Home BUSINESS WATANZANIA WAHIMIZWA KUFANYA UTALII WA NDANI

WATANZANIA WAHIMIZWA KUFANYA UTALII WA NDANI

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wazalendo Halisi. Kulia ni Mwenyekiti Petro Mponzi na kushito ni Sidi Mgumia ambaye ni Makamu Mwenyekiti
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumaro akifafanua jambo kwa wanakikundi cha Wazalendo Halisi  walipotembelea Bunge hivi karibuni

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumaro akiwaeleza wanakikundi cha Wazalendo Halisi  namna ambavyo Serikali inapambana na ujangili katika hifadhi za taifa.

Na: Sidi Mgumia, DODOMA.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kushiriki katika utalii wa ndani.

Ameyasema hayo hivi karibuni mjini Dodoma wakati akizungumza na wanakikundi cha watalii wa ndani maarufu kama Wazalendo Halisi waliokuwa wamealikwa Bungeni ili kujifunza namna linavyoendeshwa.

Dk. Ndumbaro alisema kuwa wizara yake kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika moja kwa moja na utalii wameshusha gharama za utalii wa ndani huku akisisitiza kuwa kutembelea mbuga za wanyama si gharama kubwa kama watu wengi wanavyofikiria.

Alizitaja gharama hizo kuwa ni  tsh 5900, kwenye hifadhi za kawaida na tsh 11,000, kwa hifadhi za Taifa kama vile Ngorongoro , Serengeti na Kilimanjaro na kusema kuwa kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi hizo ni njia mojawapo ya kuendeleza sekta ya utalii ili kuongeza pato la Taifa na utolewaji wa huduma za kijamii.

Kuhusu mapato ya Wizara, Waziri Ndumbaro alisema kuwa kwa sasa sekta ya utalii inaliingizia taifa asilimia 27 ya pato la taifa.

Akizungumzia suala la ujangili, Dk Ndumbaro alieleza kuwa changamoto bado ipo na kusisitiza majangili ni watu tunaoishi nao na kwamba kukabiliana nao inahitajika nguvu kubwa.

Aliongeza kuwa katika kuendelea kukabiliana na janga hilo, Serikali ni lazima iwe macho na watu wanaoanzisha makazi jirani na hifadhi kwani ni kiashiria mojawapo cha ujangili.

“Vijiji vipya navyo tunaamini ni maeneo yanayochangia ujangili , vijiji vinaingia  hifadhini kufanya ujangili, hivi vijiji vipya vinavyoanzishwa, navyo vinasababisha ujangili ukifuatilia kwa makini utabaini malengo yao ni ujangili.”

Akielezea kuhusu wafanyakazi wa hifadhi kufanya kazi kwenye mazingira magumu, alisema serikali imekuwa ikijitahidi kuweka mazingira mazuri kwa watumishi wote wa wizara hiyo ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa umakini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Wazalendo Halisi, Petro  Mponzi alisema wao kwakupitia kikundi chao wamejitolea kuhamasisha utalii kwakutembelea vivutio mbalimbali kwasababu waanaamini ili kuweza kumshawishi mtu kuhusu vivutio hivyo ni vyema ukawa tayari umefika huko kwanza kwani hiyo inakupa nafasi nzuri yakuelezea uzuri wa ulichokiona.

“Tumetembelea maeneo kadhaa ya utalii ambayo kiukweli tumejionea mambo mazuri na tunawasihi watanzania kujitokeza na kutembelea maeneo hayo kwani gharama ni nafuu lakini pia hawatajutia kuona yaliyomo katika vivutio hivyo zikiwemo mbuga za wanyama, maeneo ya kihistoria na vivutio vingine vingi vinavyopatikana ndani ya Tanzania” alisisitiza Mponzi

Naye Katibu wa kundi hilo Felister Fungaredi alisisitiza kuwa ni vyema kuendelea kupenda vya kwetu kwa kutembelea vivutio vilivyomo katika nchi yetu na kuondokana na dhana kuwa vipo kwa ajili ya wageni tu kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mponzi, Wazalendo Halisi ni kikundi kinachoundwa na  watalii wa ndani 21 wakiwemo wanawake na wanaume, huku makao makuu yake yakiwa mkoani Iringa.

Wanachama wa kikundi hicho cha hiari ambao wamejitolea kuwa mabalozi wa utalii baada ya kutambua kuwa jukumu la kuutangaza utalii ni la wote, wanatoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na baadhi wakiwa nje ya nchi.

Malengo yao makuu yakiwa ni kuhamasisha Watanzania kufanya utalii wa ndani na kushiriki katika kufanikisha malengo ya serikali ya kuvitangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya Tanzania.

Katika kufanikisha malengo hayo, wanakikundi hao wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambapo tayari wamekwisha tembelea maeneo kadhaa ya utalii jambo ambalo limewapa fursa ya kuwaelimisha wananchi wengine katika jamii zao juu ya uwapo wa idadi kubwa ya vivutio bora na vizuri vya utalii nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here