Home LOCAL WIZARA YA AFYA YATOA MAFUNZO KWA WABUNGE KUHUSU MAGONJWA YA KIFUA KIKUU...

WIZARA YA AFYA YATOA MAFUNZO KWA WABUNGE KUHUSU MAGONJWA YA KIFUA KIKUU NA UKOMA1


NA:  WAMJW-DODOMA.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imetoa mafunzo kwa wabunge wa Bunge la Tanzania kuhusiana na magonjwa ya Kifua Kikuu na Ukoma ili kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu magonjwa haya mawili yanayosumbua jamii.

Akiongea wakati ufunguzi wa mafunzo hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wajumbe wengi wa kamati ya bunge ya masuala ya ukimwi, kifua kikuu na madawa ya kulevya waliomba na kupendekeza kuandaliwa kwa mafunzo mahususi kwa ajili ya kuongeza ufahamu wa magonjwa ya Kifua Kikuu na Ukoma.

Dkt. Gwajima amesema Mwaka 2006, Serikali iliitangaza rasmi ugonjwa wa TB kuwa Janga la Kitaifa ambapo mwenendo wa utekelezaji katika kudhibiti TB hapa nchini unaonesha kuwa nchi imefanikiwa katika kupunguza vifo na maambukizi mapya yatokanayo na ugonjwa wa Kifua Kikuu.

“Ripoti za Shirika la Afya duniani zinaonesha kwamba nchi yetu inafanya vizuri katika mapambano ya kudhibiti Kifua Kikuu, Pamoja na mafanikio haya bado tuna changamoto ya kumfikia kila mtanzania mwenye tatizo hili”. Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima ameongeza kuwa Matibabu ya TB yanagharimiwa na Serikali katika kituo chochote cha afya bila kujali kama ni cha Umma au binafsi, mgonjwa hapashwi kutozwa malipo yoyote. 

Ameendelea kusema kuwa TB inaweza kumpata mtu yoyote bila kujali jinsia, cheo, au umri na kuitaka jamii kufuata kanuni za afya ili iweze kujiepusha na maambukizi mapya.

Hata hivyo Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa TB inatibika na kupona kabisa iwapo mgonjwa atawahishwa katika kituo cha kutolea huduma za afya, lakini endapo atacheleweshwa na kuwekwa kwenye utaratibu wa matibabu anaweza kupoteza maisha.

Kwa upande wa ugonjwa wa Ukoma, Waziri Gwajima amesema nchi yetu ilifikia kiwango cha kimataifa cha utokomezaji mnamo mwaka 2006, kwa sasa nchi imejielekeza katika mbinu na mikakati ya kukamilisha utokomezaji katika Halmashauri chache zipatazo 21 ambazo hajizifikia viwango vya utokomezaji ifikapo mwaka 2025. 

Mwisho Waziri Gwajima amesema ni matarijio ya Wizara mafunzo hayo kwa wabunge  yataongeza ufahamu juu ya magonjwa haya na hivyo kuongeza chachu ya kuyatokomeza. Pia yatasaidia kuongeza hamasa katika Jamii hususani katika kupambana na ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao bado ni tatizo kubwa nchini.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here