Na: Faraja Mpina, DODOMA.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amefanya mazungumzo na watendaji wakuu wa kampuni za simu na kuwapa angalizo kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni mali ya Serikali hivyo ujenzi, upanuzi na uendelezaji wake upo chini ya Serikali na sio makampuni ya simu kufanya ujenzi wowote wa Mkongo wa Mawasiliano.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika kikao chake kilichoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kufanyika jijini Dodoma leo (Juni 7,2021) kikilenga kuzungumzia mkakati wa Mfuko huo kutangaza awamu ya sita ya zabuni ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo yenye usikivu hafifu na mipakani.
Aidha, Dkt. Ndugulile ametumia kikao hicho kuyaalika makampuni ya simu kushiriki katika zabuni hizo zitakazotangazwa hivi karibuni na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutengeneza mazingira wezeshi ya kufanya uwekezaji katika maeneo mengi zaidi nchini ili kuwafikishia wananchi huduma za mawasiliano kwasababu ni haki yao ya msingi na Wizara yake ina wajibu wa kuwafikishia wananchi huduma hiyo.
“Huduma ya mawasiliano sio anasa ni huduma ya msingi ambayo kila mwananchi anatakiwa kufikishiwa huduma hii kwa kuangalia uhitaji wake kibiashara, kiusalama, kijamii na kiuchumi”, alizungumza Dkt. Ndugulile.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amewaasa watoa huduma wanapojenga minara ya mawasiliano kuhakikisha wanakuwa na nishati mbadala kwasababu nishati ya mionzi ya jua inayotumika kwenye minara hiyo katika baadhi ya maeneo haiwezi kufanya kazi wakati wa usiku na kusababisha kutokupatikana kwa huduma ya mawasiliano kitu kinachohatarisha usalama wa eneo husika.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba amesema kuwa anaamini makampuni ya simu wataichukulia kwa uzito stahiki zabuni hiyo pindi itakapotangazwa na Mfuko huo ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafikishwa katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano na maeneo ya mipakani ambayo yanagusa pia usalama wa nchi.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya simu ya Airtel Dkt. Prosper Mafole amesema kuwa amefurahishwa na ahadi ya Wizara hiyo ya kujenga kilomita 1880 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwenda katika ngazi za makao makuu ya wilaya ambapo ujenzi huo utatatua changamoto kubwa ya ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Ufundi wa Vodacom Andrew Lupembe ameishukuru Wizara kwa ushirikiano inayotoa kwa makampuni ya simu na kutoa kipaumbele cha Mkongo wa Taifa ambao utajengwa katika mfumo ambao upande mmoja ukikatika upande mwingine unafikisha mawasiliano kwa wananchi.
Mpaka sasa Serikali imejenga kilomita 7610 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchini, huku ujenzi wa kilomita 409 ukiendelea na kilomita 1880 zikipangwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa lengo la kuendelea kuwafikishia wananchi huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari