Home LOCAL TGNP , WADAU WATOA MAONI KWA MRENGO WA KIJINSIA KUHUSU BAJETI KUU...

TGNP , WADAU WATOA MAONI KWA MRENGO WA KIJINSIA KUHUSU BAJETI KUU YA SERIKALI MWAKA 2021/22


MAONI YA WADAU JUU YA
BAJETI KUU YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2021/2022

11JUNE 2020.

Bajeti yenye Mrengo waJinsia:
Chachu ya Uchumi Jumuishi, Viwanda na Maendeleo ya Watu

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wadau kutoka asasi za kiraia na vikundi vya kijamii kutoka mikoa mbalimbali nchini tulipata fursa mnamo tarehe 10 Juni mwaka huu, kupitia mjadala wa Bajeti ya Taifa,kufuatilia kwa pamoja na kuchambuabajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 iliyokuwa ikiwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (MB) na baadae kutoa maoni yetu juu ya bajeti hiyo iliyotanguliwa na hotuba ya Hali Halisi ya Uchumi wa Tanzania.

Kama inavyojulikana, Bajeti kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inatoa mwelekeo wa mipango ya maendeleo kwa kila sekta kwa mwaka unaohusika.


Bajeti Kuu ya Serikali ni kielelezo cha jinsi gani Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga na kupendekeza mwelekeo wa namna afua zilizopendekezwa katika sekta mbalimbali zitagharamiwa ili kuleta mabadiliko katika nchi kwa mwaka husika. Hivyo basi, Bajeti Kuu ya Serikali ni kielelezo kikubwa na muhimu sana katika kuashiria jinsi Serikali Kuu inapendekeza kuletea wananchi wake maendeleo kulingana na mahitaji au malengo ya kitaifa.

Bajeti hii ni ya kwanza chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa kwanza Mwanamke nchini na ukanda wa Afrika Mashariki, ambaye ametamka wazi katika hotuba zake mbalimbali kuwa masualaya usawa wa kijinsia ni kapaumbele chake kikubwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali yake ya Awamu ya Sita. Tunatumia fursa hii kumpongeza kwa kuonesha nia ya dhati ya kutekeleza agenda na maono ambayo kama mashirika yanayotetea haki za wanawaketumekuwa tukiipigania kwa muda mrefu sasa.

Tunapongeza Serikali ya Awamu ya Sitakwa kazi wanayoifanya katika kusimamia utekelezaji wa sera, na mipango ya maendeleo kwa manufaa ya taifa na watanzania. Hali kadhalika yako mambo ambayo bado yanahitaji kuongezewa nguvu ili kuhakikisha tunafikia lengo la kuwa na maendeleo endelevu yenye kujumuisha ustawi wa makundi yote na kudumisha haki za msingi za binadamu ikiwemo usawa wa jinsia, katika kufikia azma ya Serikali ya awamu hii ya kufikia uchumi shindani, viwanda na maendeleo ya watu.

Tumeshuhudia kuwepo kwa jitihada zenye lengo la kuboresha sekta za huduma kwa jamii, sekta ambazo kwa kiwango kikubwa zinawagusa wanawake moja kwa moja. Jitihada hizo ni pamoja na kuboresha miundo mbinu ya huduma za afya kama vile ujenzi wa hospitali 99, hospitali 10za rufaa za mkoa, zahanati 1,198, ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Mwananyamalana kufikia asilimia 51 ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo la kina mama na mtoto. katika mkoa wa Simiyu. Hatua hizi zimechangia kwa kiasi fulani kupunguza vifo vya kina mama na watoto. 

Pamoja na juhudi hizo bado kuna changamoto katika upatikanaji wa huduma za uzazi salama bila gharama kubwa au tozo, hususani kwa wanaohitaji upasuaji.Tunaamini kuwa hawa wanawake wanaoleta nguvu kazi ya taifa hawatakiwi kulipia huduma hiyo kabisa kwani ili taifa liendelee linahitaji watu na wanaoleta watu duniani ni wanawake; wanahitaji kuenziwa kwa kazi hiyo nzito.

Kwa upande mwingine, bado kuna upungufu wa vituo vya afya na zahanati kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini na mijini, jambo ambalo linasababisha changamoto kubwa sana kwa wanawake hasa wale wajawazito na waliofikia hatua ya kujifungua; bajeti pia haijaanisha kwa kiwango gani imejipanga katika kupunguza upungufu wa watumishi wa afya; baadhi ya vituo vya afya hasa vijijini havina huduma za maji na umeme.

