Na: Mwandishi WHUSM, DAR ES SALAAM.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kufanya kongamano la siku tatu la ukombozi wa Bara la Afrika kuanzia Mei 21 mpaka Mei 23 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu wa kongamano hilo Bwana Boniface Kadili amesema kuwa kongamano hilo la siku tatu lina lengo la kufundisha vizazi vya sasa juu ya ushiriki wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
“Lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ukombozi wa bara la Afrika hasa ushiriki wa nchi yetu katika ukombozi wa nchi mbalimbali hususani nchi za kusini mwa Afrika,” alisema Bwana Boniface.
Aidha aliongeza kuwa katika kongamano kutakuwa na kikao kazi kitakacho husisha Sekta ya Michezo na Sekta ya Utamaduni ambapo maafisa Utamaduni na maafisa Michezo watapata fursa ya kujadiliana changamoto mbalimbali zinazozikabili sekta hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amesema kuwa katika kikao kazi hicho ambacho kitawakutanisha Maafisa Michezo toka Halmashauri zote nchini pamoja na baadhi ya wadau wa Michezo kitakuwa ni fursa pekee ya kujadili changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya Michezo nchini.
“Katika kikao kazi hicho ndiyo wakati muafaka wa kujadiliana kuhusu changamoto zinazo ikabili sekta ya mchezo ikiwemo miundombinu ya michezo pamoja na usimamizi wa Michezo kuanzia ngazi ya shule ya msingi,” alisema Mkurugenzi Singo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni, Dkt. Emanuel Temu amesema kuwa katika kongamano hilo watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya Utamaduni Duniani pamoja na kuangalia changamoto mbalimbali zinazoihusu sekta ya Utamaduni nchini.
“Katika kongamano wadau wa Utamaduni watapata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali yanayoikabili sekta ya Utamaduni kwani kwa sasa misingi ya Utamaduni inapotea hivyo ni fursa pekee ya kukumbushana masuala ya tamaduni zetu ili tuweze kurithisha vizazi vijavyo,” alisema Dkt. Temu.
Kongamano hilo litajumuisha wadau mbalimbali nchini wakiwemo wazee walioshiriki katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika pamoja na wanazuoni na wanafunzi wa shule za msingi mpaka vyuo vikuu.