Home LOCAL RC KUNENGE AZINDUA KAMPENI YA “USIPIME NGUVU YA MAJi”.

RC KUNENGE AZINDUA KAMPENI YA “USIPIME NGUVU YA MAJi”.

DAR ES SALAAM.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Kunenge  amezindua kampeni ya “Usipime Nguvu ya Maji” leo tarehe 03 Mei,2021 kwa kuwataka wananchi wa Mkoa huo kuchukua tahadhari ya Mafuriko ya Maji yaendayo kasi.

Akiongea  na Wahariri wa Vyombo Mbalimbali vya Habari Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema Kufuatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) juu ya uwepo wa mvua za Vuli ambazo tayari zimeanza kunyesha na tayari athari za mvua hizo zimeanza kuonekana wananchi wote wanapaswa kuacha kuyajaribu maji yanayotembea ili waweze kuwa salama wao pamoja na Mali zao

Mhe. Kunenge amesema katika kufuatilia madhara na vifo vinavyotokana na mafuriko, utafiti umeonyesha kuwa zaidi ya Asilimia sabini na tatu ya watu waliopoteza maisha ni kwa sababu ya kujaribu kuvuka maji kwa miguu au kwa kutumia vyombo vya usafiri Kama vile bajaji, pikipiki au magari na hatimaye kusombwa na maji.

Amesema kuwa Maji ya mvua wakati wote yanakuwa na nguvu na kasi ambayo huwezi kuiona kwa macho hivyo amewataka Wananchi kutokudharau maji ambayo hawajui Kina chake,nguvu na kasi yake.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unazindua kampeni hii ili kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuacha kuyajaribu maji yanayotembea kwani yanaweza kuwa na Mambo mengi ndani yake sambamba na ukubwa wa kina chake.

Ili kufikisha kampeni hii kwa wananchi wote Mhe. Kunenge ametoa Rai kwa Vyombo vyote vya Habari, Blogs, Mitandao ya Kijamii, na Wenye Mabango ya Kielektroniki kusaidia kusambaza ujumbe huu kwa watu wote na kwa haraka.

Aidha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imeweka ujumbe huu kwenye Tovuti yake ya www.dsm.go.tz sambamba na kuwapatia “Flash sticks” wahariri waliofika kwenye Mkutano huo.

Mkoa unaendelea kuwaelekeza wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam,hususani wanaoishi katika maeneo ambayo yanakumbwa na mafuriko mara kwa Mara kuendelea kujihadhari kwa kuhamia maeneo salama zaidi.

 Aidha, wananchi wote wanatahadharishwa kutovuka maji ambayo yanatembea kwa kasi kipindi cha mvua kwani yanaweza kusababisha athari mbaya ikiwa ni pamoja na kifo.

Serikali kwa upande wake imekuwa ikijenga Kingo za mito mbalimbali, kujenga madaraja na kujenga Barabara mbalimbali ili kuondoa mafuriko katika Mkoa huu. Alisema Mhe. Kunenge.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here