua – Tabora (km 389.7); Barabara ya Mtwara – Newala – Masasi (km 210); Barabara ya Masasi – Songea – Mbamba Bay (km 343.2); Barabara ya Nzega – Tabora (km 289.7); Barabara ya Msimba – Ruaha Mbuyuni/Ikokoto Mafinga (km 234.8); Igawa – Songwe –Tunduma na Mchepuo wa Mbeya (km 273.5); na Makambako – Songea na Mchepuo wa Songea (km 295).
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani zikiwemo: barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port (km 117); Isaka – Lusahunga (km 242.2); Nyakahura – Kumubuga – Murusagamba na Kumubuga – Rulenge – Kabanga Nickel – Murugarama (km 141); Sumbawanga – Mpanda – Nyakanazi (km 432.56); Nyanguge – Musoma na mchepuo wa Usagara (km 202.25); Nyamuswa – Bunda – Kisorya (km 107.4); Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi (km 121); Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi (km 341.25); Tarakea – Holili (km 53); Barabara ya Mpemba – Isongole (km 51.2); na barabara ya Geita – Bulyanhulu – Kahama (km 120). 

Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara za kupunguza msongamano za Jijini Dar es Salaam (km 138.5) pamoja na barabara za mikoa, kuboresha miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kwa awamu zote nne, ujenzi wa barabara za juu (Flyover) Jijini Dar es Salaam, barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma pamoja na barabara za vijijini na mijini kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). Vilevile, Serikali itaendelea na ujenzi wa madaraja makubwa yakiwemo madaraja ya New Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kirumi (Mara) na Mkenda (Ruvuma).

