Home LOCAL ASKOFU MKUU WA ANGLIKANA DKT. MNDOLWA AWASISITIZA WAUMINI WA KANISA HILO KUFUATA...

ASKOFU MKUU WA ANGLIKANA DKT. MNDOLWA AWASISITIZA WAUMINI WA KANISA HILO KUFUATA KANUNI ZA IBADA.

 Na: Maiko Luoga TANGA. 

Waumini wa Kanisa Anglikana Tanzania wamesisitizwa kufuata Kanuni na taratibu za Ibada kwa kutumia miongozo ya Vitabu vya Sala, nyimbo za Dini na nyimbo Standadi za Kanisa Anglikana Tanzania ili kuimarisha kicho cha Ibada na kuwasaidia Vijana kulijua Kanisa na mambo yake. 

Wito huo umetolewa Juni 26, 2021 na Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Dkt, Maimbo Mndolwa wakati akitoa huduma ya Kipaimara kwa Wanafunzi wa Makanisa ya Anglikana Magula, Misozwe na Mt, Blandina Mlingoti yaliyopo Wilayani Muheza Dayosisi ya Tanga. 

“Kanisa Anglikana linaendeshwa kwa Kanuni na Taratibu pamoja na uimbaji wa nyimbo zetu binafsi, tunapaswa kuzifahamu na kuzitumia nyimbo za Dini na nyimbo Standadi ambazo ndio ibada kamili ya Kanisa, sasa tumeacha vyetu tunatumia vya wengine naomba tubadilike hata hao waliomba nyimbo zetu hapo awali” Askofu Maimbo Mndolwa. 

Aidha alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha waumini wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tanga kuhakikisha wanaendelea kuibua maeneo ya ujenzi wa makanisa mapya, kuboresha majengo yaliyopo ambayo ni makongwe sambamba na kushiriki kueneza injili ili kuwaokoa wengine.

Canon Christopher Kiango Kasisi kiongozi Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tanga ametoa wito kwa Makasisi kuhakikisha wanaweka alama za utambuzi wa makanisa kwenye maeneo yao ili Jamii iyatambue kwa haraka pindi inapohitaji msaada wa Kanisa katika eneo husika.

“Tuweke vibao kuyatambulisha makanisa yetu ili Jamii inapohitaji huduma ijue Kanisa Anglikana linapatikana wapi kwenye eneo gani pia itasaidia kuwatambulisha wageni wanapotutembelea kwenye maeneo yetu” alieleza Canon Christopher Kiango Vicar General Tanga.

Baadhi ya Waumini wa Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga wamepongeza jitihada za uongozi wa Dayosisi hiyo za kuendelea kuimarisha uhai wa Kanisa na watu wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here