Home LOCAL WAMILIKI WA MAABARA BUBU WATAKIWA KUSAJILI MAABARA ZAO

WAMILIKI WA MAABARA BUBU WATAKIWA KUSAJILI MAABARA ZAO

kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt Bones Uiso wakati akifungua mkutano bodi ya maabara binafsi wa uhamasishaji wa huduma za maabara kwa wamiliki wa mkoa wa Arusha.

Msajili wa Bodi ya Maabara binafsi Dominic Fwiling’afu akiongea na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa na wamiliki wa maabara binafsi mkoani Arusha.

Picha ya pamoja ya ya washiriki wa mkutano bodi ya maabara binafsi wa uhamasishaji wa huduma za maabara kwa wamiliki wa mkoa wa Arusha uliotolewa na bodi hiyo.

NA: NAMNYAKI KIVUYO,ARUSHA.

Wito umetolewa kwa wamiliki wa vituo vya Maabara  bubu kuhakikisha wanasajili maabara zao pamoja na kuajiri wataalamu waliosomea na kupata usajili ili kuweza kutoa huduma sahihi kwa jamii.

Wito huo umetolewa na kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Arusha Dkt Vones Uiso wakati akifungua mkutano bodi ya maabara binafsi wa uhamasishaji wa huduma za maabara kwa wamiliki wa maabara  mkoa wa Arusha kwa niaba ya mganga mkuu wa serikali ambapo alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya uwepo wa maabara bubu na kuwepo kwa watoa huduma katika baadhi ya maabara ambao hawajasomea utoaji wa huduma hizo.

Dkt Uiso alisema kuwa wizara ya afya kupitia bodi ya maabara binafsi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa maabara zilizopo nchini zinafuata kanuni na miongozo ili huduma ziweze kuwafikia walengwa kwa usahihi na sio kufanya kitendo cha kimaabara kwa kuhisi na kutoa majibu yasiyo sahihi jambo linalohatarisha maisha ya wagonjwa.

“Maabara ni eneo nyeti sana, bodi inajukumu la kuhakikisha kuwa kanuni na miongozo iliyowekwa inafuatwa na kutekelezwa kwa usahihi lakini pia ni jukumu la watoa huduma kutekeleza kwa vitendo ili huduma bora ziweze kuwafikia walengwa,”Alisema Dkt Uiso.

Alieleza kuwa lengo la mkutano huo ni  kuwafanya wamiliki wa maabara binafsi za mkoa wa Arusha kupata uelewa wa pamoja kuhusiana na sheria, kanuni na taratibu zinazoelekeza majukumu yao kama wamiliki na wadau bodi hasa katika sheria ya namba 10 ya mwaka 1997.

“Mafanikio yatakayopatikana  katika mkutano huu yatachangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma bora za afya  nchini kwani huduma za maabara zina umuhimu wa pekee katika kutambua magonjwa na vyanzo vya magonjwa,” Alisema .

Aidha alifafanua kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kuajiri watu wasio na utaalamu wala usajili kutoka kutoka baraza la wataalamu wa maabara na kuto kusajiliwa kwa maabara pia kuna  baadhi ya waliojisajili kusuasua katika ulipaji wa ada, kuanzisha maabara sehemu ambazo hazitakiwi kuwa na maabara, maabara kutokufuata misingi ya ubora, mashine kutofanyiwa matengenezo na uwepo wa maduka ya dawa yanayofanya huduma za kimaabara.

Kwa upande wake msajili wa bodi ya maabara binafsi Dominic Fwiling’afu alisema kuwa mwaka jana walifanya ukaguzi na lengo la mkutano huo ni kutoa taarifa ya ukaguzi huo na kutoa miongozo nini kifanyike pamoja na kutoa elimu ya namna gani huduma za maabara zinatakiwa kufanyika.

“Kwa mkoa wa Arusha tumekagua maabara 107 na katika ukaguzi huo tulibaini maabara 47 ambazo hazikupitia taratibu za usajili,udanganyifu wa watumishi ambapo kati ya maabara zote maabara 34 tu ndio zilikidhi vigezo vya kulipa tozo za kila mwaka na asilimia 30 tu ndio zinazingatia ubora,” Alieleza Fwiling’afu.

Alifafanua kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa watanzaniawanapata huduma bora  hivyo  katika mkutano huo watajadiliana na kuweka mikakati ambapo pia aliwataka wananchi kutoa taarifa pale wanapona  kuna maabara  zimeanzishwa katika mitaa yao ili ziweze kufuatiliwa kama zimepata usajili na kuzingatia kanuni na sheria za maabara.

Naye  kaimu meneja wa mamlaka ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba kanda ya Kaskazini (TMDA) Proches Patrick alisema kuwa kupitia mkutano huo watatoa na kuhakikisha kuwa wamiliki wa maabara wanapata elimu stahiki ili wananchi waweze kupata huduma bora za kimaabara na kuondokana na changamoto zilizopo.

“Majibu ambayo hayastahili yanaua, yanapelekea mgonjwa kuumwa zaidi hivyo tutaotoa elimu ili maabara ziweze kutoa majibu sahihi kwa ugonjwa fulani yatayopelekea mgonjwa kwenda kupata tiba sahihi,”Alisema.

Alifafanua kuwa wanataka kuona wananchi wanapata huduma bora ambazo zitawahakikishia kwenda kuzitengeneza afya zao ambapo wamekuwa wakifanya ukaguzi katika maabara binafsi na za  serikali kwa lengo la kuhakiki vifaa tiba vinavyotumika katika maabara, vitendanishi lakini pia uhakiki wa uwepo wa bidhaa za serikali zinazotumika katika maabara binafsi.

Alieleza kuwa katika kaguzi hizo wamekuta kuna baadhi ya mapungufu  kadhaa ambayo yatawasilishwa katika mkutano huo kwa lengo la kuhakikisha jamii inaondokana na mapungufu

Hayo ambapo baadhi ni pamoja na maabara binafsi kutumia vifaa tiba na vitendanishi vya serikali jambo ambalo ni kosa kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here