Home LOCAL KUTOKA BUNGENI JIJINI DODOMA MHE, EDWIN SWALLE ASIMAMA NA WANANCHI WA LUPEMBE,...

KUTOKA BUNGENI JIJINI DODOMA MHE, EDWIN SWALLE ASIMAMA NA WANANCHI WA LUPEMBE, ASHAURI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA UMEME VIJIJINI,

 Na:Maiko Luoga. 

“Asante sana Mhe, Spika kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya nishati, Mhe, Spika kwanza niungane na Wabunge wenzangu kutoa pongezi nyingi sana kwa Mhe, Waziri, Naibu Waziri wake na timu nzima ya Wizara hii kwa kazi njema wanayoifanya”

“Hata mimi ni shuhuda ambae nimekuwa nikiongea na Mhe, Waziri na Naibu Waziri wamekuwa wasikivu sana, Mhe, Spika Sera yetu ya Umeme inasema, umeme kila Kijiji hata kwenye Hotuba ya Mhe, Waziri inaeleza idadi ya Vijiji ambavyo bado havijapata umeme vitapata”

“Lakini sisi katika Jimbo la Lupembe Mhe, Spika bado tupo kwenye shida ya kupata umeme kwenye ngazi ya Kata zipo Kata ambazo hazina umeme kabisa ukiacha Vijiji, Mhe, Spika Kata kama za Ukalawa, Ikondo, Mfriga, Idamba, hakuna Umeme”

“Katika maeneo haya kulikuwa na Mtu binafsi alikuwa na umeme unaitwa CEFA ambao Wizara waliwapa nafasi ya kutoa umeme kwa baadhi ya Vijiji lakini Mhe, Spika kwa masikitiko makubwa sana ule umeme wa CEFA kwanza ni bei ghari sana kwakuwa ni wa binafsi”

“Pili umeme ule umekuwa na changamoto hauna uwezo wa kuendesha hata mashine ya kusaga, Mhe, Spika vipo baadhi ya Vijiji maeneo ya Image ikifika jioni saa mbili Wananchi wamerudi majumbani wakiwasha Televisheni zao hawawezi kuona kwakuwa umeme ule hauna nguvu”

“Hata Redio za kawaida umeme huu hauna uwezo wa kuendesha, kilichobaki sasa Wananchi wanaendesha mashine na redio zao kwenye sehemu za Starehe kwa kutumia mafuta”

“Naishauri sana Serikali katika karne hii ya ishirini na moja muda ambao tupo katika sera ya Viwanda kuwa na Jimbo ambalo hata umeme kwenye Kata haujafika Mhe, Spika hatutendi haki kwa Wananchi hawa”

“Jimbo la Lupembe Mhe, Spika lina fursa nyingi za utajiri kwaajili ya Viwanda, Lupembe tunalima sana zao la Chai kuna Viwanda zaidi ya viwili vinahitaji umeme, Pia tunalima sana matunda hasa Nanasi”

“Wapo watu wengi wanania ya kuwekeza kwenye nanasi maeneo kama ya Madeke lakini kwasababu hakuna nishati ya umeme wanashindwa kuweka Viwanda ambavyo vingetoa ajira nyingi sana kwa Vijana wetu”

“Kulikuwa na fursa nzuri ya kuweka Viwanda vya zao la Parachichi kwenye Jimbo hili la Lupembe lakini kwasababu ya changamoto ya ukosefu wa umeme Mhe, Spika wawekezaji wengi hawaji tena”

“Mhe, Spika naishauri sana hii Wizara ya Nishati kwenye maeneo ambayo kuna umeme kiasi wa REA kuna shida kubwa na mara kadhaa nimezungumza na Mhe, Naibu Waziri Mhe, Byabato kwamba umeme ambao upo nao umekuwa kero ni bora hata usingekuwepo”

“Wananchi wana mashine zao mteja amefika kusaga unga kabla hajamaliza umeme unakatika kwahiyo Mwananchi anashindwa kwenda kufanya kazi nyingine anakaa kusubiri hadi umeme urudi na haujulikani utarudi saa ngapi”

“Wananchi wana mashine ndogo katika Viwanda vidogo vya kuranda mbao kama kuna msiba umetokea inatakiwa waandae mbao kwaajili ya shughuli ya msiba umeme unakatika, kukatika Umeme ni tatizo kubwa kwa nchi nzima, namwomba sana Waziri kama walivyozungumza Wabunge wengi hapa hii nishida ukiachilia mbali kupeleka umeme kila Kijiji, kuwa na umeme ambao hauna uhakika ni kero kubwa Mhe, Spika” 

“Mhe, Spika wapo Wananchi wamepata hasara sana wameunguza Redio na Mwananchi wangu mmoja mpaka nyumba yake imeungua Mhe, Spika kwasababu ya kero ya umeme kukatika kila wakati”

“Pamoja na sifa nyingi tulizotoa kwenye Wizara yake nimwombe Mhe, Waziri tatizo la umeme kukatika, Umeme kutotabirika, kutokuwa na nguvu, Wizara hii itoe kipaumbele cha kuboresha isiwe tu kipaumbele cha kupeleka umeme kwenye kila Kijiji”

“Naunga mkono hoja, alimaliza Mhe, Edwin Esoss Swalle Mbunge wa Jimbo la Lupembe CCM Mkoani Njombe akichangia Wizara ya Nishati Bungeni Jijini Dodoma.

Previous articleSERIKALI YATOA MSIMAMO WA CHANJO NCHINI
Next articleDIWANI MALISA AOMBA ENEO LA HALI YA HEWA KUJENGA SHULE NA ZAHANATI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here