Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na zoezi la kutoa elimu kwa wateja wake wa Jiji la Dar es Salaam na miji ya Pwani juu ya mabadiliko ya usomaji wa mita za maji na upokeaji wa bili za maji uliofanywa
hivi karibuni.
Hatua hiyo inatokana na mabadiliko ya usomaji wa mita yaliyofanywa na Mamlaka kutoka tarehe 1 hadi 15 kwenda tarehe 20 hadi 30 ya kila mwezi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juu ya mabadiliko hayo, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya mikoa ya Pwani wamepongeza mabadiliko hayo na kusema yamefanyika wakati muafaka na yataleta tija kwa Mamlaka na Wananchi kwa ujumla.
“Tunaishukuru DAWASA kwa mabadiliko haya ya usomaji mita kwa tarehe za mwisho wa mwezi, sisi wananchi tulishasema sana kuhusu kuletewa bili tarehe tofauti tofauti wakati vipato vyetu vinatofautiana” alisema ndugu Ramadhan Abdul mkazi wa Kinondoni Shamba.
Zakia Mrisho mkazi wa kitongoji cha Sanze, wikaya ya Kisarawe anasema mabadiliko hayo yamewasaidia sana wananchi wanaotegemea vipato vyao mwisho wa mwezi.
“mfano sisi watumishi wa umma kipato chetu kikuu ni mshahara unalipwa mwisho wa mwezi, vile DAWASA walikuwa wanatusomea bili na kutuma message muda wowote halikuwa jambo zuri, tuliishia kugombana nao na wakati mwingine kuleteana vitisho mbalimbali. Lakini kwa mabadiliko haya tunajua wamesikia kilio chetu na wakaamua kujirekebisha” alisema bi Zakia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara na huduma kwa wateja DAWASA, Bi
Rithamary Lwabulinda amesema mabadiliko hayo yaliyofanywa na Mamlaka
yalifanyiwa utafiti wa kina na shirikishi yaliyolenga kuboresha huduma za
majisafi na usafi wa mazingira.
“Mara kwa mara huwa tunatenga muda wa kuongea na wateja wetu,hivyo mabadiliko haya ni miongoni mwa sauti za wateja wetu walizotushauri juu ya uboreshaji wa huduma zetu ili kuweza kuwafikia wengi zaidi” alisema Bibi Lwabulinda