Home LOCAL NIPE FAGIO YASISITIZA UMUHIMU WA MAZINGIRA SAFI NA SALAMA KWA WATOTO.

NIPE FAGIO YASISITIZA UMUHIMU WA MAZINGIRA SAFI NA SALAMA KWA WATOTO.

Mratibu Sera kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali Nipe Fagio, Bi Veronica Hollela (Kulia) akizungumza kuitambulisha Taasisi wakati sherehe za kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika zilizofanyika katika Shule ya Msingi Bonyokwa katika manispaa ya Ilala.  Katikati ni Mratibu Mawasiliano wa Taasisi hiyo Muddy Kimwery na Afisa Uhamasishaji Jamii Abdallah Mikulu (Kushoto). 


Mwenyekiti wa Mtaa wa Bonyokwa uliopo katika Manispaa ya Ilala, Bw. Shabani Maliyatabu akizungumza kuwakaribisha wageni waalikwa wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika zilizofanyika katika Shule ya Msingi Bonyokwa katika manispaa ya Ilala.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Nipe Fagio wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wa Bonyokwa uliopo katika Manispaa ya Ilala, Bw. Shabani Maliyatabu (wapili kushoto) wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika zilizofanyika katika Shule ya Msingi Bonyokwa katika manispaa ya Ilala.

Na: Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM.

 

KATIKA kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, taasisi isiyo ya kiserikali ya Nipe Fagio imesisitiza kuwa ni muhimu serikali, taasisi, makampuni yanayozalisha taka na jamii kwa ujumla kuongeza jitihada katika utunzaji wa mazingira ili kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa mazingira.

 

Hayo yamezungumzwa na Mratibu Sera wa Taasisi ya Nipe Fagio, Bi Veronica Hollela wakati wa tukio maalum lililofanyika katika Shule ya Msingi Bonyokwa la kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 16 mwezi Juni kila mwaka.

 

Bi Veronica amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa mtoto anaishi na anasema katika mazingira Safi na Salama ni lazima jamii, serikali na wadau mbali mbali waupokee mfumo wa Taka Sifuri ambao ni mfumo endelevu na jumuishi wa usimamizi na udhibiti wa Taka ngumu kuanzia kwenye uzalishaji uhifadhi, usafirishaji na utumiaji wa bidhaa.

 

“Ni muhimu jamii ijifunze kutenganisha taka kwa ajili ya kurahisisha uhifadhi na utumiaji wa taka kama rasilimali ikiwemo utengenezaji wa mbolea ya mboji itokanayo na taka ozo na urejelezaji wa taka,” alisema Bi. Veronica.

 

Aliongeza kuwa mfumo huu wa Taka Sifuri ni muhimu sana kwa sababu ni mfumo unaotoa fursa ya ajira kwa jamii, na pia ni mfumo unaohakikisha mtaa unakuwa na safi na salama kwa watoto na jamii kwa ujumla. Huu ni mfumo unaomilikiwa na jamii kwa asilimia mia moja wakiwemo watoto ambao ni taifa la leo.

 

Aidha naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Bonyokwa Bw. Shabani Maliyatabu katika tukio hilo alisema kuwa jambo la muhimu ni kuwasisitiza wazazi na walezi kwamba nyumbani pawe chou cha mambo na matendo mema, ugomvi na vurugu nyumbani upelekea kuharibu mienendo na tabia za watoto wengi.

 

“Mzazi au mlezi ukiwa rafiki kwa mtoto na mtoto atakuwa rafiki kwa familia na kuwa na matendo na maadili mazuri,” alisema Bw. Maliyatabu.

 

Bw. Maliyatabu aliishukuru taasisi ya Nipe Fagio kwa kushiriki maadhimisho hayo lakini pia kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo za kata yake ya Bonyokwa hususani katika sekta ya mazingira kwa kuhakikisha Bonyokwa inakuwa safi na salama kwa Watoto na jamii nzima.

 

Mwisho.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here