Kwa upande wa upatikanaji wa maji, Serikali imefanikiwa kwa kiwango fulani kumtua ndoo mama vijini na mijini kwa asilimia 72.3 na 85 kufikia kukamilika kwa
miradi 1845 ya maji vijijini na mijini.  Pamoja na miradi hii kukamilika lakini bado tatizo la maji ni changamoto maeneo mengi hususani vijijni ambapo ndipo wananchi wengi wanaishi na pia kwenye taasisi za umma kama vituo vya afya na taasisi za elimu. Tukumbuke kuwa maji ni huduma kwa namna yoyote huduma ya maji isigeuke kuwa chanzo cha mapato au biashara. 

Kwa upande wa elimu, Serikali imepanga kufanya mapitio ya Sera ya Elimu kuendana na muktadha uliopo, tunatarajia ushiriki mpana wa wadau mbalimbali katika mchakato huu muhimu. Pia,Serikaliimeendelea kuongeza fursa ya kila mtoto kwenda shule kwa kugharamia elimu msingi bila ada. 

Ikumbukwe kuwatangu elimu bila ada ianze sasa ni miaka 7, hivyo uhitaji wa wanafunzi kuingia kidato cha kwanza utakuwa kubwa,ni matumaini yetu kuwa maandalizi yamefanyika hasa katika kutenga rasilimali za kutosha kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba watapata fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari bila vikwazo.

Hata hivyo, katika kumkomboa mtoto wa kike shuleni, bajeti imeendelea kuwa kimya katika upatikanaji wa sodo (pedi/ taulo za kike) na miundo mbinu ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike, walio kwenye mfumo wa elimu ya msingi na sekondari. Bajeti haijataja mafungu au kutoa maelekezo yoyote kwa Halmashauri za Wilaya, au mamlaka za elimu kuyazingatia mahitaji haya katika mafungu ya fedha wanayopata. Kuna umuhimu wa serikali kutoa maelekezo ya kuwezesha upatikanaji wa bajeti hii ili kuwasaidia wanawake na watoto wa kike kuondokana na fedheha na changamoto za kiafya wanazokutana nazo wakiwa katika hedhi kwa kukosa vifaa safi na salama vya kujisitiri wakiwa katika hedhi.

Tunaendelea kutoa wito kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sitainayojali usawa wa jinsia kuondoa tozo ya VAT kwenye pedi ambayo ilirudishwa mwaka 2019. Kama kodi ya VAT imeondolewa kwa bidhaa nyingine ni muhimu kuangalia hili suala kwa jicho makini zaidi kusaidia wanawake na wasichana.

Katika sekta ya kilimo, sekta ambayo inawaajiri wanawake kwa zaidi ya asilimia
57.  Serikali ya Awamu ya Sitaimetoa kipaumbelekatika kuimarisha sekta ya kilimo kutoa mali ghafi kwa ajili ya viwanda. Tunatarajia juhudi hizi zitasaidia ushiriki wa wakulima wadogo wadogo ambao wengi wao ni wanawake ili waweze kufaidika na juhudi hizi.

Hata hivyo, bado bajeti haija chambua kwa umakini changamoto za ufikiaji wa maeneo ya kilimo kwa vijana na wanawake, na kuhusu changamoto za ufikiaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali kwa wakulima wanawake na vijana. Aidha, Bajeti Kuu ya Serikali pia haikuelekeza kwa ufasaha jinsi makundi ya wanajamii wanawake na vijana wanavyostahili kuelekezewa mitaji na mikopo ya kilimo, au kuelekeza kiwango fasaha mikopo na mitaji kwa makundi hayo.Tumefarijika kuwa gharama za kulipia umiliki wa ardhi na kurasimisha ardhi zimepungua tunaipongeza serikali
kwa hili.

Kwa upande wa uziduaji, bajeti ya Serikali Kuu na ile ya kwenye sekta ya uziduaji,
haijaainisha kwa ufasaha jinsi gani wanawake na vijana walio kwenye sekta ya uziduaji wanamilikishwa na kulindwa kisheria katika maeneo yao ya uchimbaji, na kupatiwa mitaji, mikopo, maarifa, na teknolojia chanya za kuboresha harakati zao za kujichumia mapato kupitia sekta hii.

 

Kukabiliana na mapungufu tuliyoainisha, tunapendeleza yafuatayo: 

 

Sekta ya Elimu.

Tunapendekeza Serikali, kupita sekta ya elimu, VETA na SIDO kuhakikisha kwamba mafunzo ya stadi mbalimbali za ufundi na sayansi yanaongeza udahili wa wasichana na vijana wa makundi ya pembezoni ili kunufaika na ajira zenye tija. Pia, Serikali itoe maelekezo kwa  Halmashauri za Wilaya kutenga asilimia ya fedha za “capitation grant” kuhudumia mahitaji ya hedhi salama kwa wanafunzi wa elimu ya msingi.

 

Sekta ya Afya.

