Home BUSINESS WAKULIMA KUNUFAIKA NA NHIF KUPITIA CRDB

WAKULIMA KUNUFAIKA NA NHIF KUPITIA CRDB

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela wakibadilishana mkataba baada ya kusaini makubaliano ya kuhudumia wakulima kupata bima ya afya

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela wakisaini mkataba wakishuhudiwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dk. Benson Ndiege

 

 

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela wakifurahi na kuonesha mkataba huo baada ya kusaini rasmi.
Menejimenti ya NHIF na CRDB wakishuhudia tukio hilo

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetanua wigo wa wakulima kujiunga na huduma zake kwa kuweka utaratibu rahisi kupitia Benki ya CRDB.

Hatua hiyo imefikiwa leo baada ya NHIF na Benki ya CRDB kusaini mkataba utakaowawezesha wakulima ambao wako kwenye vyama vya ushirikia vya msingi kulipiwa na CRDB mchango wa mwaka wa bima ya afya ambao wataurejesha bila riba wakati wa msimu wa mavuno.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema kuwa Mfuko umefikia uamuzi huo kwa lengo la kuhakikisha unawafikia wakulima wengi zaidi na kuwahakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu wakati wowote.

“Jambo hili la ushirikiano na CRDB ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wetu Mhe. Samia Hassan Suluhu ambaye ameweka msisitizo mkubwa katika suala la wananchi kuwa na bima ya Afya, hivyo tunaamini tutawafikia wakulima wengi zaidi kutokana na ushirikiano huu,” alisema Mkurugenzi Mkuu Bw. Konga

Alisema kuwa kupitia mpango huo wa Ushirika Afya, zaidi ya wakulima 300,000 wanatarajiwa kujiunga na huduma za NHIF hatua ambayo itasaidia sana wakulima kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu lakini pia uhakika wa uzalishaji wao kupitia kilimo.

“Mpango huu ni rahisi na hauna gharama ya ziada kwa mkulima atakayenufaika kwani ataanza kutumia huduma za matibabu na atalipa baada ya kuuza mazao yake na malipo hayo hayana riba yoyote,” alisema Bw. Konga.

Alisisitiza umuhimu wa wakulima hao kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kutumia fursa hii kiurahisi kwa kuwa haitatolewa kwa mtu mmoja mmoja.

Aidha aliwahakikishia wakulima watakaojiunga na mpango huu kupata huduma bora zaidi kutoka kwenye mtandao mpana wa vituo vya kutolea huduma ambavyo viko nchi nzima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kitendo cha kusaini mkataba huo wa ushirikiano utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wananchi katika kujiunga na Bima ya Afya bila ya kuwa na kikwazo cha fedha za kujiunga.

“Tutamlipia mkulima mchango wa bima ya afya wa mwaka Shilingi 76,800 ambayo inamuwezesha kupata huduma yeye mwenyewe na kwa watoto chini ya umri wa miaka 18 tutamlipia Shilingi 50,400. Aidha, unaweza kulipiwa mchango wa Shilingi 355,200 utakaonufaisha mkulima na mwenza wake na watoto wake wanne kwa mwaka.

” Ukiwa na Afya nzuri utaweza kupanga mipango yako vizuri na utashiriki shughuli za maendeleo hivyo hii ni fursa kwa wakulima kuwa na Bima ya Afya kwa uwezeshaji huu usiokuwa na riba,” alisema Bw. Nsekela.

Akizungumzia taratibu za upatikanaji wa huduma hiyo ya Ushirika Afya alisema huduma hiyo itatolewa kwa wakulima walio katika vyama vya ushirika pamoja na wategemezi wao. “Katika makubaliano yetu, CRDB tutalipia michango ya bima ya afya na wakulima watarejesha fedha hizo wakati wa msimu wa mauzo,” alisema.

Mkataba huo pia umesainiwa mbele ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege ambaye alisema kuwa suala la kuwawezesha wakulima kupata Bima ya Afya ni la msingi sana kwa kuwa litasaidia wakulima wengi kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.

“Tunawaomba wananchi ambao ni wakulima kuwa ndani ya vyama vya msingi ili muweze kufikiwa na kupata huduma ya Bima ya Afya na niwahimize viongozi wa Vyama vya Ushirika kuweka kwenye mipango yenu suala la Bima ya Afya, ” alisema Mrajis Ndiege.

Alihitimisha kwa kusema kuwa mpango wa Ushirika Afya umeongeza dhamani ya mwanaushirika kwa sababu inampa fursa ya kupata bima ya afya na kuwa na uhakika wa matibabu.

Previous articleRAIS SAMIA AHUTUBIA MABUNGE MAWILI YA KENYA ( BUNGE LA KENYA NA BUNGE LA SENETI) JIJINI NAIROBI
Next articleRAIS WA ZANZIBAR ALHAJ DK.HUSSEIN ALI MWINYI AMEJUMUIKA NA WANANCHI WA MKOA WA KASKAZINI PEMBA KATIKA FUTARI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here