Home LOCAL HEDHI SIO UGONJWA WALA LAANA – Waziri Gwajima

HEDHI SIO UGONJWA WALA LAANA – Waziri Gwajima

DODOMA.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hedhi wanayopata wanawake sio ugonjwa wala laana bali ni uumbaji wa Mungu katika kumkamilisha mwanamke.

Waziri Gwajima amesema hayo leo katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu siku ya hedhi ambayo inaadhimishwa kila mwaka duniani kote kila ifikapo tarehe 28 mwezi Mei ambayo mwaka huu ina kaulimbiu inayosema “Ni wakati wa kuchukua hatua ili kuhakikisha vifaa vya kujisitiri/taulo za hedhi zinapatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa msichana/mwanamke”.

“Siku ya hedhi duniani inaadhimishwa kila mwaka, licha ya mwaka jana kutofanyika kutokana na changamoto ya Covid 19 lakini jumuiya ya Kimataifa imeendelea kufahamishana, kuelimishana na kukumbushana juu ya jambo hili muhimu kwa njia ya mtandao. Lengo kuu ni kueleza Dunia na Umma wa Tanzania kuwa hedhi sio ugonjwa wala laana bali ni hali ya kawaida na Baraka ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu inayomtokea msichana mara baada ya kuvunja ungo kama ishara ya mabadiliko kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi”. Amesema Waziri Gwajima.

Waziri huyo ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kila siku wanawake zaidi ya milioni 12 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wanakuwa kwenye Hedhi duniani.

Aidha, Waziri Gwajima amesisitiza Hedhi Salama akimaanisha kwamba msichana au mwanamke anapokuwa katika siku zake anatakiwa kuzingatia mazingira salama na anapata huduma zote muhimu ikiwemo miundombinu ya vyoo vyenye usiri, maji safi, taulo za kike au vifaa salama vya kujisitiri na utupaji salama wa vifaa/taulo za kike zilizotumika.

Hata hivyo, Waziri amesema kuna baadhi ya wasichana au wanawake wanakua katika mazingira ya kutokua na hedhi salama ambayo inachangiwa na miundombinu duni ya vyoo, kukosekana kwa maji safi na salama, matumizi ya vifaa vya hedhi visivyo salama na utupaji ovyo wa vifaa vilivyotumika.

“Matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na OR -TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau wa Hedhi Salama mwaka 2019, yanaonesha Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya ajenda ya afya ya hedhi. Hata hivyo, changamoto ni nyingi katika ngazi ya jamii hususan kuwa na uelewa mdogo wa jamii juu ya hedhi salama. Kwa mfano ni asilimia 28 tu ya wasichana ndiyo wenye uelewa thabiti juu ya hedhi salama”. Ameongeza Waziri Gwajima.

Takwimu zinaonesha kuwa maeneo mengi hapa Nchini jamii inakosa uelewa wa umuhimu wa hedhi salama. Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kuonesha ukosefu wa uelewa wa hedhi salama ni pamoja na Halmashauri za Namtumbo, Muleba, Mbeya, Igunga, Temeke, Karatu, Tandahimba, Rorya, Kusini Unguja na Kaskazini Pemba ambayo jamii yake ilionekana inauelewa mdogo juu ya suala la hedhi salama. Huku utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ukionesha kuwa asilimia 60 ya wasichana walionekana kutomudu gharama za taulo za kike.

Hata hivyo, Waziri Gwajima amewashukuru wadau kupitia mtandao wa hedhi salama kuendelea kuhamasisha upatikanaji wa vifaa vya hedhi salama ndani ya nchi kwa unafuu na ubora unaotakiwa ili kila mhitaji kwa makundi yote aweze kutumia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here