Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan akimkabidhi vipeperushi Muuguzi Mfawidhi, Bwana Stanley Mahundo wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Dodoma leo (Mei 12, 2021). Katika hafla hiyo Tume ilikabidhi vitu vingine mbalimbali vyenye jumla ya thamani ya TZS 160,000.
Keki iliyoandaliwa na THBUB kwa ajili ya wauguzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Dodoma yenye ujembe wa Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, 2021 usemao: “Wauguzi ni sauti inayoongoza dira ya huduma ya afya.”
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa Dodoma mara baada ya kukabidhi keki. Keki hiyo ilitolewa kama ishara ya kutambua na kuwashukuru Wauguzi nchini kwa mchango wao wa kutetea haki ya kuishi ya wananchi hapa nchi.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan akikabidhi moja ya cartons za maji ya kunywa kwa Muuguzi Mfawidhi Hosptiali ya Rufaa Dodoma, Bwana Stanley Mahundo wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Dodoma leo (Mei 12, 2021).
Mhe. Dkt. Fatma Khalfan akikabidhi moja ya mifuko ya sabuni ya kufulia kwa Muuguzi Mfawidhi Hosptiali ya Rufaa Dodoma, Bwana Stanley Mahundo leo (Mei 12, 2021).
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wauguzi wa Hosptali ya Rufaa Dodoma leo (Mei 12, 2021). Wengine (waliokaa) kutoka kulia ni Muuguzi Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Dodoma, Bwana Stanley Mahundo na msaidizi wake, Bi. Patricia Kabendera. (Picha zote na Suzan Ndashuka)
DODOMA.
Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema kuwa changamoto zinazowakabili wauguzi hapa Nchini zinaweza kuondoshwa kwa wadau wote ndani na nje ya nchi kushirikiana kwa pamoja na kudhamiria kuziondosha.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati wa kuwapongeza wauguzi katika maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani inayoadhimishwa tarehe 12 mwezi Mei kila mwaka.
Jaji Mwaimu amesema kuwa Pamoja na umuhimu wa kada hiyo hapa nchini bado kuna changamoto nyingi zinazoikabili kada hiyo ikiwemo uchache wa wauguzi, kutukanwa, kukashifiwa na mara nyingine kupigwa na ndugu wa wagonjwa wanaowahudumia, uhaba wa vifaa na vitendea kazi, msongamano wa wagonjwa kwenye vituo vya afya, na uhaba wa fursa za kujiendeleza kielimu.
Ameongeza kuwa kwa upande mwingine utendaji wa kazi zao unaathiriwa na ongezeko la uvunjwaji wa maadili ya kitaaluma kwani vipo visa na malalamiko dhidi ya baadhi ya wauguzi ikiwemo rushwa, kuvujisha siri za wagonjwa na matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa.
“Tunapoadhimisha siku hii muhimu, Tume inapenda kutoa wito ufuatao kwa wadau na Serikali iendelee kuwekeza zaidi katika tasnia ya uuguzi ili wapatikane wauguzi wengi zaidi ili kupunguza nakisi ya wauguzi nchini na kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwaendeleza wauguzi kitaaluma” Amesema Jaji Mwaimu.
Aidha ameongeza kuwa “Serikali iendelee kuweka mazingira bora na salama ya kufanyia kazi, ikiwemo kuboresha maslahi ya wauguzna wazingatie maadili ya kitaaluma na kuwajibika licha ya changamoto zinazowakabili” Amesisitiza.
Amewataka Wauguzi na watendaji wengine katika sekta ya Afya wahakikishe kuwa haki za binadamu zinazingatiwa katika utoaji wa huduma za Afya na watambue kuwa kila mtu anayo haki ya kupata huduma ya Afya bila kujali jinsia, kabila na nafasi yake katika jamii.
Pia amewasihi wananchi wajiepushe na vitendo vinavyoweza kuwavunja moyo wauguzi na watoa huduma ya Afya, ikiwemo lugha chafu na kujichukulia sheria mkononi.
Siku ya Wauguzi Duniani uadhimishwa Mei 12 kila mwaka ambapo ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu ni “Wauguzi sauti inayoongoza, Dira ya huduma ya afya”