Mwenyekiti wa TPSF Angelina Ngalula akizungumza wakati wa mkutano wa mwezi ulioandaliwa na TWCC Jijini Dar es Salaam. |
Mwenyekiti wa TWCC Taifa Mercy Silla akizungumza mbele ya wanachama wa chama hicho (hawapo pichani) wakati wa mkutano huo Mei 29,2021 Jijini Dar es Salaam. |
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula amewataka wafanyabiashara na Wajasiriamali kuacha kufanya biashara ya aina moja kwa muda mrefu ambazo kwa namna moja ama nyingine haziwafanyi kukua kibiashara na badala yake kutafuta fursa ya kufanya biashara zaidi ya moja ili kuweza kukuza mitaji yao.
Ngalula ameyasema hayo katika mkutano wa wafanyabiashara ulioandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) unaofanyika kila mwezi kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara wanawake ili kujifunza mambo mbalimbali ya kibiashara na fursa zinazopatikana kwenye chama hicho.
Amewataka wajasiriamali na wafanyabiashara kutafuta fursa za kuweza kuanzisha biashara zenye mtaji mdogo zinazoendana na hali halisi ya kiuchumi ili kuweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
“Ndugu zangu wafanyabiashara msikubali kung’ang’ania biashara moja huku unaona kuwa haitoki utakuta mjasiriamali ameshikiria biashara hiyo hiyo kwa miaka mingi kila maonesho unamkuta nayo hiyo hiyo huku akilalamika kuwa biashara ngumu, ni vizuri kujaribisha biashara nyingine ambayo unaona unaweza ukauza na maisha yakaenda” amesisitiza Ngalula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC Taifa Mercy Silla amesema kuwa mkutano huo una lengo la kutoa fursa kwa wanachama wao kuweza kujifunza namna ambavyo wanaweza kukuza mitaji yao na kutanua wigo wa biashara zao ambapo wadau mbalimbali kutoka kwenye sekta tofauti yakiwemo Mabenki hualikwa ili kuweza kuzungumza na wafanyabiashara hao kwa kueleza fursa wanazozitoa katika kuhakikisha wanaendeleza na kukuza mitaji yao.
“Mara nyingi kwenye vikao vyetu hivi vya Breakfast Meeting huwa tunatoa fursa kwa wanachama wetu kuweza kujua vitu mbalimbali kutoka kwa wadau ambao huwa tunawaalika kuweza kushiriki na kueleza fursa zilizopo lakini pia huwa tunawakumbusha kuwa pia Serikalini kuna fursa ambazo wamezitoa kwaajili ya wajasiriamali katika halmashauri na mimi nimewaambia hapa ukienda utakuta wanawake wamepewa fursa ukienda kwa vijana kuna wanawake, ukienda kwa walemavu kuna wanawake, kwa hiyo wanawake ni jeshi kubwa na pia tuna uwezo.” Amesma Mercy.