  1. Usafiri wa Majini; Serikali itaendelea kuboresha usafiri wa majini kwa kujenga na kukarabati meli katika maziwa makuu ikijumuisha MV Mwanza Hapa Kazi Tu, MV Liemba na MV Umoja, ujenzi wa maegesho ya vivuko na ununuzi na ukarabati wa vivuko. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na bandari za maziwa makuu zikijumuisha Bandari ya Ziwa Victoria na Nyasa. 
  1. Usafiri wa Anga:  Miradi itakayotekelezwa ni: Ukarabati wa jengo la Pili la abiria (JNIA-TB II);  kuboresha huduma katika viwanja vingine vya ndege na ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji – NIT. Aidha, Serikali itaendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege ikiwa ni pamoja na kiwanja cha kimataifa cha Songwe, Msalato, viwanja vya mikoa pamoja na kuanza ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kigoma, Sumbawanga, Tabora na Shinyanga. 
  1. Nishati: Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi ya kufua umeme ya Kinyerezi I Extension – MW 185, Rusumo – MW 80, Malagarasi MW 45 na Kikonge – MW 330; Mradi wa njia za kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi; mradi wa kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 400 – North – West Grid Extension (Iringa – Mbeya – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi); mradi wa kusafirisha umeme wa kV 220 Geita – Nyakanazi na mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 400 Singida – Arusha – Namanga. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini pamoja na miradi ya gesi asilia na mafuta ikijumuisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta safi kutoka Dar es Salaam (Tanzania) hadi Ndola (Zambia) na usambazaji wa gesi asilia kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mtwara na Lindi. 
  1. Mapinduzi ya TEHAMA: Serikali itaendelea kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kuendelea na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; ujenzi wa Mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi unaojumuisha mradi wa Tanzania ya Kidigitali; na kuimarisha matumizi ya Serikali mtandao katika utoaji huduma kwa umma.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, miradi ifuatayo itatekelezwa:
  1. Uzalishaji Viwandani: Katika eneo hili miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: kiwanda cha Mashine na Vipuri KMTC; kuboresha Shirika la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC); kiwanda cha Kuunganisha Matrekta ya URSUS – TAMCO – Kibaha; eneo la Kongano ya Viwanda – TAMCO; na mradi wa mashamba na viwanda vya mazao ya mafuta. Aidha, Serikali itaendeleza Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (SEZ/EPZ) ya Tanga, Kigoma, Kahama, Bunda, Songwe, Manyara, Arusha na Mtwara; kuimarisha taasisi za utafiti na maendeleo ya viwanda na kilimo zikiwemo CAMARTEC, TIRDO, SIDO na TEMDO; na kuimarisha uzalishaji viwandani kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).
  1. Ubiasharishaji wa Mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia ASDP II 
  1. Kilimo: Maeneo yatakayopewa msukumo ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; kuimarisha huduma za upimaji matabaka na ubora wa udongo; kuwezesha uanzishwaji wa mashamba makubwa ili kuwa kitovu cha teknolojia bora kwa wakulima wadogo; kuongeza matumizi ya teknolojia na mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi; kuongeza matumizi ya teknolojia bora katika uzalishaji wa mazao ili kuongeza uzalishaji na tija; na kuimarisha vituo vya utafiti wa mbegu bora, vyuo vya mafunzo na vituo vya mafunzo ya wakulima na huduma za ugani. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo zana za kilimo, mbegu bora za mazao, mbolea na viuatilifu; kuimarisha miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo; uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo; na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi. Vilevile, Serikali itaendelea kuhamasisha uzalishaji wa mazao yakiwemo mazao ya kimkakati ya mkonge, chikichi, tumbaku, pareto, korosho, kahawa na pamba. 
  1. Mifugo: Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) itaendelea kuimarisha huduma za ugani, tafiti, tiba na udhibiti wa magonjwa ya mifugo; kuboresha huduma za uhimilishaji mifugo; kuimarisha Kampuni ya Ranchi za Taifa; kujenga machinjio ya kisasa na minada ya mifugo; kuboresha huduma za unyweshaji mifugo, malisho na vyakula vya mifugo; na kuimarisha vyuo vya mafunzo ya mifugo.
  1. Uvuvi: Miradi itakayotekelezwa inajumuisha kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania – TAFICO; kuimarisha na kuendeleza ulinzi wa rasilimali za uvuvi na mazingira; kujenga na kuimarisha miundombinu ya mazao ya uvuvi; kukarabati vituo vya ukuzaji viumbe maji; kuimarisha huduma za ugani, Taasisi ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).
  1. Uchimbaji wa Madini, Vito vya Thamani na Gesi Asilia: Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP) kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuanzisha mradi wa makaa ya mawe ya kupikia (coal briqquette) kupitia Shirika la Madini la Taifa – STAMICO; na kufanya tafiti za jiolojia kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo na utafiti wa madini ya viwandani (gypsum, iron, graphite, limestone, coal, radioactive, helium gas) kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania – GST.
  1. Huduma
  1. Maliasili na Utalii: Miradi itakayopewa kipaumbele ni pamoja na mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii katika Maeneo ya Kipaumbele – REGROW; mradi wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori Tanzania; mradi wa Kujenga Uwezo wa Taasisi na Mafunzo ya Misitu na Ufugaji Nyuki; mradi wa Panda Miti Kibiashara; mradi wa Kuwezesha Mnyororo wa Thamani ya Mazao ya Nyuki – BEVAC; mradi wa Uendelezaji wa Utalii wa Mikutano na Matukio – MICE; na Programu ya Misitu na Uendelezaji wa Mnyororo wa Thamani ya Mazao ya Misitu – FORVAC.
  1. Huduma za Biashara: Katika kuendeleza huduma za biashara, Serikali itaweka mkazo katika uendelezaji wa Kituo cha Biashara na Ugavi Kurasini ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kabambe wa uendelezaji wa eneo hilo pamoja na kutafuta wawekezaji mahiri. 
  1. Huduma za Fedha: Katika kuendelea kuimarisha huduma za fedha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ili kuongeza utoaji wa mikopo ikijumuisha mikopo kwa miradi ya uhifadhi wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi; utoaji  elimu ya fedha kwa umma; na kuendelea kusimamia masoko ya mitaji. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha uendeshaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Benki ya Maendeleo ya Kilimo – TADB, Soko la Mitaji na Dhamana, huduma za bima, huduma ndogo za fedha pamoja na huduma jumuishi za fedha. 
  1. Usimamizi wa Mashirika ya Umma: Serikali itaimarisha usimamizi na uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuhakikisha kuwa yanazalisha na kutoa huduma kwa tija. Lengo ni kuyawezesha kujiendesha kwa faida na kutoa mchango stahiki (gawio) Serikalini kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
