Home LOCAL BILIONI 9 ZALIPWA UJENZI WA MAKAO MAKUU YA UHAMIAJI DODOMA.

BILIONI 9 ZALIPWA UJENZI WA MAKAO MAKUU YA UHAMIAJI DODOMA.

Na: Abubakari akida, DODOMA.
Shilingi Bilioni 9.1 zimelipwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa SUMA JKT ikiwa ni sehemu ya malipo ya gharama ya Ujenzi wa Mradi wa Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dodoma ambao kukamilika kwake utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 20.

Hayo yamesemwa na Mhandisi wa Mradi huo, Issa Mohammed akisoma taarifa ya mradi huo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi oktoba mwaka huu.

“Lengo letu ni kumaliza mradi huu katikati ya mwezi Oktoba, pamoja na kuzingatia muda bado tunachukua tahadhari kubwa kuhakikisha ubora na uimara unaotegemewa kufikiwa kuanzia kwenye msingi hadi kukamilisha mradi mzima huku tayari tukiwa tumeshalipwa kiasi cha fedha Bilioni 9.1/=  hii ikijumuisha malipo ya awali kwa ajili ya watoa huduma  ambayo thamani yake ni Bilioni 1.3” alisema Mhandisi Issa

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo alisema miradi hii iliyoachwa na Hayati John Magufuli ni muhimu imalizwe ili kiasi hicho cha fedha za Watanzania kitumike ipasavyo.

“Miradi hii imetumia fedha nyingi tena fedha zetu za ndani,ifike wakati miradi hii ikamilke  maana hakuna fedha iliyotoka nje kwa maana msaada kwahiyo kazi iendelee ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, nawaomba wafanyakazi wafanye kazi usiku na mchana ili jengo hili lianze kutumika kama lilivyokusudiwa” alisema Naibu Waziri Khamis

Mradi huo ulianza rasmi tarehe 28 Mei mwaka 2019 ukijumuisha ujenzi wa jengo la Ofisi lenye urefu wa ghorofa nane na sakafu ya chini, uwekaji wa mifumo ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na kusawazisha ardhi ya nje ya jengo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here