NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Solomon Mwangamilo amewataka waendesha bodaboda kuwa na nidhamu ya kazi kwa kuithamini na kuikubali biashara ya kubeba abiria kuwa ni kazi na ajira rasmi ikiwa ni pamoja na kutokuwafumbia macro wachache wanaharibu biashara hiyo kwa kutenda uhalifu.
SP Mwangamilo alitoa rai hiyo Katika kikao chake na waendesha bodaboda wanaofanya shughuli ya kubeba abiria Jiji la Arusha kwa kata ta wanajumuisha kata tatu ambazo ni kata ya kati, Levolosi na Kaloleni.
Alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kuwajengea uwezo waendesha bodaboda kuhusiana na suala zima la utii wa sheria za usalama barabarani, kuongeza ushirikiano baina ya bodaboda na Jeshi la Polisi hasa katika mapambano dhidi ya uhalifu sambamba na kupunguza matukio ya ajali za barabarani.
Alieleza kuwa vitendo vya uhalifu barabarani kwa baadhi ya vijana hutokana na mihemko ya ujana na kutolea mfano kupasua mfumo wa upumuaji maarufu kwa jina la exosti na kulipua milipuko mikubwa mithili ya baruti, ambapo vitendo hivyo huleta usumbufu na taharuki kubwa kwa watu wengine hususani maeneo ya mahospitali.
Aidha alitoa wito kwa vijana kutambua kuwa wao ni sehemu ya jamii, hivyo wanawajibu mkubwa wa kufichua wahalifu na matukio ya uhalifu katika maeneo yao ili Jiji la Arusha liendelee kuwa shwari hasa kwa kuzingatia ni kitovu cha utalii nchini.
“Hawa vijana ambao wanafanya mihemko na kufanya uhalifu wa barabarani ama wa kijinai wanatoka katika jamii, kwaiyo muwe wa kwanza kuchukia vitendo hivyo, tufikishieni taarifa sisi jeshi la Polisi kwa mficho ili tuweze kuwafikia wale watu wachache ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.” Alisisitiza SP Mwangamilo.
Kwa upande wake Katibu wa bodaboda kata ya Levolosi Hemed Mbaraka alisema kutoka na kikao hicho jiji la Arusha litaenda kubadilika kwani wao kama bodaboda wataenda kuhimizana suala la utii wa sheria sambamba na kukemea matendo mengi ya kiuhalifu ambayo yalikuwa yanaonekana yanatendwa na bodaboda.
Naye Johnson Lema dereva bodaboda toka kituo cha Namanga alisema watahakikisha wanaenda kushirikiana na Jeshi la Polisi kukamata pikipiki zote zinazotenda uhalifu hususani zile ambazo zinatoa milio mikubwa na kuzifikisha katika vituo vya Polisi.
Pia Lema aliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua baadhi ya bodaboda ambao wanatabia ya kuvamia vituo ambavyo hawajasajiliwa baada ya kutenda uhalifu katika maeneo yao.
Hata hivyo kikao hicho kimehudhuriwa na madereva bodaboda zaidi ya 100 ni muendelezo wa vikao vya Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha na wadau wa usalama barabarani hususani makundi ya bodaboda ambavyo vinafanyika kila wiki.
Picha
0031 Ni
0032 Ni .