  1. Usimamizi wa Uchumi Jumla: Serikali itaendelea kuimarisha usimamzi wa viashira vya uchumi jumla ikijumuisha: kudhibiti mfumuko wa bei; utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha uzalishaji na mauzo nje, kuongeza ajira, mapato ya fedha za kigeni, kupunguza utegemezi wa kibajeti na hivyo kuimarisha ustawi wa maisha ya watu.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kukuza uwekezaji na biashara, Serikali itatekeleza miradi na programu mbalimbali zitakazoimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa katika kukuza biashara. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Biashara na Uwekezaji (Blueprint) ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi. Miradi mahsusi itayotekelezwa ni pamoja na: mradi wa kuboresha mfumo wa kodi; mradi wa uendelezaji wa masoko ya bidhaa; kuendelea na udhibiti wa ubora wa bidhaa; na kukuza Soko la Bidhaa Tanzania – TMX kwa kujumuisha mazao ya chai, mkonge, kokoa, kahawa, mpunga, mahindi, mbao, pamba, mazao ya mifugo na nyanya kwenye soko la bidhaa.
  1. Mheshimiwa Spika, katika eneo la kuchochea maendeleo ya watu, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unaakisi maisha ya watu. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha maisha ya watu kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu na mafunzo kwa ujumla, afya na ustawi wa jamii, kinga ya jamii, huduma za maji na usafi wa mazingira. Katika mwaka 2021/22, Serikali itatekeleza miradi ifuatayo:
  1. Afya na Ustawi wa Jamii: Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa za Mount Meru (Arusha), Mbeya, Sekou Toure (Mwanza), Mwananyamala (Dar es Salaam), Tumbi (Pwani), Maweni (Kigoma), Manyara, Mawenzi (Kilimanjaro), Katavi, Njombe, Geita, Simiyu, Songwe, Kwangwa (Mara) na Shinyanga; kuboresha miundombinu katika hospitali za mikoa; kuimarisha upatikanaji wa damu salama kwa kununua vitendanishi vya maabara, vifaa vya kuhifadhi damu na kugharamia uendeshaji Mpango wa Damu Salama; kununua na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; kuendelea na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, Kifua Kikuu na Ukoma na magonjwa ya kuambukiza; kuimarisha vyuo vya mafunzo ya afya; kuimarisha tafiti za afya, huduma za tiba asili na tiba mbadala; kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za afya nchini; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati. Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi na ukarabati wa vyuo vya maendeleo ya jamii pamoja na kuwezesha huduma za ustawi wa jamii.
  1. Elimu: Kuendelea na utoaji wa elimumsingi bila ada na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi na vyuo vya ualimu vya Ndala, Kitangali, Shinyanga na Mpuguso. Aidha, Serikali itaendelea na ukarabati wa vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Mzumbe, Sokoine (SUA), Ardhi, Ushirika Moshi, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
  1. Ardhi, Mipango Miji, Nyumba na Maendeleo ya Makazi: Katika kuendelea kupanga, kupima na kumilikisha ardhi mijini na vijijini, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya uimarishaji wa mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani, uimarishaji wa miundombinu ya upimaji na ramani na uboreshaji wa milki za ardhi na upangaji wa matumizi ya ardhi.
  1. Huduma ya Maji Safi na Maji Taka: Serikali itaendelea kuboresha huduma za maji mijini na vijijini kwa kutekeleza miradi ya maji katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa; kujenga na kukarabati miradi ya maji katika miji mikuu ya mikoa; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya Masasi – Nachingwea, Same – Mwanga – Korogwe, Ziwa Victoria – Igunga, Nzega na Tabora, Ziwa Victoria – Kahama – Shinyanga; kuboresha huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam; na kuendelea na ufuatiliaji na uratibu wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji – WSDP II.
  1. Hifadhi ya Jamii: Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuimarisha Programu ya Kusaidia Kaya Maskini na kuboresha huduma za hifadhi ya jamii kwa kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Sekta ya Jamii (2019/20 – 2022/23).
  1. Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi: Serikali itaendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali ikiwemo: kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu; kuwezesha taaasisi za fedha zinazogharamia maendeleo ambazo ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Maendeleo TIB. Kupitia uwezeshaji huu, shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, uzalishaji viwandani na biashara zinatarajiwa kukuzwa na kuendelezwa.
  1. Kuongeza Mapato katika halmashauri: Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuwezesha halmashauri kujitegemea kimapato ikijumuisha miradi ya masoko ya kimkakati, stendi, maegesho ya malori, viwanda ili kuongeza wigo wa utoaji huduma, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na hatimaye halmashauri kujitegemea.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza rasilimali watu, msukumo wa pekee utawekwa katika miradi na programu ambazo zinalenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu nchini. Miradi na programu hizo ni pamoja na: ukuzaji ujuzi wa nguvukazi na kuimarisha upatikanaji wa takwimu za soko la ajira; kukuza ubunifu na kuwezesha uhawilishaji wa teknolojia kwa vijana na watu wenye ulemavu; na kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha tasnia ya habari, burudani na michezo, Serikali itaendelea kuongeza wigo wa usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC); kukusanya na kusambaza habari na taarifa kwa wananchi kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini; kujenga vituo vya mazoezi na kupumzikia wananchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Geita; kuimarisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa nchini; na upanuzi wa Chuo cha Michezo cha Malya.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mchango na umuhimu wa Sekta Binafsi katika ugharamiaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Baadhi ya miradi itakayotekelezwa ni: ujenzi wa viwanda vya dawa muhimu na vifaa tiba; uendeshaji wa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam awamu ya kwanza; ujenzi wa hoteli ya nyota nne na kituo changamani cha biashara katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; kusambaza gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; na ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi chini ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Aidha, Serikali itaendelea kuishirikisha sekta binafsi zikiwemo taasisi za fedha katika kugharamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha mashirikiano ya kikanda na kimataifa ikijumuisha kukarabati na kujenga majengo ya ofisi za balozi katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Oman na Ethiopia. Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa vyumba tisa (9) vya mihadhara katika Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam.
  1. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 utaendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha Muungano wetu. Miradi itakayotekelezwa kwa pamoja Tanzania bara na Visiwani ni pamoja na:
  1. Kukarabati na kujenga Ofisi na Makazi ya Makamu wa Rais Wete – Pemba na Kilimani – Dodoma na kukamilisha ukarabati wa Ofisi na Makazi ya Makamu wa Rais Tunguu – Zanzibar;
  2. Kuongoa ardhi iliyoharibika na kuboresha kingo za mito katika maeneo ya Kaskazini A (Unguja) na Kishapu (Shinyanga) katika maeneo ya mradi kwa kutekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kupitia mifumo ya ikolojia; na 
  1. Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) ambapo shughuli zilizopangwa ni kutambua na kutathmini hali za ustawi wa maisha ya kaya 886,724 za walengwa wa Mpango na kuhawilisha ruzuku kwa kaya maskini 1,146,723 katika maeneo 186 ya utekelezaji kwa mizunguko sita (6) ya malipo Tanzania bara na Visiwani.
  1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu miradi ya kipaumbele yanapatikana katika Kitabu cha Mpango, Sura ya Nne.

