Wadau wa maji bonde la ziwa Tanganyika waliokutana katika mkutano watatu wakujadili mambo mbalimabili yanayohusu sekta ya maji. |
Na, Saimon Mghendi,Kigoma
VIKUNDI vya wadau wa bonde la ziwa Tanganyika vimeiomba serikali kuhakikisha kuwa inatunga sheria kali itakayolinda vyanzo vya maji katika ziwa Tanganyika hali ambayo itaepusha uharibifu wa vyanzo hivyo kutokana na shughuli za kibinadamu.
Wakizungumza jana kwenye mkutano huo wa wadau hao uliofanyika mjini Kigoma kwenye ukumbi wa Bonde la ziwa Tanganyika ambapo wamesema kuwa elimu bado inahitajika hasa kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa vyanzo vya maji ambako wanaendesha shughuli za kilimo.
Aidha jukwaa hilo la Bonde kwa Mkoa wa Kigoma ni mkutano wa tatu uliokutanisha wataalamu na wadau wengine ili kujadili namna bora ya kulinda vyanzo vya maji.
Baadhi ya wadau hao Mekrina Ntamahungilo, mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji mto Mkukuti Kigoma, Kudra Mahamudu Issa ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji mto Mungonya uliopo wilaya ya Kigoma wakichangia mada wamesema tangu kuanzishwa kwa makundi hayo yameleta tija kwa bonde Pamoja na serikali.
Aidha walisema kuwa elimu hiyo imekuwa na tija kwao lakini wakatumia mwanya wa kikao hicho kilichojumuisha viongozi mbalimbali wa Bodi za maji kanda ya Ziwa Magaharibi akiwemo mwakilishi wa Wizara ya Maji George Lugomela ambaye ni mkurugenzi wa raslimali za maji wa wizara ya maji Pamoja na mwenyekiti wa Taifa jukwaa mtambuka la matumizi ya maji Eng.Mbogo Futakamba, wakiiyomba serikali kutunga sheria kali ili kudhibiti wimbi la uharibifu wa vyanzo vya maji kwenye ziwa Tanganyika.
“Ili kukabiliana na uharibifu huo kwenye vyanzo vya maji pamoja na elimu hiyo inayotolewa na vikundi vyetu tunaomba serikali na Wizara kwa pamoja itungwe sheria kali ili na ikiwezekana akikutwa mwananchi amesababisha uharibifu wa miundo mbinu ya maji kwenye vyanzo akamatwe afikishwe polisi na kufunguliwa kesi tukifanya hivyo kwa watu wachache watakuwa na hofu kama ilivyo kwa watu wa misitu wakikukuta porini,” Alisema Kudra.
“Mimi nashauri tuendelee kutoa elimu tusitumie nguvu kubwa mfano kuna wakati tumepata taarifa ya wananchi kufanya uharibifu kwenye chanzo cha maji lakini nashukuru wananchi ni waelewa tuliongea nao kama marafiki baadae wakaachana na mambo waliyokuwa wakiyafanya pembeni ya vyanzo vya maji kwani ukimpelekea polisi utakuwa umemtisha sana,” alisema Mekrina.
Hata hivyo mdau mwingine Simon Mghendi alishauri bodi ya maji bonde la Ziwa Tanganyika kutumia vyombo vya Habari katika kutoa elimu kutokana na kwamba vyombo hivyo vinawafikia watu wengi kwa wakati mmoja kupitia Habari zitakazoandikwa hali ambayo pia itasaidia wananchi kuacha kuharibu vyanzo vya maji vya ziwa Tanganyika.
Wadau hao Walisema kuwa licha ya elimu kuanza kusambaa kwa wananchi kupitia makundi yaliyoanzishwa na bonde wamebaini changamoto lukuki dhidi wananchi wanaoishi pembezoni mwa vyanzo vya maji katika mito na ziwa Tanganyika waliiomba serikali itunge sheria kali dhidi ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji vya ziwa Tanganyika.
Hata hivyo kaimu Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la maji Ziwa Tanganyika Mkoa wa Kigoma,David Manyama akizungumza gazeti hili mara baada ya mkutano huo wa tatu uliohusisha wadau hao Pamoja na wataalamu mbalimbali alisema kuwa shughuli za taasisi hiyo zimeainishwa kwenye sheria Na. 11 ya mwaka 2009 inayoongozwa na sera ya maji ya mwaka 2002.
“Kazi zetu kubwa ni tatu, kwanza ni kulinda vyanzo vya maji lakini katika kutekeleza kazi zote tunakutana na changamoto ya wananchi kukiuka sheria namba 11 ya mwaka mwaka 2009 ambayo inazuia mtu yeyote kufanya shughuli zozote iwe kilmo na mambo mengine ndani ya mita 60,” alisema Mkurugenzi David Manyama.
Pia alitumia mwanya huo kuwaonya wananchi wanaoendelea kutekeleza shughuli zao kwenye vyanzo vya maji na hasa ndani ya mita 60 na kuongeza kuwa kwa yeyote atakaye kiuka sheria hiyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ukilinganisha na kwamba elimu inatolewa mara kwa mara.
picha.