Home WANANCHI WATOA USHIRIKIANO MKUBWA KWA MAKARANI KATIKA ZOEZI LA SENSA TUNDURU

WANANCHI WATOA USHIRIKIANO MKUBWA KWA MAKARANI KATIKA ZOEZI LA SENSA TUNDURU

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Wakili Julius Mtatiro kulia,akiwapokea makarani  na wasimamizi wa mahudhui wakati walipofika kwa ajili ya zoezi la sensa ya watu  na makazi lililoanza leo nchini kote.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru  ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la usalama la wilaya hiyo Julius Mtatiro kushoto akitoa taarifa za kaya yake kwa karani wa sensa Jafari Matewele.

karani wa sensa Jafari Matewele kulia, akijaza taarifa mbalimbali alipofika nyumbani kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro mapema leo asubuhi.

Na: Muhidin Amri, Tunduru

BAADHI ya wananchi waliokuwa wanasafiri kutoka wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuelekea maeneo mbalimbali ya nchi,wameipongeza Serikali kwa namna ilivyoratibu vizuri zoezi la sensa ya watu na makazi iliyoanza leo nchini kote.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao waliokutwa wakihesabiwa katika kituo kikuu cha mabasi mjini Tunduru walisema,sensa ya mwaka huu itafanikiwa kutokana na hamasa kubwa iliyofanywa na Serikali ambapo wananchi wengi wamepata uelewa umuhimu ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Ali Mnonjela,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwekeza nguvu kubwa ili kufanikisha zoezi hilo muhimu  na kuwaomba wananchi ambao bado hawajahesabiwa kujiandaa na kutoa ushirikiano kwa makarani walipoewa dhamana ya kutekeleza zoezi hilo.

“Mimi nimehesabiwa hapa kituo cha mabasi wakati najiandaa kwenda  Dar es slaam,utaratibu huu haujawahi kufanyika kabisa kwa miaka ya nyuma,naiomba serikali yetu iendelee kusimamia mipango mingine  ya maendeleo kama ilivyofanya kwenye zoezi hili”alisema.

Naye Hidaya Hausi,ameipongeza serikali kwa kuwajali watu wenye dharura wakiwamo wasafiri kwa kuwapatia nafasi ya kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi la mwaka 2022.

Hidaya,ameishauri Serikali  kuongeza muda ili  zoezi hilo lifanyike zaidi ya wiki moja  kwa ajili ya kutoa nafasi kwa  wananchi wenye changamoto na dharura mbalimbali wapate nafasi ya kushiriki na kupata haki yao ya msingi.

Naye mkazi wa kijiji cha Majimaji wilayani humo Swalehe Kalonga alisema, sensa ya mwaka huu imefanyika kisomi zaidi na amependa namna makarani walivyojipanga katika kuuliza maswali ya msingi yanayohusu kaya zao,hali ya kipato,ulemavu na elimu na  tofauti  na miaka ya nyuma ambapo maswali yalikuwa machache na hayakuwapa nafasi kubwa  wananchi kutoa taarifa zao muhimu.

Msimamizi wa sensa ya watu na makazi wa wilaya ya Tunduru Enock Kabakaki ambaye aliambatana na  baadhi ya makarani alisema, zoezi limekwenda kama lilivyopangwa na kuwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa makarani watakaopita katika maeneo yao.

Alisema,zoezi hilo limeanza usiku wa saa 6 na dakika 1 kwa kupita katika maeneo yote yanayohitaji kujaza dodoso maaluma kama vile vituo vya mabasi,nyumba za kulala wageni na maeneo wanayoishi watu wasio na makazi maalum.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro alisema, kwa ujumla  zoezi la sensa katika wilaya hiyo limeanza vizuri ambapo kazi kubwa imefanyika kwa makarani kupitia katika maeneo  mbalimbali ikiwamo nyumba za kulala wageni.

Alisema,makarani 1,392 ambao wamesambazwa katika vitongoji vyote 1,175 na tangu asubuhi zoezi lililopoanza  hadi sasa  hakuna changamoto yoyote  iliyojitokeza na kuwataka wananchi ambao bado hawajahesabiwa kujiandaa kushiriki na kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo.

Alisema,wananchi katika vijiji mbali mbali wanatambua kwamba wana jambo lao na haliwezi kufanikiwa kama hawatajitokeza kwa wingi  kuhesabiwa  kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi linalofanyika mwaka huu.