Vihatarishi vya Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2021/22

  1. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango unaweza kuathiriwa na vihatarishi vya ndani na nje. Vihatarishi vya ndani ni pamoja na: rushwa; uharibifu wa mazingira; ushiriki mdogo wa sekta binafsi; na kutotabirika kwa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele ya Mpango. Vihatarishi vya nje ni pamoja na: mabadiliko ya tabianchi; mtikisiko wa uchumi wa kikanda na kimataifa; majanga asilia; na mlipuko wa magonjwa yanayoathiri dunia.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vihatarishi vya utekelezaji wa Mpango, Serikali itachukua hatua mbalimbali ikijumuisha: Kuendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wanaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa; kuendelea kuboresha mazingira wezeshi ya biashara ili kupunguza gharama za uwekezaji; kuimarisha maandalizi ya miradi; kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi; kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi kwa lengo la kuongeza wigo wa kodi; kuimarisha taasisi za ndani za kugharamia maendeleo ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji; na kuimarisha usimamizi na udhibiti wa mifumo ya kieletroniki ya Serikali.

Mikakati mingine ni pamoja na: Kuhamasisha uwekezaji wa ndani katika kujenga viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo, ikijumuisha kuimarisha kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi – Climate Smart Agriculture; kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani ili kuongeza ushindani katika masoko ya nje; kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya majadiliano ili kuzuia matukio yanayoweza kuhatarisha amani nchini; na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na maendeleo ya kiuchumi ya kikanda na kimataifa.