Tunapendekeza,serikali itenge bajeti yenye kulenga na kuhamasisha utoaji wa Bima za Afya kwa gharama sawa na bure kwa wajane wenye uhitaji, wazee na wanawake na kaya masikini nchini.

  

Pia, tunakumbusha serikali kutimiza makubaliano ya Abuja, ambayo nchi imeridhia, ya kutenga asilimia 15 ya bajeti kuu kwa jili ya bajeti ya afya. Tunatoa wito kwa Serikali na wadau wengine kuongeza uwekezaji katika kutoa elimu ya umuhimu na namna ya kuzuia magonjwa ili kupunguza gaharama za matibabu ya magonjwa yanayozuilika. Ujenzi wa uchumi shindani wa viwanda na maendeleo ya watu unahitaji nguvu kazi ya afya bora.

 

Sekta ya Maji.

Tunapendekeza Serikali kuelekeza sekta ya maji kutanua na kujazilisha (densification) mtandao wa huduma ya maji safi na salama, kwa kuweka mikakati ya kupata fedha zitakazowezesha suala hilo. Pia, Serikali kuelekeza sekta ya maji kuondoa tozo za maji kwa taasisi za umma kama shule na vituo vya huduma za afya. Pia, Wizara ya maji kutoa maelekezo kwa idara za maji za mikoa kuwezesha upatikanaji wa maji kwa wajane, wazee, kwa tozo za viwango vya chini kabisa, au
hata bila tozo yoyote. Vituo vya kulelea Watoto wenye chanagamoto na vituo vya
wazee vipewe maji bila gharama yoyote.

 

Sekta ya Kilimo.

Kufanikisha ushiriki wa wanawake na vijana katika uchumi shindanishi, tunapendekeza  sekta ya kilimo itenge rasilimali za kutosha kuwalenga wanawake na vijana katika ufikiaji wa mikopo ya masharti au riba nafuu, upatikanaji wa teknolojia sahihi za uzalishaji na uhifadhi, na  ufikiaji rahisi wa masoko wezeshi, ufikiaji sahihi wa taarifa za tafiti za mbegu bora na mifumo ya kilimo cha umwagiliaji, upokeaji wa taarifa za tafiti za Taasisi za Kilimo, na kuwa wateja wakuu wa
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). 

 

Pia, Serikali izielekeze Halmashauri za Wilaya kwa makusudi, kujenga masoko mapya kwenye maeneo yenye mvuto mkubwa kwa bidhaa za wajasiriamali wanawake na vijana. Pia, tunakumbusha serikali kutimiza makubaliano ya Malabo, ambayo nchi imeridhia, kutenga asilimia 10 ya bajeti kuu kwa ajili ya bajeti ya kilimo. 

 

Sekta ya Uziduaji.

Tunapendekeza sekta ya uziduaji ielekeze jitihada kubwa zaidi kuhakikisha vijana na wanawake
waliyo kwenye shughuli za uziduaji wanamilikishwa maeneo yao, wanapatiwa mafunzo
na teknolojia za uchimbaji wa kisasa, wanapewa taarifa za kitaalam kuhusu upatikanaji wa madini, wanajengewa mbinu mpya za uchimbaji na uziduaji, na kuhakikishiwa ufikiaji wa masoko na bei wezeshi kwa bidhaa zao za madini.

 

Kwa ujumla tunapendekeza,

 

·  Bajeti ya Serikali itoe matamko na maelekezo kwa watumishi wa Serikali kusimamia utoaji wa asilimia 30 ya kandarasi za umma, na ajira wapewe wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama sera na kanuni zinavyoelekeza.

 

·  Aidha mifumo ya kidijitali iwe rafiki zaidi kwa wanawake na vijana wa pembezoni katika kupasha na kupokea taarifa za kibiashara na masoko. 

 

·  Bajeti ya Serikali Kuu ielekeze sekta ya Viwanda na Biashara, na pia TAMISEMI, kuongeza ufikiaji wa huduma za masoko kwa bidhaa zinazozalishwa na wanawake na vijana wa pembezoni ili waweze kunufaika na uchumi shindani, na Maendeleo ya viwanda.

 

· Serikali iongeze nguvu katika kubuni vyanzo vya mapato ambavyo havimuumizi au kumuongezea mzigo mwananchi wa kawaida hususani wanawake. Kuongeza makato kwenye mafuta kutamuongezea moja kwa moja mzigo mwananchi wa kawaida kwa ongezeko hili kuna uwezekano mkubwa wa bidhaa na huduma mbambali kupanda gharama.

 

Imetolewa na,

Lilian Liundi,

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)

Kwa niaba ya wadau walioshiriki mjadala wa bajeti ya Taifa, 2021/22.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here