Ugharamiaji wa Mpango 2021/22

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021/22, shilingi bilioni 13,326.8 zinakadiriwa kutumika ili kugharamia miradi ya maendeleo. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 37 ya Bajeti yote ya Serikali. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 6,180.0 ni matarajio ya mapato ya ndani, shilingi bilioni 4,190.9 ni mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara na shilingi bilioni 2,955.9 ni misaada na mikopo nafuu kutoka nje. Sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo itatumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya kielelezo. Aidha, miradi mingine ya maendeleo, itaendelea kugharamiwa kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) pamoja na utaratibu wa Kampuni Maalum (Special Purpose Vehicles).
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kufanya yafuatayo: kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi utakaowezesha kupanuka kwa wigo wa kodi; kuimarisha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari ikiwemo kuboresha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA na kutoa elimu kwa umma; kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi; kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato; kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; na kuoanisha na kuboresha tozo na ada mbalimbali. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mfumo wa Dirisha Moja la Kielektroniki (Tanzania Electronic Single Window System – TeSWS) ili kurahisisha upitishaji wa mizigo katika vituo vya mipakani pamoja na kupunguza gharama za kufanya biashara nchini; kuendelea kusimamia Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (Government Electronic Payment Gateway – GePG); kusimamia malipo ya tozo na ada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa michango stahiki inawasilishwa kwa wakati kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Vilevile, Serikali itaimarisha usimamizi wa fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zinazopelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo kupitia mfumo wa uratibu wa fedha zinazopelekwa moja kwa moja kwa watekelezaji wa miradi ya maendeleo (D-fund Management Information System) pamoja na kuimarisha maandalizi ya miradi ya maendeleo.

Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa za Utekelezaji

  1. Mheshimiwa Spika, ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa ni moja ya nyenzo  muhimu inayowezesha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo. Katika mwaka 2020/21, Wizara ya Fedha na Mipango ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi 248 katika sekta za Uchukuzi, Viwanda, Elimu, Afya, Ujenzi, Utawala Bora, Kilimo, Mifugo, Maji na Biashara inayotekelezwa Tanzania Bara na Visiwani. Serikali itaendelea kutumia mbinu na viashiria vilivyoainishwa katika Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ili kupima utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2021/22 na kuchukua hatua za kutatua changamoto zitakazobainika katika utekelezaji. Aidha, Serikali itaendelea kuzingatia miongozo mbalimbali ya ufuatiliaji na tathmini ya Mpango ikiwemo Sheria ya Ununuzi wa Umma, SURA 410, Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348. Vile vile, Serikali itatoa Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya kuongoza uratibu wa ufuatiliaji na tathmini ili kupata matokeo tarajiwa.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa wadau, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na sekta binafsi katika kuratibu na kusimamia ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango itapokea na kuchambua taarifa za ufuatiliaji na tathmini kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo – NPMIS. Vilevile, Wizara itaandaa na kutoa taarifa ya mwaka ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutafsiri malengo na viashiria vya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 katika Mipango na Bajeti za kisekta kwa mwaka 2021/22. Aidha, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaelekezwa kuandaa Mpango Kazi pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo, kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo na kuwajengea uwezo watumishi katika tasnia ya ufuatiliaji na tathmini. 
  1. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaendelea kuandaa na kutoa miongozo mbalimbali ya ukusanyaji, uchambuzi na uchakataji wa takwimu za viashiria vinavyosaidia katika ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango. Miongozo hiyo itapaswa kuzingatiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi wakati wa kuandaa taarifa za kitakwimu za mwenendo na matokeo ya utekelezaji wa Mpango. Aidha, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma zitaandaa taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na programu na kuziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Vilevile, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha na Mipango.

MAJUMUISHO

  1. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, Mpango huu ni wa kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Kama inavyofahamika, nchi yetu imefanikiwa kuingia katika kundi la nchi za hadhi ya uchumi wa kipato cha kati kupitia utekelezaji wa Mipango iliyotangulia. Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2021/22 unalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuimarisha utulivu wa viashiria vya uchumi jumla na kasi ya ukuaji wa uchumi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na kuongeza uwekezaji wa viwanda vinavyotumia nguvukazi na malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini hususan mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, madini na gesi asilia, kuendeleza ujenzi wa miundombinu wezeshi na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta mbalimbali ikijumuisha sekta ya viwanda na kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu nchini hususan katika kuwajengea vijana stadi za kazi ili waweze kujiajiri na kuongeza tija katika uzalishaji; na kuchochea maendeleo ya watu kwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya, elimu, maji na umeme vijijini.

HITIMISHO 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ninaomba kutumia fursa hii kuwashukuru wadau wote wa maendeleo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Taasisi za Dini, Washirika wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kujenga uchumi wa nchi yetu. Ushirikiano wao umewezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Ninawaomba waendelee kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mpango ili kufikia malengo tuliyojiwekea.
  1. Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22. Aidha, ninawashukuru watendaji  wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba kwa kusimamia kikamilifu maandalizi ya hotuba hii.
  1. Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii na vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango (www.mof.go.tz).
  1. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.
  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here